Imeandikwa na Lucy Lyatuu na Maulid Ahmed, Kilwa;
WAKATI Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ikiamuru wafanyakazi takribani 5,000 wa Tanesco kulipa viwango sawa vya bei za umeme kama ilivyo kwa wananchi wengine, na ikiridhia kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari mosi, mgawo wa umeme unaanza tena leo.
Mgawo wa umeme uliositishwa wiki moja iliyopita, umetangazwa jana mjini Kilwa mkoani Lindi ikiwa ni kutokana na Kampuni ya Pan African Energy inayozalisha gesi asili katika kisiwa cha Songosongo kupunguza uzalishaji kwa ajili ya kufanyia matengenezo kisima kimoja kati ya vitano ilivyonavyo.
Mahitaji ya matengenezo ya kisima hicho yaligundulika Septemba mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema Tanesco imelazimika kuanza tena mgawo tena kutokana na upungufu wa megawati 40, akisema “tunalazimika kupunguza uzalishaji katika mtambo wa Ubungo ambapo baada ya kuzalisha umeme wa megawati mia moja, sasa tutalazimika kuzalisha megawati 60, na ratiba tutartoa baada ya kuipanga.”
Mramba alitangaza mgawo huo mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakati alipotembea Kilwa Kisiwani kunakozalishwa gesi asilia kwa ajili ya kuiuzia Tanesco na Kampuni ya Songas.
Akitoa taarifa kuhusu kukifanyia matengenezo kisima hicho, Naibu Meneja Mkuu wa Pan African Energy, William Chiume alisema kutokana na matengenezo hayo, watapunguza uzalishaji kwa asilimia 16 kutoka futi za ujazo milioni 86 hadi 76, ambazo ni sawa na megawati 40.
Alisema matengenezo hayo yatachukua kati ya wiki nne na tano kuanzia sasa. Hata hivyo, alisema waathirika wakubwa ni Tanesco, kwani Songas wataendelea kupata gesi kutokana na mkataba walionao. Songas pia wanaiuzia umeme Tanesco.
Songas inaiuzia Tanesco megawati 182 za umeme kwa siku na wakati mitambo ya Tegeta inazalisha megawati 45, Ubungo megawati 100, yote ya gesi asili wakati mahitaji ni megawati 833 kwa siku.
Wakati mgawo huo ukitangazwa Kilwa, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Haruna Masebu alitoa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Ewura wa maombi ya Tanesco ya kubadilishiwa bei za umeme, na kueleza kuwa Bodi imekubali ombi hilo na imepandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari mosi.
Masebu alisema wafanyakazi hao wamekuwa wakilipia viwango maalumu, hivyo Bodi imeamuru walipe kama ambavyo wananchi wengine wanalipia na endapo hawatotekeleza itaonekana wakati wa ukaguzi.
Akifafanua zaidi, Mkurugenzi wa Umeme wa Ewura, Anastas Mbawala alisema wafanyakazi wa Tanesco wanakadiriwa kufikia 5,000 na wamekuwa wakilipa Sh nne kwa kila uniti ya umeme, ingawaje kwa wale ambao ni mke na mume, alikuwa anapewa mmojawapo na sio wote.
Kuhusu bei ya umeme, Masebu alisema maombi ya Tanesco yalitolewa Mei 28, mwaka huu na mchakato ulianza mara moja wa kukutana na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili kwa kina suala hilo ili kila mmoja aridhike na hatua zitakazofuatia.
Masebu alisema mikutano ilifanyika Agosti katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Tabora na Dar es Salaam, na kwamba “baada ya kukutana na wadau mbalimbali na kujadili kwa kina suala la kubadilishiwa bei hizo, Ewura iliona kuna hoja ila hawawezi kukubali maombi hayo kama yalivyoletwa na Tanesco.”
Alisema Tanesco waliomba kuwe na mpangilio wa kubadilisha bei ya umeme kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2011 kwa asilimia 34.6, asilimia 13.8 na asilimia 13.9 ili waboreshe huduma zao na kuwa endelevu wakati wote.
Kadhalika alisema Tanesco waliomba pia mabadiliko hayo yaende pamoja na kuwa na uwezo wa kurekebisha viwango vya umeme wakati wowote, kuruhusiwa kubadilisha bei ya umeme katikati ya kipindi hicho kulingana na mabadiliko ya bei za mafuta na kubadilika kwa viwango vya umeme kadri ya matumizi.
Alisema ni kweli Tanesco wanahitaji zaidi ya Sh bilioni 691 ili itoe huduma endelevu, hivyo Ewura imekubali ombi lao kwa asilimia 18.5 ikiwa ni pungufu ya asilimia 16.1 huku gharama nyingine kutokubaliwa hadi hapo watakapopata mtaalamu mshauri atakayefanyia kazi suala hilo na kuona kama viwango hivyo vinafaa.
Alisema kwa marekebisho hayo, bei ya umeme kwa watumiaji wadogo wanaotumia umeme usiozidi kilowati 50 watalipia Sh 60 kwa kila uniti kutoka Sh 49 za awali huku watumiaji wa kawaida watalipia Sh 157 kutoka Sh 129.
Kuhusu kufungua akaunti maalumu, alisema baada ya kukusanya fedha hizo za viwango vipya, Tanesco wanatakiwa kufungua akaunti ya fedha hizo na kuagiza kuwa zielekezwe katika kazi husika ambapo Ewura watakuwa wakikagua kila baada ya miezi mitatu.
Masebu alisema kutokuwakubalia Tanesco kupandisha umeme wasingekuwa na uwezo wa kujiendeleza na vilevile hatua hiyo inatoa nafasi kwa wawekezaji wengine kujiingiza katika sekta hiyo.
No comments:
Post a Comment