Rais Dk Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na kikosi cha Timu ya Kili Stars, Ikulu Dar es sakaam
Timu ya kilimanjaro Stars mabingwa wa michuano ya Kombe la Chalenji
Hatmaye timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ ilitwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Chalenji iliyoukosa kwa miaka 16 baada ya kushinda 1-0 katika mechi yao ya fainali dhidi ya Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.
Nahodha Shadrack Nsajigwa ndiye aliyefunga goli la ushindi kwa njia ya penati katika dakika ya 42 baada ya beki Ng’oran Kouassi kunawa mpira katika eneo la 18 na mwamuzi Bamlack Tessama kutoka Ethiopia kutoa adhabu hiyo.
Huku wakishangiliwa na mashabiki 60,000 waliojazana kwenye uwanja huo, Stars walicheza kwa kasi kuanzia mwanzo wa mchezo, lakini ni wageni ndio walioanza kupeleka hatari langoni mwa Stars wakati Dion Marc alipopiga shuti kali lililodakwa kwa ustadi na kipa Juma Kaseja katika dakika ya saba.
Stars walijibu mapigo kwa shambulizi lililomaliziwa kwa shuti kali na kiungo Jabir Aziz katika dakika ya 17, ambalo hata hivyo lilipanguliwa na kipa Ali Sangare wa Ivory Coast.
Katika dakika ya 26, Ivoru Coasta walipoteza nafasi ya kufunga wakati Kaseja alipowahi kutoka golini lakini mshambuliaji Kone Zoumana akapiga mpira kwa kichwa nje ya lango lililokuwa wazi.
Kaseja ‘alimbania’ goli mshambuliaji Kipre Bolou baada ya kudaka shuti alilopiga dakika moja kabla ya mapumziko.
Stars walipoteza nafasi kadhaa nzuri za kuongeza magoli, zikiwemo za dakika za 57, 67 na ile ya dakika ya 81 wakati walipogongeana pasi safi, mpira ukianzia kwa Henry Joseph, Salum Machaku na Jabir Aziz kuanguka wakati akikaribia kufunga.
Kwa kutwaa ubingwa huo Stars walitwaa zawadi ya kitita cha dola za Marekani30,000 (sawa na Sh. milioni 43) huku Ivory Coast walioshika nafasi ya pili wakipata zawadi ya dola za Marekani 20,000 (Sh. Milioni 29).
Uganda waliotwaa nafasi ya tatu baada ya kushinda 4-3 dhidi ya Ethiopia jana, walikabidhiwa zawadi ya dola za Marekani 10,000 (Sh. milioni 14.5).
Kwa mara ya mwisho, Stars ilitwaa kombe la Chalenji mwaka 1994 wakati michuano hiyo ilipofanyika Nairobi nchini Kenya.
NSAJIGWA, KASEJA
Beki na nahodha wa Stars Shadrack Nsajigwa alitangazwa kuwa mchezaji bora wa michuano huku kipa Juma Kaseja akitwaa tuzo ya kuwa kipa bora na mshambuliaji Felix Sunzu wa Zambia aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga magoli matano.
Kikosi cha Stars
Kaseja, Idrisa/Kigi Makassy (dk 13) Rashid, Nsajigwa, Stephano Mwasika, Juma Nyoso, Kelvin Yondan, Shaaban Nditi, Jabir Aziz, Nurdin Bakari, Salum Machaku na John Bocco.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment