Sunday, 12 December 2010

MUHAS yamtunuku Rais Kikwete shahada ya heshima




na Hellen Ngoromera





RAIS Jakaya Kikwete jana alitunukiwa shahada ya juu ya heshima ya udaktari wa afya ya jamii na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Kikwete alitunukiwa shahada hiyo na Rais mstaafu wa awamu ya pili ambaye ni mkuu wa chuo hicho, Ali Hassan Mwinyi, kutokana na kutambua mchango wake katika sekta ya afya nchini.
Akizungumza baada ya kutunukiwa shahada hiyo, Rais Kikwete, alisema awali wakati anataarifiwa kuhusu suala hilo hakuamini wala kutegemea.
“Awali wakati napokea taarifa juu ya hili niligwaya na wala sikutegemea, nilijiuliza kwa nini, lakini baadaye nilitambua kuwa naipokea shahada ya heshima kwa niaba ya Watanzania hivyo naipokea kwa heshima tunu hii,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo alisema mafanikio katika sekta ya afya yamefikia mahali pazuri kutokana na juhudi mbalimbali za wadau wa sekta hiyo ambao wamekuwa wakitoa michango mbalimbali pamoja na ushauri.
Aliweka wazi kwamba ataendeleza juhudi alizozianzisha hasa kutilia mkazo uboreshwaji wa sekta ya afya bila kuchoka kwa kuwa hata yeye inamhusu pia.
“Sekta ya afya ni muhimu, hata ukiwa rais utaugua na utakufa,” alisema Rais Kikwete.
Katika mahafali hayo wahitimu 573 kati yao 149 walitunukiwa diploma na 52 diploma za juu katika fani mbalimbali za sayansi shirikishi za afya.
Pia wahitimu 261 walipata shahada ya kwanza na wengine 111 shahada ya uzamili

No comments:

Post a Comment