Saturday, 25 December 2010

Katiba Mpya Haikwepeki-Waziri Samia

Na Salma Said
MJADALA wa kutaka katiba mpya ambao unaendelea kujadailiwa nchi nzima na watu mbali mbali wakiwemo wasomi na wanaharakati unaelezwa kuwa ni haki ya kila mmoja kuujadili.
Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Bwawani Mjini Unguja baada ya kumalizika ziara yake ya siku nne visiwani hapa.
Samia alisema suala la katiba mpya kwa Watanzania ni jambo lisilokwepeka kufanyika na wananchi wanaodai ni ni haki yao kwani wao ndio wanaopaza sauti ya kuidai.
“Kama imefikia hatua ya Watanzania kudai katiba mpya hiyo ni haki yao na ni lazima Serikali ikisikilize kilio chao kwani katiba ipo kwa ajili yao” alisema waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja.
Waziri huyo alisema wimbi la madai ya mabadiliko ya katiba lilionekana kuhitajika zaidi Zanzibar miezi mitatu iliyopita na baada ya marekebisho ya 10 ya katiba ilifanya mabadiliko ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya kumalizika kwa uchaguzi sasa wimbi hilo limehamia upande wa pili wa Tanzania bara.
Alisema kuwapo kwa harakati na wanaharakati wanaodai katiba mpya ya Tanzania ni moja ya haki yao kidemokrasia, kwa kuieleza Serikali hisia zao hasa baada ya kuona umuhimu wa hivi sasa kuwa na katiba mpya.
Serikali itakaa na kusikiliza matakwa ya wananchi kwani suala la katiba kwa sasa ni jambo lisilokwepeka kutokana na mahitaji ya wakati hasa kwa kuzingatia katiba iliyopo ni ya muda mrefu na lazima iwe inakidhi haja kwa wakati husika alisema.
“Madai yanayotolewa na wananchi juu ya suala la mabadiliko ya katiba ni haki yao, na serikali itakaa na kuyaangalia maeneo ambayo itaona inafaa kufanyiwa mabadiliko”,alisema Waziri huyo.
Akizungumzia suala la Muungano ambalo ndilo lililomfanya afanye ziara ya kujitambulisha kwa viongozi wa serikali mpya ya umoja wa kitaifa, alisema wanafanya mapitio kuyaangalia maeneo yote yenye utata kisheria, kikatiba na kiutendaji.
Alisema ingawa changamoto ziliomo katika mambo ya Muungano hazitaisha, lakini zitapatiwa njia muafaka juu ya jinsi ya kukabiliana nazo kwa njia ya mazungumzo ya pande zote mbili kila itapohitajika kufanya hivyo huku serikali zote mbili zikizingatia maoni yaliotolewa kwa pande zote.
Alifahamisha kuwa ingawa Zanzibar hivi sasa imo katika serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini imehakikisha kuwa inadumisha Muungano wa serikali mbili kama ilivyoanzishwa na waasisi wa Muungano huo Marehemu Abeid Karume na Marehemu Mwalimu Nyerere..
Alisema hofu waliyonayo baadhi ya wasomi na wananchi kudai muundo wa serikali ya Zanzibar kuwa na utata katika Katiba ya Tanzania, sio jambo litaloifanya serikali iliopo isiwe na uwezo katika utekelezaji wa shughuli zake kwa mambo yalimo katika katiba ya Muungano.
Waziri huyo alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya mfumo wa serikali ya Umoja wa kitaifa ipo kihalali kikatiba kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar kwa vile wao ndio walioitaka na sio upande wa Muungano hivyo kuna kila sababu ya mfumo huo kuheshimiwa kwa kuwa ni chaguo la wazanzibari.
Alisema jambo linalohitajika ni kuangalia kama kuna vipengele vya Katiba Muungano vinavyoonekana vina utata wa kisheria, kiutendaji na kikatiba kufanyiwa mabadiliko.
Akizungumzia juu kero za Muungano ambazo bado zimeshindwa kutekelezeka licha ya vikao vya Muungano kuzipatia utatuzi likiwemo suala la wafanyabishara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, alisema wizara yake itajitahidi kuondoa matatizo hayo ambayo yanafanywa na watendaji wa TRA.
Alisema anashindwa kufahamu kwanini tatizo hilo liendelee kuwepo kwani Mamlaka ya Mapato Tanzania ni moja ambayo hiyo hiyo inafanyakazi Bara na Zanzibar.
“Mamlaka ya Kodi Tanzania iliopo bara na Zanzibar zina nguvu sawa na viwango vimoja katika kutoza kodi, hatutambui utata unakuwa wapi hata wafanyabiashara watozwe kodi mara mbili”,alisema.
Waziri Samia alisema Wizara yake itaendelea kutoa elimu zaidi juu ya ufahamu mambo ya Muungano, ili kuifanya jamii iwe na uelewa zaidi.
Waziri Samia alizitembelea Wizara mbali mbali za serikali ziliopo chini ya taasisi za Muungano na pamoja na zile ambazo zisizo za Muungano

Kutoka Zanzibar Yetu

No comments:

Post a Comment