Saturday, 20 November 2010

Msimamo wa Chadema moto


20th November 2010

  CCM sasa yaandaa azimio wafukuzwe ubunge
  Wadau mbalimbali nchini watoa maoni yao
  Wasema ni demokrasia, hawakuvunja sheria
Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati

Siku moja tu baada ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumsusia Rais Jakaya Kikwete, wakati akitoa hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 10 mjini Dodoma, CCM kimesema kinajiandaa kupeleka bungeni azimio la kuondoa ushiriki wa wabunge hao.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Dodoma na Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, alipozungumza na waandishi wa habari.
“Wabunge hao wamekula kiapo cha kutii na kuilinda Katiba, lakini kitendo cha kutomtambua Rais aliyewekwa madarakani kwa mujibu wa Katiba hiyo hiyo ni uvunjaji wa Katiba na hivyo hawastahili kuwemo bungeni,” alisema Chiligati.
“Tunawashauri wajiondoe bungeni haraka, vinginevyo wajiandae kuondolewa kwa azimio la Bunge hadi watakapogundua kwamba Rais yupo na serikali ipo,” alisema.
Wabunge wa Chadema juzi walinyanyuka na kutoka nje ya Bunge mara Rais Kikwete alipoanza kuhutubia, hali ilisababisha Rais kusimama kwa muda kusubiri hali hiyo itulie. Pia wabunge wa CCM waliwazomea walipokuwa wanatoka.
Chiligati jana alisema kukataa matokeo ya urais na kukubali matokeo ya ubunge na udiwani, inaleta maswali mengi ambayo hayana majibu.
“Sasa vipi na kwa wakati gani kura za urais wa Chadema pekee ziliibiwa? Huu ni uzushi wenye lengo la kujenga tabia ya usavimbi na kuleta vurugu nchini. Tunatoa wito wananchi wapuuze uzushi huu,” alisema na kuongeza:
“Tunasisitiza kwamba tamko la Chadema limesheheni uongo na uzushi na linalenga kuamsha na kuchochea chuki, fujo na uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi.”
Chiligati alisema tamko la Novemba 15 mwaka 2010, la kutoyatambua matokeo ya urais na wabunge wa chama hicho na juzi kutoka nje ya ukumbi kususia hotuba ya Rais ni mkakati wa kuwaandaa wafuasi wao kuleta vurugu na uvunjifu wa amani.

MBOWE AMJIBU CHILIGATI
Akizungumza na NIPASHE, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema Chiligati anazungumza kishabiki na kwamba walichokifanya juzi hawakuvunja sheria yoyote ya nchi.
Alisema kitendo walichofanya juzi kililenga kuwaonyesha Watanzania na jumuiya ya kimataifa kuwa kilichofanyika katika uchaguzi, matokeo yake hayakuwa sawa.
Alisema kitendo kilichofanyika kinafanywa na mabunge yote yanayofuata demokrasia ya kweli na kwamba Chiligati alitakiwa kusikiliza hoja na si kutoa vitisho. “Mwenye mamlaka ya kumthibitisha rais katika uchaguzi ni Tume ya Uchaguzi na si lazima kila mtu kumtambua Rais anayechaguliwa,” alisema na kuongeza kuwa:
“Kama Chiligati anaona kuwafukuza bungeni ni sawa basi na wafanye hivyo haraka sana kwa sababu maisha hayapo ndani ya Bunge peke yake na sisi kama wanasiasa tutapata majukwaa ya kuzungumzia siasa hata nje ya Bunge…sisi hatuogopi kufukuzwa ndani ya Bunge,” alisema Mbowe.
Alimtadharisha Chiligati kuwa kama anadhani kuwa hilo ni suluhisho na afanye hivyo aone moto utakaowaka siku zote.
Ofisa mwandamizi wa Bunge, alisema kuwa sio rahisi kuwatimua wabunge wa Chadema kwa sababu kitendo walichofanya hakikuvunja sheria yoyote.
Ofisa huyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini, alisema kuwa wabunge hao wangekuwa wamekiuka sheria na kanuni za Bunge kama wangesusia vikao vya Bunge.
