Monday, 22 November 2010

Michezo

Dar Stars, Zanzibar Heroes ukame wa mabao


na Juma Kasesa

TIMU ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na Kombaini ya Nyota wa Dar es Salaam, ‘Dar All Stars’ jana zilishindwa kutambiana na baada ya kwenda sare ya bila kufungana, katika mechi ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo uliokuwa na kosa kosa nyingi za mabao, Dar All Stars ndiyo walikuwa wa kwanza kuliandama lango la Zanzibar Heroes, baada ya Musa Hassan ‘Mgosi’ kukosa bao dakika ya 19, baada ya kutanguliziwa mpira na Salum Swedi aliyekuwa amepanda mbele, lakini shuti lake likaokolewa na kipa Mwadini Ally.
Heroes walijibu shambulizi hilo dakika ya 36, baada ya Abdulhalim Humud kuunasa mpira uliokuwa umeshindwa kuokolewa na mabeki wa Dar All Stars, lakini akababaika na mpira kuokolewa.
Kipindi cha pili, kilianza kwa kasi kwa kila timu kujaribu kusaka bao, lakini mabeki wa kila upande walikuwa imara kuokoa hatari langoni mwao.
Dakika ya 60, Ally Ahmed wa Zanzibar nusura aipatie bao timu yake, baada kuchomekewa pasi na Humud, lakini shuti lake likaokolewa na kipa Ivo Mapunda.
Dakika ya 70, shuti la Jerryson Tegete lilitoka sentimeta chache ya lango la Heroes, baada ya kupokea pasi ya Rashidi Gumbo na kufanya mechi hiyo kumalizika bila ya kufungana.

No comments:

Post a Comment