na Moses Ng'wat, Mbeya |
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mbeya, Sambwee Shitambala, ametangaza kujiuzuru nafasi hiyo, kwa kile alichodai kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa zinazoelekezwa dhidi yake. Shitambala ambaye pia alikuwa mgombea ubunge Jimbo la Mbeya Vijijini amejiuzulu nafasi hiyo kutokana na kutuhumiwa kuwa amehogwa sh milioni 600 na Chama cha Mapinduzi (CCM), hivyo kusababisha ashindwe kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni. Alitangaza uamuzi huo jana alipozungumza na waandishi wa habari kuelezea tathmini ya uchaguzi mkuu ambapo katika mkutano huo aliongozana na viongozi wa chama hicho, Eddo Makata-katibu wa mkoa-na kaimu mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama hicho, Xavery Mwalembe. Alisema licha ya kuchukua uamuzi huo mzito wa kuachia nafasi, bado atabaki kuwa mwanachama mwaminifu na alichokifanya ni kutoa nafasi kwa uongozi wa juu wa chama hicho kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli. Alisema shutuma zinazoelekezwa kwake ambazo pia zinatolewa na wanachama wa CHADEMA na viongozi zimemuweka katika wakati mgumu na kwamba njia pekee ambayo inaweza kusaidia kubaini ukweli ni yeye kujiondoa kwenye nafasi hiyo na uchunguzi ufanyike kwa njia ya haki na huru. Hata hivyo, Shitambala alisema anashangazwa na tuhuma hizo za rushwa kuelekezwa zaidi katika jimbo la Mbeya vijijini wakati yapo majimbo ambayo CHADEMA ilikuwa imeyapa kipaumbele kikubwa cha kushinda katika uchaguzi mkuu, lakini katika hali ya ushindani chama hicho hakikuweza kupata ushindi uliotegemewa. “Tulikuwa na majimbo 150 ambayo chama kilikuwa na uhakika wa kushinda kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo miongoni mwao Songea, Njombe na Tarime, lakini hatukuweza kushinda kama ilivyotokea Mbeya Vijijini sasa nashangaa kwa nini mimi natuhumiwa,” alisema Shitambala. Mbali na tuhuma hizo za kudaiwa kuhongwa na kusababisha mwenyekiti huyo kujiuzulu, alieleza mambo mengi yaliyosababisha ashindwe kwenye kinyang’anyiro cha ubunge uchaguzi wa mwaka huu ikiwemo jiografia ya jimbo la Mbeya Vijijini na pia baadhi ya mawakala wake hususan wa kata ya Inyala ambao walikimbia na hawajulikani waliko hadi sasa. Alisema pamoja na kujiuzulu kwake hana mpango wa kuhamia chama chochote cha siasa na kwamba kama ataamua kuhamia chama kingine cha siasa itakuwa ni maamuzi yake na hayatakuwa maamuzi ya kununuliwa. |
No comments:
Post a Comment