• Komandoo alisema si mapapai
  • hayataoza kule “Kiinua miguu”
  • Sasa wanadai fidia nje ya Mahakama
Na Mwandishi Wetu
Wale waliodaiwa kuwa ni wahaini waliotaka kupindua serikali ya Komandoo, Dr. Slamin Amour Juma, sasa watakaa meza moja na serikali ya Dr. Shein kujadili uwezekano wa kulipwa fidia.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Mahakama Kuu kuridhia maombi ya wakata rufaa ambao kupitia mawakili wao walitaka shauri lao litoke mahakani ili kutumia fursa ya kuwepo maridhiano wazungumze na serikali.
Wakata rufaa hao wanataka kulipwa fidia kwa vile waliwekwa ndani kwa kile ambacho wanadai kwamba ni madai ya kupika kinyume na sheria.
Kwa madai hayo waliwekwa ndani kwa zaidi ya miaka miwili ambapo baadhi ya watu walipojaribu kuwaombea huruma ya Rais, wakati huo Komandoo Salmin, alidai kuwa hao si mapapai.
“Mwache akae, (yeye) si papai, halitaoza”, alidaiwa kusema Dr. Salmin alipoombwa amwonee huruma mmoja wa watuhumiwa hao ambaye inadaiwa kuwa wana undugu wa damu.
Kauli hiyo ilihitimisha jitihada za wanasiasa na wana ndugu ambao walidhani kwamba hapakuwa na sababu ya msingi ya kuwaweka watuhumiwa ndani, na kwamba hata kama ingekuwepo, Rais angeweza kutumia mamlaka yake kuwaonea huruma.
Kwa jibu hilo la Komandoo Salmin Amour, watuhumiwa wakasota “Kiinua miguu’ pale Kilimani kwa zaidi ya miezi 24.
Hatua ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kuridhia kutoa fursa ya wakata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu ili kufanyike mazungumzo ya kulipwa fidia walioshitakiwa kwa kosa la uhaini na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imefikiwa mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya majaji wa mahakama hiyo E. N. Munuo, E. A. Kileo na Stevin Bwana baada ya mabishano makali ya kisheria kati ya mawakili wa wakata rufaa na wakatiwa rufaa hiyo.
Kabla ya Mahakama Kuu kuitupilia mbali keshi hiyo kwa madai ya kukosekana uthibitisho wa madai ya walalamikaji 18 wa kesi ya uhaini, kila mmoja wao alitaka alipwe fidia ya shilingi millioni 360.
Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Salum Kihiyo Julai 20 mwaka 2009, iliwahusu walalamikaji dhidi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar , Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa SMZ.
Katika shitaka la msingi hapo Novemba 29 mwaka 1997, walalamikaji walidai kuwa walalamikiwa kwa mamlaka yaliokuwa nayo bila ya sababu za msingi walitoa amri ya kukamatwa kwa madai ya uongo ya kula njama kuwapachka kosa kubwa chini ya kifungu cha 355 cha kanuni ya adhabu sura ya 13 ya sheria za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar .
Wakadai kuwa, baina ya Novemba 29 mwaka 1997 na Mei 1998 maafisa hao kwa kufuata amri ya polisi walikawamata walalamikaji 18 kwa mashataka ya uhaini kinyume na kifungu cha 26 kanuni ya adhabu sura ya 13 ya sheria za SMZ.
Katika shauri hilo, Kamishna wa Polisi Zanzibar na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), waliwakilishwa na mawakili, Malata na Pius Mboya kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali (Tanzania) huku Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Zanzibar aliwakilishwa na Fatma Saleh na Said Hassan kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.
Kwa upande wa wakata rufaa waliwakilishwa na mawakili Nassor Khamis na Hamid Mbwezeleni na Salim Mkonji ambao muda wote walitaka shauri hilo lisisikilizwe kama ilivyopangwa kufuatia mabadiliko ya kisiasa yaliyotokea hapa Zanzibar kufuatia kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa.
Katika kuweka mkazo wa hoja hiyo wakili Nassor alisema kanuni ya 2 na ya 106 (19) za mahakama hiyo zinatoa fursa kwa mahakama hiyo iwapo inafaa kutoa uamuzi mwengine kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
“Waheshimiwa majaji kwa hali ya kisiasa ilivyo sasa hapa Zanzibar naomba kesi iakhirishwe ili tufanye mazungumzo na serikali hata kama yote tuliyoomba hayatopatikana ila iwapo hatukuafikiana kesi iendelee”, alisema wakili wa walalamikaji.
Hata hivyo kwa upande wake wakili Mboya alisema pamoja na kupongeza hatua ya kisiasa iliyofikiwa alitaka hukumu ya mahakama kuu izingatiwe na kesi iendelee kusikilizwa na mahakama hiyo ya rufaa.
Wakili Nassor alisema hafikirii kuwa pamoja na kutolewa hukumu na mahakama kuu, hadharani kama itazuwia kufanyika mazungumzo na serikali juu ya malipo ya fidia na hatimaye waiarifu mahakama ya rufaa.
Kutokana na majadiliano hayo makali kutoka kila upande, hatimae Jaji Munuo akaridhia hoja ya kufanyika mazungumzo nje ya mahakama hiyo kwa masharti iwapo hautofikiwa muafaka waendelee kusikiliza kesi hiyo katika mahakama hiyo.
Mazungumzo hayo zaidi yalilenga maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa Novemba 5 mwaka jana kati ya aliyekuwa rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais chini ya mfumo mpya wa serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar.
Miongoni mwa walalamikaji katika shauri hilo wamo mawaziri wawili katika serikali hii mpya ya awamu ya saba ambao ni Juma Duni Haji (Waziri wa Afya) na Hamad Masoud Hamad (Waziri wa Miundo mbinu na Mawasiliano.)
Mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali, ndugu wawili Abass Zam na Ali, Said Zam Ali, Pembe Ame Manja, Mohammed Ali Maalim, na Hamad Mmanga Khalfan.
Walalamikaji wengine ni Ramadhan Shamna Ali, Hamza Makame Omar, Nassor Seif Amour, Sharif Haji Dadi na wanawake wawili akiwemo Zeleikha Ahmed Mohammed na Zena Juma Mohammed
Wengine ni aliyekuwa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohammed, Abdallah Said Abeid, Soud Yussuf Mgeni (marehemu) na Hassan Said Mbarouk (marehemu) waliofariki dunia mwaka jana.
Kesi hiyo ya watu 18 walidaiwa kupanga njama za kufanya uhaini kwa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ilifunguliwa wakati wa utawala wa Dk Salmin Amour Juma (Komandoo) aliyekuwa rais wa Zanzibar na kuendeshwa na mawakilili mbali mbali wa upande wa serikali wakiwepo wale wa kutoka nchini Nigeria.
Annur