Katika hatua nyingine, wananchi mbalimbali wametoa maoni tofauti kuhusu uamuzi wa wabunge wa Chadema kutoa nje wakati Rais Kikwete akitoa hotuba ya kulifungua Bunge la Kumi mjini Dodoma juzi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Haji Semboja, alisema wabunge wa Chadema walifanya kitendo cha kishujaa.
Dk. Semboja alisema kitendo hicho ni njia mojawapo ya kufikisha ujumbe kwa Rais Kikwete kwamba hawakuridhika na ushindi alioupata katika uchaguzi mkuu mwaka huu kutokana na kuwepo kasoro nyingi.
Aliongeza kuwa wabunge hao walitumia njia nzuri kufikisha ujumbe badala ya kuingia barabarani na kuwahamasisha wafuasi wao kufanya fujo ambazo mwisho wake ungekuwa mbaya.
Dk. Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema wabunge wa Chadema kutomtambua Rais Kikwete ni moja ya mbinu ambayo hutumiwa na vyama vya siasa ulimwenguni kueleza kutokuridhiswa kwao na baadhi ya maamuzi yanayofanywa na Serikali au vyombo vyake.
Dk. Bana, ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, alisema: “Walichokifanya Chadema ni haki yao kwani ni moja ya mbinu zinazotumiwa na vyama vyote duniani kutuma ujumbe pale wanapoona kuwa hawakutendewa haki. “CUF kilishawahi kufanya hivyo huko Zanzibar.”
Hata hivyo, Dk. Bana alisema Rais Kikwete hakujipachika kwenye urais bali alitangazwa kuwa ameshinda kiti hicho na Nec, chombo ambacho kwa mujibu wa sheria ndicho kilicho na dhamana ya kumtangaza Rais.
Alisema Chadema walipaswa kuilaumu na kuisusia Nec ambayo ndiyo iliyomtangaza Rais Kikwete na siyo kumnunia Rais ambaye hakujipachika kwenye madaraka hayo.
“Chadema kama Chama makini cha upinzani hapa nchini kilicho na watu wenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja za msingi mbele ya umma, wana njia nyingi nzuri zaidi ya kueleza madai waliyonayo na wakafanikiwa kuliko hii waliyoamua kuitumia,” alisema.
Dk. Bana alieleza kuwa Chadema wana njia ya kwenda kwa wananchi kushitaki pale wanapokuwa na masuala yanayoiathiri nchi na mara nyingi umma wa Watanzania umewaelewa na kuwaunga mkono.
Alisema kuwa kuna masuala kama orodha ya mafisadi waliyoitoa Mwembe Yanga ambapo walitaja majina ya mafisadi wakubwa nchini.
Alisema kuna ajenda ya ufisadi waliyozunguka nayo nchi nzima katika Operesheni Sangara ambayo ndiyo imewapa viti vingi vya wabunge.
Alieleza kuwa Chadema vilevile wana nafasi ya kulitumia Bunge kurekebisha sheria za uchaguzi ambazo zinaipendelea CCM na hata sheria zinazompa Rais mamlaka ya kuteua watendaji wa Nec.
Dk. Bana aliiasa Chadema ielewe kwamba inaungwa mkono na wananchi wengi kwa sasa na ndiyo maana imepata mafanikio makubwa katika uchaguzi wa mwaka huu, hivyo inapaswa ijizatiti kufanya kazi za kuwakomboa wananchi kama ilivyoahidi kwenye kampeni zake.
UVCCM YAWALAANI
Umoja Wa Vijana wa CCM (UVCCM) umelaani hatua hiyo.
Makamu Mwenyekiti UVCCM, Beno Malisa, alidai kitendo hicho ni igizo la Chadema kwa kuwa kinawanyima haki wananchi waliowachagua wabunge hao.
“Sasa wabunge wanasusia hotuba ya Rais ambayo ndiyo inatoa dira ya utendaji wa serikali kwa miaka mitano ijayo. Februari mwakani ndiyo inajadiliwa na Bunge, sasa hawatashiriki katika kuijadili ?”alihoji.
Harold Sungusia kutoka kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) alisema wabunge hao walitumia haki yao ya kidemokrasia katika kuonyesha kutoridhishwa na ushindi wa Rais Kikwete.
