Kheri yote inapatikana pale Mwenyezi Mungu anaporidhika na mja wake, na funguo za kheri zimo katika Dua pamoja na unyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu na kuonesha kumpenda kwa kutenda yale yanayomridhisha na pia kumuogopa kwa kuepukana na makatazo yake. Mja anapokabidhiwa na Mola wake funguo hizi basi ajue kuwa Mola wake anamtakia kheri, na anaponyimwa basi ajue kuwa amefungiwa milango ya kheri
Saturday, 18 December 2010
Noti mpya kuanza kutumika Januari
ILI kulinda uhalali wa fedha zake pamoja na kuzuia uchavu wa haraka wa noti za Tanzania, Benki Kuu nchini (BoT), imezindua noti mpya zitakazoingizwa kwenye mzunguko wa fedha mwanzoni mwa Januari mwakani, ili zitumike sambamba na zile zinazotumiwa kwa sasa.
Akizindua noti hizo za shilingi 10,000, 5,000, 2,000, 1,000 na 500 makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam jana jioni, Gavana wa BoT, Prof. Beno Ndulu alisema, tofauti na za awali, noti hizo zina alama mpya tatu zitakazolinda usalama wa fedha hizo dhidi ya wataalamu wa kughushi wanaoongezeka kwa kasi kutokana na mabadiliko makubwa ya teknolojia duniani.
Alizitaja alama hizo kuwa ni pamoja na ile iliyojificha ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere inayochukua nafasi ya ile ya twiga katika noti za viwango vyote, alama mpya kiteknolojia inayotembeatembea wakati noti husika inapogeuzwa, na ile inayobadilika au kugeuka rangi.
Kadhalika, alisema, mbali na kupunguzwa ukubwa, noti hizo zitatambuliwa kirahisi na walemavu wa macho kutokana na alama maalumu zilizowekwa kwa ajili yao katika kila kiwango.
Alama hizo ni pamoja na mistari iliyovimba, pamoja na ile ya V ambazo zimewekwa kwa idadi maalumu inayoelezea kila kiwango cha noti husika.
Mabadiliko mengine yamefanywa katika picha za wanyama nyati, tembo na simba ambazo zilitumika zikiwaonesha wakiwa na viwiliwili vyao, ambapo katika noti mpya, picha zinazoonekana ni za vichwa vya wanyama hao pekee.
Vilevile, noti hizo ambazo kwa maelezo ya Ndulu, zimetengenezwa kwa karatasi zinazotokana na pamba kwa asilimia mia moja, zimeongezwa ubora wa hali ya juu kwenye kingo zake ili kuzuia zisikunjike hovyo na kusababisha kuchanika.
Ndulu alisema, licha ya gharama ya kutengeneza noti mpya kushuka kwa asilimia kadhaa, ubora wa noti hizo umezidi kupanda na kukaribia wa dola za Marekani kwa kuwa karatasi zilizotumika kutengeneza za Tanzania ni sawa na zinazotumika kutengeneza baadhi ya viwango vya dola hiyo.
Sababu za kutolewa kwa noti mpya zimeelezwa kuwa ni kuziba pengo la mahitaji ya noti linalotokana na kuchakaa kwa zilizopo kwenye mzunguko, kukidhi mahitaji yanayotokana na mabadiliko ya kiuchumi na ongezeko la watu pamoja na kuboresha uimara na mvuto wa noti hizo.
Kabla ya mabadiliko ya sasa, BoT imekwishabadilisha noti mara saba, mara ya mwisho ikiwa mwaka 2003.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment