Dk Shein Apewa Agizo na Wazee wa CCM
WAZEE wa CHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar wamemtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein kuwa muumini na muendelezaji mzuri wa Mapinduzi ya Januari 12, 1984.Wazee hao walieleza matumaini yao kwa Dk. Shein kuwa atakuwa mtendaji bora zaidi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuwa muumini mzuri wa kuendeleza Mapinduzi ya Januari 12 1964. katika ziara yake iliyoanza jana katika mikoa ya Kusini Unguja.
Wazee hao walimpongeza Dk. Shein kwa ushindi alioupata katika uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na wamesema wana matumaini makubwa na baraza la mawaziri alilolichaguwa kuwa litafanya kazi kwa mashirikiano makubwa ili kuleta maendeleo.
Wazee hao hao wamemueleza Dk. Shein katika ziara yake ya kutembelea wilaya kumi za Zanzibar ambapo zira hiyo aliianza jana, Makunduchi Wilaya ya Kusini na hatimae alizungumza huko Dunga Wilaya ya Kati na kueleza madhumuni ya ziara hiyo ikiwa ni kutoa shukurani kwa wananchi na wana CCM kwa kufanya uchaguzi kwa salama na amani sanjari na amani na utulivu.
Dk Shein alifuatana na mkewe Mama Mwanamwema Shein, na kuzungumza na Viongozi wa CCM, Jumuiya za CCM na Wazee wa CCM wa ngazi ya Tawi, Wadi na Jimbo katika ziara ya kutoa shukurani tokea kumalizika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huu.
Wamesema matumaini yao ni kuwa baraza lililoundwa litaweza kufanya kazi vizuri na wananchi wote wamefarijika na Baraza hilo la Mawaziri ambalo linatarajiwa kujenga matumaini makubwa ya kuweza kupata maendeleo zaidi.
Mapema Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mashirikiano makubwa waliompa na hatimae CCM kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi uliopita.
Dk Shein alisema kuwa kuzungumza na wazee ni utamaduni na heshma ya CCM kwa kutambua umuhimu wa wazee ikiwa ni pamoja na kupata busara zao ambapo aliwashukuru wazee hao na kueleza kuwa juhudi zao zimeweza kuzaa matunda na hatimae chama cha CCM kuweza kupata ushindi sanjari na kuendeleza amani na utulivu iliyopo nchini.
Aidha, Dk. Shein aliwahakikishia wazee hao kuwa ataendelea kufanya kazi nao ikiwa ni pamoja na kupokea busara, hekima na ushauri wao ili kuweza kuimarisha chama pamoja na kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitoa wito kwa wazee hao kuendelea kufanya kazi kwa pamoja , kuendeleza mashirikiano kwa lengo la kufuata nyayo za chama cha ASP za umoja na mashirikiano.
Alieleza imani yake kuwa wazee hao wataendelea kushirikiana kwa pamoja ili kukiimarisha chama na kuweza kuwasaidia viongozi wao pamoja na kuweza kuwapa nguvu vijana kufanya kazi zao vizuri.
Dk. Shein aliwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kufanya uchaguzi wa haki, amani na utulivu mkubwa ulioonesha kupevuka kwao kidemokrasia ambao umeipa heshima kubwa Zanzibar Kitaifa na Kimataifa.
Dk. Shein aliwapongeza Wazanzibari wote kwa kushiriki katika uchaguzi kwa amani na utulivu na kueleza kuwa kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kutekeleza ahadi na kuimarisha maendeleo.
Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Saba anayoiongoza yenye mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itafanya kazi vizuri na ataisimamia vyema bila ya hofu katika kutekeleza majukumu yake na atatenda haki kwa Wazanzibari wote bila ya kujali tofauti ya itikadi za kisiasa.
Alieleza kuwa asilimia ya ushindi iliyopatikana katika Mkoa wa Kusini Unguja ni kubwa na imeweza kuthibitisha wazi kuwa Mkoa huo ndio ngome ya CCM.”Hiyo ndio sifa ya CCM ya kuahidi na kufanya” alisema Dk.Shein.
Dk. Shein alieleza kuwa nia ni kuona ahadi zote alizozitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi uliopita zinafanikiwa ikiwa ni pamoja na kupata maendeleo na kuahidi kuwawezesha akina mama kama alivyoahidi wakati wa Kmpeni za uchaguzi na kusema kuwa lengo lipo vile vile la kuanzisha Benki yao ya Wanawake.
Alieleza kuwa aliahidi kutekeleza kampeni kwa ustaarabu yeye na viongozi wenziwe na ndivyo ilivyofanyika hatua ambayo imeipelekea Zanzibar kupata sifa ndani na nje ambayo ilipelekea uchaguzi uwe wa amani na utulivu. Pia Dk. Shein aliwashukuru wananchi wote walioshiriki kwa njia zote katika kufanya kampeni zilizoipa ushindi CCM.
Alisema kuwa Mapinduzi yanabeba umuhimu mkubwa kwa wananchi kwa kuwawezesha kiuchumi, kijamii na kisiasa na kuweza kuimarisha maendeleo katika sekta zote zikiwemo elimu, afya, huduma muhimu ikiwemo maji safi na salama na nyenginezo kazi ambayo itaendelea kuimarishwa.
Dk. Shein alieleza kuwa ahadi yake ya kuimarisha sekta ya michezo na kuwajengea mazingira mazuri wasanii wa vikundi vyote kwa kuwajengea studio ya kisasa lipo pale pale.
Pia, Dk. Shein alitoa wito kwa wanaCCM kushirikiana na kuwa kitu kimoja ili kuweza kukiimarisha Chama na kueleza kuwa ana imani kuwa kundi lililopo hivi sasa ni kundi la CCM.
Alieleza kuwa chama chake kitaendelea kufuata Katiba na Sheria za nchi katika mfumo mzima wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Nae Mama Mwanamwema alitoa salamu zake za pogezi na shukurani kwa WanaCCM wa Wilaya ya Kusini kwa kuweza kumuunga mkno Dk Shein na kuwashukuru kwa kutimiza ahadi zao kwa vitendo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Saleh Ramadhan Ferouz, nae alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kufanya kampeni ambazo hatimae CCM imepata ushindi mkubwa sana katika ushindi wa Majimbo kwa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani.
Alisifu juhudi za Dk. Shein alizochukua mchana na usiku, ambazo zimeweza kuleta ushindi mkubwa, na kumpongeza kwa niaba ya wanaCCM kwa umakini na busara kubwa aliyofanya ya kuunda Baraza la Mawaziri.
Nao wana CCM wa Wilaya ya Kusini Unguja walieleza kutekeleza ahadi yao ya Wadi zote 11 na Majimbo mawili kuwa yatachukuliwa na CCM ahadi ambayo waliitoa wakati Dk. Shein alipofika Wilayani humo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita na kueleza kuwa Mkoa wa Kusini ni Ngome ya CCM.
No comments:
Post a Comment