Mwenyekiti wa wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nathanael Mlaki, alisema kitendo cha wanasiasa hao ni cha ujasiri na ukomavu wa kisiasa na kuwataka kuendelea kupigania mabadiliko ya Katiba ya nchi. Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, alisema hakuna haja ya kuwepo kwa malumbano kuhusiana hatua ya wabunge hao.
Alisema jambo la msingi ni kutakiwa kufanya uchambuzi wa kutosha kuhusiana na jambo hilo na kufanyiwa uboreshaji wa kutosha wa Katiba ya nchi.
Nkya alisema wabunge hao walikuwa wanafikisha ujumbe kwa wananchi kuwa uchaguzi wa mwaka huu haukuwa wa haki.
Alisema kuwa kuwepo kwa uchaguzi za uwazi inasaidia kwa asilimia kubwa kutatua tatizo hilo.
Kaimu Mufti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Ismail Makusanya, alisema japo uamuzi uliochukuliwa na wabunge hao wa Chadema ni wa demokrasia, walitakiwa kutumia hekima na busara kabla ya kuchukua uamuzi huo.
Sheikh Makusanya alisema wabunge hao walipaswa kutafakari jambo hilo kwa vile msimamo wa kutomtambua Rais Kikwete, unaweza kuzua mfarakano miongoni mwa wananchi.
Imamu Mkuu wa Msikiti wa Kwa Mnyamani, Buguruni, jijini Dar es Salaam, Sheikh Muhammad Iddi, alisema kitendo kilichofanywa na wabunge hao dhidi ya Rais Kikwete si cha busara.
ARUSHA NAO WAUNGA MKONO
Baadhi ya wananchi jijini Arusha wamesema kitendo hicho ni cha kishujaa, lakini wengine wamedai kuwa ni mchezo wa kuigiza.
Walisema kwa mujibu wa nchi za Afrika, demokrasia haiendi kirahisi pasipo 'kukanyagana viatu' na wakataja nchi za Kenya, Zimbabwe na Zanzibar kuwa ni moja ya vielelezo vya nchi zilizofikia amani baada ya misuguano kama hiyo.
“Mifano ipo mingi, nchi kama Zimbabwe, Kenya na Zanzibar, watawala walishinikizwa kufuata demokrasia baada ya kuichakachua na sasa mabadiliko tunayaona na wengi wanayafurahia,” alisema mkazi wa Mbauda, Fortunatus Mushi.
Alisema kwa uzoefu, Serikali inaonekana kuwa haiko tayari kutengeneza Katiba mpya itakayokidhi mahitaji ya sasa ya wadau wote na itakayotoa haki na ustawi wa taifa na wananchi wake, serikali inapata kigugumizi pia kuunda Tume ya Taifa ya Uchaguzi itakayokuwa huru na kutenda haki kwa wadau wagombea wote wa vyama vya siasa.
Alisema hatua ya wabunge wa Chadema kutoka ndani ya Bunge mbele ya rais, itasaidia kwa kiasi kikubwa kuiambia jamii ya kimataifa kwamba Tanzania kuna shida na lazima utafumbuzi utafutwe.
Naye Amina Salehe, mkazi wa Mbauda, alisema kitendo cha wabunge hao kuondoka mbele ya Rais ni kitendo cha busara kuliko kutumia nguvu kudai haki yao ya kikatiba.
Kwa upande wake Mansoor Mohamed alisema wabunge wa Chadema walitumia haki yao ya kidemokrasia, kufikisha ujumbe kwa dunia na taifa kwa ujumla.
Alisema kama wasingetoka nje ya ukumbi taifa na dunia wasingefahamu kuhusu msimamo wao na kile walichonacho, ila kwa kufanya hivyo watu watawafuata na kuwahoji na kupata kiini cha tatizo.
Mkazi wa Kimandolu, Nanyaro Kaanaeli, alisema walikuwa sahihi kutoka bungeni kwani hakuna namna yoyote ya kuonyesha kutoikubali serikali kwani toka mwanzo chama hicho kilikataa wazi kutambua ushindi wa Kikwete.
