Saturday, 20 November 2010

CCM, Chadema na CUF wavuna viti maalum zaidi

Na Muhibu Said 20th November 2010


Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imeviongezea vyama vya CCM, Chadema na CUF wabunge baada ya kila chama kugawiwa viti maalum viwili zaidi vya wanawake katika Bunge.
Uamuzi huo wa Nec ulitangazwa jana na Mkurugenzi wake wa Uchaguzi, Rajabu Kiravu, unaifanya CCM kufikisha jumla ya wabunge 67 wa viti hivyo, huku Chadema ikifikisha 25 na CUF 10.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kiravu alisema Tume imefikia uamuzi wa kukipa kila chama mgawo wa viti viwili zaidi maalum vya wanawake katika Bunge.
Viti hivyo ni kati ya viti sita vilivyokuwa vimebaki, baada ya majimbo saba kushindwa kufanya uchaguzi katika majimbo mengine 232 yaliyoko Tanzania Bara na Zanzibar.
“Vyama vyote; CCM, Chadema na CUF kila kimoja kimepata viti viwili viwili,” alisema Kiravu.
Jumla ya viti vyote katika Bunge ni 341; viti maalum vya wanawake vikiwa 102 na vile vya kutoka majimboni 239.
Uamuzi huo wa Nec unatokana na uwiano wa kura, ambazo kila chama kilipata katika uchaguzi mdogo, uliofanyika katika majimbo hayo, Novemba 14, mwaka huu.
Majimbo hayo, ni Mpanda Mjini, Mpanda Vijijini, mkoani Rukwa na Nkenge, mkoani Kagera (Tanzania Bara); pia Magogoni, Mwanakwerekwe, Mtoni na Wete (visiwani Zanzibar).
Katika uchaguzi huo, CUF ilivuna wabunge watatu katika majimbo ya Magogoni, Mtoni na Wete, wakati CCM ilipata wabunge watatu katika majimbo ya Mwanakwerekwe na Mpanda Vijijini na Nkenge na Chadema ilipata mbunge mmoja katika Jimbo la Mpanda Mjini.
Awali, CCM ilipata mgawo wa viti 65 maalum vya wanawake katika Bunge, Chadema 23 na CUF vinane.
Vyama hivyo vilivuna wabunge hao kutokana na uwiano wa kura walizopata waliokuwa wagombea wao wa ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31.
Kabla ya uchaguzi huo mdogo kufanyika, CCM ilivuna wabunge 193 waliowania ubunge kupitia majimboni, Chadema 22 na CUF 24 katika uchaguzi huo (wa Oktoba 31).
Kutokana na idadi hiyo, sasa CCM ina jumla ya wabunge wa majimbo na viti maalum 260, Chadema 47 na CUF 34.

No comments:

Post a Comment