| • Kusaini mkataba leo na Dina Ismail |
| BAADA ya mchakako wa muda mrefu wa kusaka kocha, hatimaye klabu ya soka ya Azam imemnasa kocha wa timu Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ Muingereza Stewart Hall na leo anatarajiwa kuingia mkataba wa kuinoa timu hiyo. Hall anamaliza mchakato wa muda mrefu wa klabu hiyo kusaka kocha atakayerithi mikoba ya aliyekuwa kocha wake Mbrazil Itamar Amorin aliyetupiwa virago kutokana na kushindwa kuipatia mafanikio timu hiyo. Habari kutoka ndani ya uongozi wa Azam zinasema kwamba pamoja na kuwepo kwa makocha wengi waliotuma maombi kutoka ndani na nje ya nchi lakini waliachana nao na kuamua kuzungumza na Hall. Kiongozi mmoja wa Azam aliliambia Tanzania Daima kuwa kutua kwa Hall kunafuatia mazungumzo baina yao na Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kabla ya kuridhia kumuachia kocha huyo kwa makubaliano maalum. Alisema, kilichowafanya waridhie ni kutokana na Zanzibar Heroes kutokabiliwa na mashindano katika siku za usoni na kama yatatokea atakwenda kuwasaidia kwani itakuwa ni kwa kipindi kifupi. “Unajua sasa hivi Zanzibar Heroes haina mashindano itakayoshiriki sana ni timu ya Taifa ya Vijana ambapo hata hivyo ZFA imesema anaweza kuwa mshauri wa ufundi,” alisema kiongozi huyo. Aidha, kiongozi huyo aliongeza kuwa pamoja na kocha huyo kutua Azam lakini atashirikiana na ZFA katika kutafuta kocha atakayerithi mikoba yake. |
No comments:
Post a Comment