Monday, 17 June 2013

Masikini CCM, yenda arijojo kama kishada 


Baadhi ya Wanachama wa CCM wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa UVCCM
Baadhi ya Wanachama wa CCM wakiwa kwenye Mkutano Mkuu wa UVCCM
AMA kwa hakika chama kilichojitokeza kuwa dume katika siasa za Tanzania – Chama Cha Mapinduzi (CCM) – kinadodomea na ni vigumu tena kurudia enzi zake za udume. Baada ya kufanikiwa kutawala katika uwanja wa siasa Zanzibar, sasa kinakwenda arijojo.
Ni arijojo kwelikweli mfano wa kishada kilichomtoroka mchunga wake baada ya kamba kukatika. Kinaonekana juu kikizidi kupaa lakini huku kikimtia simanzi mwenyewe aliyekitengeneza, akakitia kamba na kukirusha kwa matumaini ya kuambaa kikiwa mikononi mwake na hatimaye kirudi kwake.
CCM ni chama kilichopoteza mvuto kwa umma wa wananchi wa Zanzibar na tayari kinachungulia kaburi. Nasema hivi kwa sababu ya ushahidi unaozidi kujitokeza. Watu wanakikimbia na kuhamia kwengine.
Nimeshuhudia hali hii wakati wa mkutano wa hadhara ulioitishwa Jumapili iliyopita na Chama cha Wananchi (CUF) katika kijiji cha Tundangaa, ndani ya Jimbo la uchaguzi la Matemwe, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mwendesha matangazo (MC) katika mkutano huo, Masoud Kibonge, alipotangaza kuwa kuna wanachama wa CCM wamejiandaa kuchukua kadi za CUF, nilijua watakuwepo kweli. Sikujua idadi yao, ila nilijua itakuwa kubwa ya kushtua.
Wakati ulipofika wa kitendo hichi, MC Masoud akavuta karatasi. Akaanza kusoma majina. Mara naona watu wanachomoka kutoka miongoni mwa umati uliohudhuria mkutano. Wanatoka na kusaidiwa kujipanga na walinzi wa amani wa chama.
Haaa! Ni watu wa makamo, lakini wengi wao ni vijana wabichi waliopigika kwa umasikini ingawa wanaishi pembeni mwa bahari iliyojaa samaki na matunda mengine ya baharibi. Kijiji cha Matemwe kipo kando tu ya Bahari ya Hindi katika upande wa kaskazini mwa kisiwa cha Unguja.
Cha kushangaza ni kwamba wale watu walikuwa wanarudisha kadi ya rangi kijani, papo hapo wanakabidhiwa kadi ya rangi nyeupe. Rangi kijani ni CCM na rangi nyeupe ni CUF, chama kinachoipa CCM muadhara wa kihistoria wa kuporomoka hadhi yake.
Kijana anaitwa jina, anaitika kwa sauti ya nguvu. Anatoka alikokaa na kuharakia kule anakoitwa. Anafika huku akidemka midundo ya beni mbili zilizokodiwa maalum kwa ajili ya kupambisha mkutano na pengine tukio hilo la kurudishwa kwa kadi za CCM kwa wasiokuwa viongozi wa CCM.
Najiuliza kwanini mtu anaitwa kukabidhiwa kadi mpya ya CUF, anafurahia wakati miaka michache iliyopita alikuwa hataki hata kusikia khabari za chama hichi kinachosakamwa kwa kila mbinu ili kisikamate mamlaka ya kuongoza dola? Jawabu ni rahisi, ametambua.
Watu wa Matemwe wametambua njia sahihi miaka 21 tangu mfumo wa vyama vingi uliporudishwa kwa mujibu wa sheria baada ya kupigwa marufuku mara tu Afro Shirazi Party (ASP) walipofanikiwa kuiangusha serikali ya uhuru ya Zanzibar Januari 12, 1964.
Njia wanayoichagua sasa kupita ni ile ambayo walikuwa hawaioni, au wakiibeza kuwa si njia njema ya wao kupita. Hakika waliibeza njia kwa sababu walipumbazwa kiasi cha kutosha na viongozi wa CCM.
“Nimeona chama hichi viongozi wake wanazungumza mambo yanayonifurahisha mimi kama Mzanzibari,” anasema Mosi Kona Haji (si jina halisi), msichana wa umri wa miaka 20, baada ya kuulizwa na mwandishi wa makala hii sababu ya kujiunga na CUF.
Mosi anasema amechukua uamuzi huo baada ya kufikiria kwa muda mrefu kutokana na kusikiliza hotuba za viongozi wa CUF kupitia kanda za video. “Kila nikisikia umefanyika mkutano wa CUF natafuta kanda yake nasikiliza nyumbani. Basi mazungumzo yao yananikuna maana naona yanatetea nchi yetu,” anasema.
Kuna jambo jingine lililompa nguvu kuipenda CUF – viongozi wake wanaeleza mipango ya kuwapatia ajira vijana ili wasihangaike kwenda kuhamia mjini bila ya kibarua. “Unajua huku tunazo hoteli kubwa lakini tunaona hivihivi wanaoajiriwa ni wageni wanaojipachika majina kama yetu. Inatuumiza maana hata kazi za kukata majani ya bustani wanakuja wanawake wageni wengine wanatoka nje ya nchi,” anasema kwa unyonge.