Hata hivyo, Julius Chami, mfanyabaishara katika soko la Kilombero na mkazi wa Lemara, alisema hatua hiyo ni ya aibu na inapaswa kulaaniwa kwani haina tija yoyote na kwamba ni kama kichekesho tu.

IRINGA WAUNGA MKONO
Baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Iringa wamesema uamuzi wa wabunge wa Chadema kuondoka ndani ya ukumbi wa Bunge ulikuwa sahihi katika kutekeleza haki ya kikatiba katika kudai haki.
Walisema uamuzi wa Chadema kumsusia Rais Kikwete pamoja na kutohudhuria sherehe za kuapishwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ni hatua kubwa inayoashiria ustawi wa demokrasia nchini kwa kuwa wabunge hivi sasa wameamka na wanajua nini kilichowapeleka bungeni.
David Ngwada alisema kuwa kilichofanywa na wabunge wa Chadema ni jambo zuri la kudai haki ya kikatiba kwa kuwa wanajua kwamba zipo njia mbalimbali za kudai haki na mojawapo ni uamuzi wa juzi ambao lengo lake ni kushinikiza mabadiliko ya Katiba na uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.
“Kususia hotuba ya Rais Kikwete ni sehemu mojawapo katika kudai haki ya kikatiba…wametimiza haki yao na hiyo inaweza kuwa hatua moja mbele, tunahitaji wabunge wa namna hii tena wenye ujasiri mkubwa,” alisema Ngwada.
Alisema kitendo hicho kimefikisha ujumbe mzito kwa watawala na kwamba hiyo ndiyo chachu ya kuwa na vyama vya upinzani ndani ya Bunge kwa kuwa lile Bunge la kupigiana makofi wakati wake umekwisha na kwamba wakati umefika watawala waone yanayopiganiwa ni haki ya Watanzania na wanapaswa kuridhia ili kuifanya nchi iendelee kuwa ya amani na utulivu.
“Maumivu ya uchaguzi bado hayajapona... ni changamoto kubwa kwa Serikali. Tunapoona kuna kutoelewana kati ya Serikali na Chadema kwa hiyo kuna haja kukaa na kuzungumza kwa pamoja. Wote wawe na busara... CCM iwe na busara na Chadema iwe na busara. Haya mambo yameanza na hatujui yataendeleaje,” alisema Sigfrid Sanga, mkazi wa Makambako Wilaya ya Njombe.
KILIMANJARO NAKO
Kwa upande wao, wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wametoa maoni tofauti kuhusiana na kitendo cha wabunge wa Chadema.
Baadhi wamesema kimeonyesha kukomaa kwa demokrasia na kufikisha ujumbe kwa Serikali na wadau wa ndani na nje ya nchi kwamba ule wakati wa kukubaliana kwa kila kitu umepitwa na wakati.
Maria Msuya, mkazi wa Msaranga mjini Moshi, alisema jambo la msingi ambalo Chadema na vyama vingine vya siasa wamepiga nalo kelele kwa muda mrefu ni mabadiliko ya Katiba.
“Juzi Chadema walisusa kumsikiliza Kikwete kwa vile tu hawakubaliani na matokeo ya uchaguzia ambayo yalimpa ushindi. Ifike mahali sasa Bunge lifanye mabadiliko ya Katiba kwani leo hii CCM inaiona ni nzuri kwao, lakini ipo siku nao watalalamikia mabadiliko ya Katiba mara chama cha upinzani kitakapoingia madarakani na kufanya haya yanayofanywa na CCM kwa sasa,” alisema.
Alisema Serikali ya CCM ijifunze kutokana na jinsi ilivyoingia madarakani, ukweli inaujua yenyewe pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kwamba kama Dk. Willibrod Slaa anazusha na kusababisha wananchi waichukie Serikali yao wampeleke mahakamani vinginevyo wananchi wataamini kwamba Serikali ndiyo inayodanganya.
Nathanael Mwandete, mkazi wa Majengo, alisema hatua hiyo ni sahihi kwani inaonyesha dhahiri kuwa ushindi wa CCM uligubikwa na kasoro nyingi.
Alisema kitendo cha wabunge wa Chadema ni haki yao ya kidemokrasia kutokana na mashaka yao dhidi ya kura za urais.
