na Bakari Kimwanga |
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimepinga kauli ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ally Hassan Mwinyi, ya kutoona sababu ya mabadiliko ya Katiba na kusema kuwa kufanya hivyo ni kujishushia hadhi mbele ya umma wa Watanzania wapenda mabadiliko ya kweli. Hayo yalisemwa jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa CUF, Amina Mwidau, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kueleza kuwa chama hicho kimeshtushwa na kauli ya Mzee Mwinyi kutokubali wala kuunga mkono mabadiliko hayo ya Katiba mpya. Alisema kitendo cha Mzee Mwinyi, kutounga mkono mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendelea kuidumaza demokrasia ya kweli kwa Watanzania. “CUF hatuamini kuwa upungufu uliyopo kwenye Katiba hiyo yeye hautambui, ila inatudhihirishia wazi kuwa kuna uwezekano wa yeye akiwa Mwenyekiti mstaafu wa CCM kuitumia au hata kushauri vifungu vyenye utata vya Katiba hiyo, kutumika kwa maslahi ya chama chao… hakika hatua hii itaendelea kumvunjia hadhi mbele ya Watanzania,” alisema Mwidau. Alisema CUF inahimiza mabadiliko ya Katiba iwapo Tanzania inataka demokrasia ya kweli. Mwidau, alisema Katiba ya sasa imeipa malamlaka Tume ya Uchaguzi ambayo Rais anayeiteua anaweza kuivunja wakati wowote bila sababu ya msingi huku vyombo vya kisheria kama Mahakama vikiwa havina uwezo wa kuchunguza lolote lililotendwa na tume hiyo ya uchaguzi kwa mujibu wa ibara ya 74. Alisema CUF inaendelea kuwasihi Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama na dini zao, vyama vyote vya siasa, taasisi zote nchini, asasi za kiraia, wanaharakati wa aina zote, kuungana kwa pamoja kudai mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokidhi mahitaji ya Watanzania wote. |
No comments:
Post a Comment