Moja ya tatizo kubwa katika nchi ni ukosefu wa ajira. Tatizo hili limesababisha wimbi kubwa la vijana kubaki vijiweni kutwa nzima wakipiga soga katika muda ambao walipaswa kuwa wanazalisha mashambani, au ofisini au viwandani, au kwenye karakana za kutengeneza vipuri mbalimbali kwa ajili ya magari au mashine.
Ukosefu wa ajira ni moja changamoto kubwa zinazoikabili serikali ya CCM nchi nzima. Mara kadhaa viongozi wakubwa katika serikali na chama chenyewe, waliopo kazini au waliokwishastaafu, wamekuwa wakiitahadharisha serikali kuwa inalea bomu la hatari.
Kwa Zanzibar, hilo ni moja tu kati ya matatizo mengi yaliyosababisha watu waichoke CCM. Kimekuwa kikilea siasa za fitina, chuki, choyo na hasadi. Chama hichi kinashindwa kusimamia sera zake na hivyo kuwanyima wananchi haki yao ya kupata maendeleo kupitia sera hizo ambazo viongozi wake walizitolea ahadi kuwa zitabadilisha maisha ya watu.
Basi baada ya kitendo cha kutoa kadi kwa wanachama wapya kumalizika, umma ukaambiwa watu 609 walichukua kadi za CUF. Wapo waliorudisha kadi za CCM, nyingine zikiwa mpya za karibuni tu, bila ya wenyewe kujitokeza hadharani ili kuchukua kadi za CUF. Kielelezo kingine cha namna kulivyoshamiri siasa za vitisho nchini na hususan maeneo ya vijijini ambako muamko wa watu kutambua haki zao huchelewa sana kulinganisha na kwenye miji.
Matemwe ni moja ya majimbo ndani ya mkoa wa Kaskazini Unguja ambayo CCM ikijinasibu kuwa ndiyo ngome yake. Mengine ni Tumbatu, Chaani, Mkwajuni na Nungwi ambalo walilipoteza mbele ya CUF kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
“Wanataharuki kwa kuona mkoa umewatoka huu. Lakini maji yaliyokwishamwagika hayazoleki au siyo wananchi?” Ndiyo kauli ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye alionesha angali kiongozi mwenye afya nzuri alipomudu kusimama kwa zaidi ya nusu saa akipokea kadi za CCM na kugawa za CUF kwa wana-Matemwe waliojiunga mkutanoni.
Taharuki imewakumba viongozi wa CCM kiasi cha kumchochea Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ahmada Khamis Ali ambaye baada ya kusifiwa wiki kadhaa zilizopita kwa ukakamavu wake dhidi ya shinikizo za viongozi wa CCM kutakiwa ateremshe bendera za Jumuiya ya Uamsho mkoani, ameridhia kuzuia makundi ya wafuasi wa CUF waliokuwa msafarani kwenda Matemwe.
Alipopigiwa kelele ateremshe bendera za Uamsho aligoma na kusema hapokei amri za ovyo labda kama zinatoka kwa Rais wa Tanzania, Kamishna wa Polisi Zanzibar na Inspekta Jenerali Said Mwema aliyemteua. Kauli hii ndiyo hasa iliyosababisha viongozi wa CCM mkoani kumshitaki kwa Rais Dk. Ali Mohamed Shein ambaye kwa bahati, hakubabaika.
Muda mfupi kabla ya kitendo cha kukabidhi kadi mpya za CUF kuwadia, alipanda jukwaa kubwa la mkutano Mwanze Abdalla Ali, ndugu wa Ali Abdalla Ali, kiongozi mwandamizi wa CCM ambaye aliwahi kuwa mbunge na mwenyekiti wa chama hicho mkoa.
Mwanze alitumia dakika moja na nusu tu kuzidi kuipasua CCM aliposema “Nasema sijakosea kujiunga na CUF kwa sababu haya yanathibitisha nia njema kabisa ya chama hichi na Maalim Seif kama kiongozi imara anayeipenda nchi yangu ya Zanzibar na watu wake.” Mwanze alijiunga na CUF Machi 3, mwaka huu kwenye uwanja wa Kishungambuzi, Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Siku hiyo, Maalim Seif alihutubia mkutano mkubwa katika kijiji ambacho CCM inatamba kuwa ni ngome yake kuu. Wanachama kadhaa wa CCM walirudisha kadi na kuchukua za CUF.
Risala ya wananchi wa Matemwe ilieleza wazi kuwa wananchi wameamua kubadilika kisiasa kwa sababu CUF inatetea Uzanzibari na kupatikana kwa Zanzibar yenye mamlaka kamili chini ya Muungano wa Mkataba katika kipindi hichi cha kutafutwa kwa katiba mpya ya Tanzania.
Hatimaye misafara ya wanachama wa CUF na wananchi waliofika Matemwe ilijikuta ikitabasamu njia nzima ya Matemwe hadi Kinyasini kutokana na kulakiwa na watu waliojipanga pembeni mwa barabara wakionesha kuunga mkono CUF.
Yote hayo ni ishara za wazi za kudodomea kwa CCM katika maeneo iliyoyatawala kwa miaka mingi na sasa kushuhudia kikiporomoka.
Chanzo: Fahamu

No comments:

Post a Comment