13th December 2010
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe
Wingu zito limetanda kuhusu hatma ya kisiasa ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, baada ya kunusurika kufukuzwa katika nafasi yake ya Unaibu Katibu Mkuu wa chama hicho kufuatia wabunge wenzake wa chama hicho kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Hali hiyo inakuja zikiwa zimepita siku mbili tangu wabunge wa chama hicho wamvue Zitto nafasi ya Naibu Mkuu wa Kambi ya Upinzani bungeni kwa tuhuma za kusaliti maamuzi halali ya chama hicho.
Hata hivyo, jaribio hilo la kumwondoa kwenye nafasi hiyo lilishindikana baada ya Kamati Kuu kumwokoa kwa kukataa kura ya kutokuwa na imani naye badala yake kamati hiyo ikaelekeza asikilizwe kwanza kabla ya kuadhibiwa. Habari kutoka ndani ya chama hicho zilisema kuwa wabunge walitaka kumtosa Zitto kutokana na kutofautiana na msimamo wa chama chake wa kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete Novemba 17, mwaka huu.
Kamati Kuu ya (Chadema) imeunda kamati ya jopo la wazee wa chama chini ya Profesa Mwesiga Baregu kumsikiliza Zitto na matatizo yake na viongozi wengine wa chama ili kuleta suluhu ndani ya chama. Jopo hilo lina wajumbe wanne ambao ni Shida Salum, Kitila Mkumbo ambaye ni Katibu, Profesa Baregu na mjumbe mmoja aliyejulikana kwa jina moja Shilungushela.
Akizungumza na NIPASHE jana, Profera Baregu alikiri kuwa ni kweli amepewa jukumu hilo na Kamati Kuu kwa ajili ya kutafuta amani ndani ya chama hicho hasa kumsuluhisha Zitto na wabunge wenzake.
Alisema tayari wameanza kujipanga kwa ajili ya kuwakutanisha wabunge wa chama hicho na Zitto ili kuweka mambo sawa ingawa hakutaja watakutana lini na wapi.
“Sijui tutakutana lini lakini itakuwa hivi karibuni bado tunajipanga tukutane na Zitto tumsikilize matatizo yake na kazi yetu ni kujenga uhusiano mwema ndani ya chama, tunataka amani itawale, ” alisema Profesa Baregu.
Hata hivyo, Profesa Baregu hakuwa tayari kuzungumzia jaribio la kumfukuza Zitto katika wadhifa wake ndani ya chama hicho na kutaka aulizwe Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa. “Hayo ya Kamati Kuu yanamhusu Katibu Mkuu ndiye anayeweza kuyazungumzia,” alisema Profesa Baregu.
Habari hizo zilisema kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imemtambua Rais Jakaya Kikwete kama Rais halali na kuagiza wabunge kushiriki shughuli zote za kitaifa.
Alipotafutwa kuthibitisha habari hizo, Dk. Slaa, alisema anatarajia kukutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kuelezea yaliyojiri kikao cha Kamati Kuu.
“Kikao chetu kiliisha usiku sana sasa tunaandaa tamko na tutawapa, sijajua kama tutaweza kukutana na ninyi leo au la lakini tutawaarifu,” alisema Dk. Slaa.
Alipotafutwa ili atoe maoni yake, Zitto alisema yeye bado ni mgonjwa na yuko kitandani hivyo hawezi kuzungumza lolote kuhusu masuala hayo ya kisiasa.
"Mimi bado naumwa hivi hapa niko kitandani nyumbani siwezi kuzungumza masuala hayo kwanza sijui chochote kinachoendelea," alisema Zitto.
Sakata la Zitto linafanana na lile la aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambalo lilisababisha kuundwa kwa kamati iliyokuwa ikiongozwa na Rais wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Wajumbe wengine wa kamati hiyo walikuwa ni Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Pius Msekwa. Kamati hiyo ya CCM ilionekana kumlenga moja kwa moja Sitta, ambaye baadhi ya wanachama wa chama hicho walikuwa wakimshutumu kuwa ndiye aliyesababisha mpasuko ndani ya chama hicho.
Jina la Sitta liliondolewa na Kamati Kuu kwenye orodha ya wanaowania nafasi ya Spika na badala yake yalipitishwa majina ya wanawake watatu ambao ni Anne Makinda, Anna Abdallah na Kate Kamba na majina yao yalipopelekwa kwenye Kamati ya Wabunge wa CCM, Anne Makinda aliibuka mshindi wa kiti cha Uspika. Sitta kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment