Saturday, 18 December 2010

Majambazi wateka vituo vya mafuta, waua


Imeandikwa na Shangwe Thani, Shinyanga;
WATU sita wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za kivita jana jioni walivamia vituo viwili vya mafuta mjini hapa na kuua mtu mmoja wakati wakiwa katika harakati za kufanikisha uporaji wa fedha katika eneo la Nyihogo wilayani Kahama, hapa.

Kamanda wa polisi mkoani hapa Daudi Siasi amethibitisha kutokea kwa tukio holo akisema lilitokea majira ya saa 12 za jioni, wakati hao waliokuwa na bunduki moja aina ya SMG na mabomu ya kutupa kwa mkono yalipokivamia kituo cha mafuta cha Lake Oil baada ya kufyatua risasi kadhaa na kufanikiwa kupora pesa kikubwa cha fedha ambacho hata hivyo kiasi chake hakikuweza kufahamika.

Katika uvamizi huo, walimjeruhi begani mtumishi wa kituo hicho, Fatum Hamadi (22) na kumwamuru Abeid Joram (28) atoe pesa ambazo walifanikiwa kumpora na baada ya uvamizi wa kituo hicho wavamizi hao walikimbilia kwenye kituo kingine cha GBP.

Wakiwa kwenye kituo hicho cha GBP walimwamuru mtumishi wa kituo hicho, Ibrahim Magembe (35) kuwakabidhi fedha zote za mauzo ya mafuta na kufanikiwa kupora kiasi cha fedha ambazo idadi yake pia haijafahamika.

Kutokana na matukio hayo, polisi waliarifiwa kuhusu uvamizi wa majambazi hao na walipofika eneo la tukio walianza kuurushiana risasi na majambazi na katika majibizano hayo, mtu mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Marco Jumanne (19) mkazi wa kijiji cha Lugela, wilayani Kahama alipigwa risasi ya kichwa na kufa papo hapo.

Kamanda Siasi alisema, watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika matukio hayo na kwamba polisi wanaendelea na upelelezi wa uvamizi huo.

No comments:

Post a Comment