Mkazi mwingine wa Manispaa ya Moshi, Claudia Kayombo, alisema kama mwananchi wa Tanzania hapendi kuona demokrasia inachezewa na kwamba anakubaliana na hatua ya wabunge hao.
TANGA WAKOSOA
Baadhi ya wananchi wa mkoani hapa wamezungumzia kwa hisia tofauti kitendo cha wabunge wa Chadema kumsusia Rais Kikwete kwamba kinaashiria uvunjivu wa amani nchini.
Wamesema ni ukweli usipopingika kwa huenda Chadema walikuwa na malalamiko ya msingi katika suala zima la madai ya kuchakachuliwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka huu, lakini namna wanayotumia kuwasilisha madai yao haiendani na matakwa ya wananchi.
Walisema kimsingi Watanzania wamezoea utulivu na amani hivyo kitendo hicho kinaweza kuleta mapokeo tofauti ndani ya jamii kutokana chama hicho kufanikiwa kukubalika katika maeneo mengi nchini.
“Kama hawa viongozi wa juu wa Chadema wameanza hivi sasa wale waliopo kuanzia ngazi ya chini ya Mitaa na Kata nao wakikataa kutoa ushirikiano na viongozi wengine ambao watakuwa ni wa CCM wananchi ndio watakaoathirika zaidi na mgogoro huo pia utakwamisha shughuli za maendeleo,” alisema Josephat Leonard, mwanaharakati wa maendeleo jijini Tanga.
Leonard alisema kitendo hicho ni dharau kwa kuwa Rais Kikwete ameshaapishwa na yupo madarakani kwa mujibu wa kanuni na sheria za nchi hivyo Chadema hawana budi kutafuta namna nyingine ya kupata suluhu ya madai yao kwa njia ya amani. “Chadema nao sasa wasiwe na maamuzi ya kuburuzana kwa sababu jana (juzi) ilionyesha dhahiri walikurupuka…sikuona sababu ya kufanya vile wakumbuke hata kama wao wanaamini matokeo yamechakachuliwa, lakini wakubali,” alisema Mariam Jumaa, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), jijini hapa na kukiomba chama hicho kutafuta suluhu ya madai yao kwa njia ya amani.
MBEYA WAKOSOA
Wakazi kadhaa wa Jiji la Mbeya wamepinga uamuzi huo kwa madai kuwa sio wa kizalendo, huku wengine wakiunga mkono kwa madai kuwa ndio njia pekee ya kuonyesha hisia zao za kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi uliomungiza Kikwete madarakani.
Mfanyakazi wa Kiwanda cha Saruji cha Mbeya, Amir Wesai, alisema kitendo cha kususia sio sahihi kwa kuwa wametumwa na wananchi wa majimbo yao kuwawakilisha bungeni.
Alisema kususia Bunge wakati Rais akitoa dira ya mwelekeo wa nchi, kinaonyesha kuwa wanajali zaidi maslahi ya chama chao kuliko maslahi ya wananchi waliowachagua na taifa.
Naye mkazi wa Soweto, Perucy Muyabi, alisema kitendo hicho si cha kizalendo na kimemdhalilisha Rais na taifa kwa ujumla machoni mwa mwa mataifa mengine.
Alisema Wabunge hao wangetafuta njia nyingine ya kuonyesha hisia zao na si kitendo walichokifanya wakati macho ya dunia nzima yakiwa yameelekezwa bungeni.
Mwenyekiti wa Mtandao wa wasomi wa Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema walikurupuka bila kujiandaa.
“Nadhani ni bahati mbaya sana kwa walivyofanya Chadema kwa sababu hawakujiandaa, kama wangejiandaa wasingeweza kumteua Tundu Lisu kwenda kuhesabu kura za Pinda aliyeteuliwa na Rais Kikwete ambaye wao wanadai kuwa hawamtambui,” alisema Mwaihojo.
Imeandikwa na Godfrey Mushi (Iringa), Lulu George (Tanga), Salome Kitomari na Charles Lyimo (Moshi), Emamanuel Lengwa (Mbeya),Charles Ngereza na Cynthia Mwilolezi (Arusha), Muhibu Said, Richard Makore, Raphael Kibiriti na Beatri

No comments:

Post a Comment