Tuesday, 21 December 2010

Dk Shein Ageuka Mbogo Awaapisha Majaji

Na Zanzibar Yetu




Hatimae Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein jana amewaapisha majaji wanne wa Mahakama Kuu ya Zanzibar katika hafla iliyofanyika Ikulu Mjini Unguja.
Majaji walioapishwa kwa mbwembwe wakiwa wamevalia majokho ni Jaji Abdulahakim Ameir Issa, Jaji Rabia Hussein Mohammed, Mkusa Issac Sepetu na Jaji Fatma Hamid Mahmoud ambaye ni Mwanawe Jaji Mkuu Zanzibar Hamid Mahmoud.
Dk Shein aliteuwa majaji wanne wa mahakama kuu tokea Novemba 29 mwezi uliopita ambapo siku ya pili Chama Cha Mawakili Zanzibar (ZSL) kilipinga uteuzi wa majaji hao kwa madai ya majaji wateule kutoksa sifa za kutosha za kuwa majaji wa mahakama kuu..
Awali Dk Shein alisita kuwaapisha majaji hao ikielezwa akisubiri uchauri kutoka kwa wataalamu mbali mbali wa sheria kufuatia utata wa kisheria pamoja na uzito wa barua aliopelekewa na ZLS iliyoeleza kwamba majaji hao bado hawajaiva kitaaluma katika fani ya sheria na kwa mujibu wa sheria tume ya utumishi ilipaswa kukaa kuidhinisha majina hayo jambo ambalo halikufanywa kwa baadhi ya majaji walioteuliwa.
Baadhi ya mawakilishi wakiongozwa na rais wa Chama Cha Mawakili Zanzibar, Yahya Khamis Hamad waliosaini barua ya kumpinga Dk Shein juu ya uteuzi wa majaji hao ambao kwa mujibu wa maelezo yao hawana sifa zinazowafanya wawe majaji wa mahakama kuu.
Rais wa Zanzibar kwa mamlaka aliyopewa alifanya uteuzi wa majaji wanne wa Mahkama Kuu pamoja na Mwenyekiti wa Mahkama ya Ardhi ambaye ni Haroub Sheikh Pandu, na majaji wanne wa mahakama kuu akiwemo Abdul-hakim Ameir Issa, Fatma Hamid Mahmoud, Mkusa Isaac Sepetu, na Rabia Hussein Mohammed.
Chama hicho kilisema uteuzi huo, ulikuwa unatumia mamlaka aliyopewa rais na Katiba ya Zanzibar, 1984 kifungu cha 94(2) na (3) ambapo Chama cha Mawakili hakina mashaka na uteuzi wa Abdul-hakim Ameir Issa, wala uteuzi wa Mwenyekiti wa Mahkama ya Ardhi, Haroub Shehe Pandu isipokuwa mashaka yapo kwa Fatma ambaye ni mtoto wake Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mkusa Isaac Sepetu na Rabia Hussein Mohammed ambao wote watatu wanadaiwa kutokuwa na sifa zinazostahiki kuteuliwa nafasi hiyo.
Aidha chama hicho kimesema kwamba Rais binafsi hawezi kuwaelewa majaji wala hakuna sababu ya kumjuwa yeyote katika Majaji wanne aliowateua ila wanachoamini uteuzi wake unatokana na ushauri uliopewa na Tume ya Utumishi ya Mahkama iliyoanzishwa chini ya Sheria Namba 13 ya mwaka 2003 ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid pamoja na wasaidizi wa rais wengine katika sekta ya sheria.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud aliitisha kikao cha tume ya utumishi ambacho anadaiwa kuwa hakikupitisha jina moja la jaji aliyeteuwa na mawakili hao ili wajadiliane lakini kikao hicho kilishindwa kufanyika baada ya kupokea barua nyengine kutoka chama cha mawakilishi kusema kwamba kikao kitakachofanyika hakitokuwa halali kwa mujibu wa sheria kwa kuwa wajumbe wa kikao hicho hawakutimia.
Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na katibu wa chama cha mawakili, Salim Mkonje iliyotumwa kwa rais wa Zanzibar ya Desemba 3 mwaka huu, ambayo tayari saini ya rais inaonesha ameshaipokea ilisema kwamba wakili, Awadh Ali Said ambaye alikuwa mjumbe wa tume ya uajiri anayetokana na chama hicho katika vipindi viwili vimekwisha tokea septemba 17 mwaka huu hivyo hawezi kuwa mjumbe tena hadi hapo atakapoteuliwa tena.
Mbali na mjumbe huyo lakini pia Jaji Mshibe Ali Bakari naye muda wake umekwisha kwa mujibu wa sheria ya tume hiyo No 13 ya mwaka 2003 koramu ni wajumbe watano kifungu cha 9(2).
“Kufutia kikwazo hiki wakili Awadh alifahamishwa na katibu wa tume ya uajiri ya mahakama asihudhurie kikao cha leo 3 Desemba jana usiku” ilisema barua hiyo kutoka kwa mawakili. Na kuongeza kwamba. “kwa sababu wajumbe waliokuwepo walikuwa sita hivyo kupungua kwa wajumbe wawili kunapelekea tume isiweze kufanya maamuzi kama sheria inavyotaka kwani yatakuwa batili kwa kukosekana koram” ilisema barua hiyo.
Aidha chama hicho wiki mbili zilizopita kiliitisha kikao chake kuteuwa jina la wakili ambaye atakiwakilisha chama hicho na kulipeleka kwa rais ili ateuliwe kuingia katika kikao hicho ikiwa pamoja na wajumbe wengine ambao sheria inasema tume hiyo iwe na wajumbe wanane akiwemo jaji mkuu, mwanasheria mkuu, mwenyekiti wa tume ya utumishi, na kadhi mkuu.
Wengine ni wakilishi anayetoka chama cha mawakili, jaji wa mahakama kuu ambaye anaendelea na kazi ya ujaji, jaji mstaafu, na mtu mwengine yeyote ambaye rais atakayeona anafaa .
Hafla ya kuwaapisha majaji hao ilifanyika juzi jioni Ikulu Mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa akiwemo Makamu wa kwanza wa rais Maalim Seif Sharif Hamad, makamu wa pili Baloazi Seif Ali Iddi na Jaji Mkuu Zanzibar, Hamid Mahmoud, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, na mawaziri mbali mbali wa serikali

No comments:

Post a Comment