Sunday, 8 July 2012

Serikali irudishe Sh16 trilioni zilizofichwa ughaibuni 

 
undefinedSIRI zinazoendelea kufichuka kuhusu matrilioni ya fedha ambazo viongozi na wafanyabiashara hapa nchini wamezificha katika benki nje ya nchi sasa zimeanza kutoa mwanga na majibu kuhusu sababu hasa za Watanzania kuendelea kuwa maskini wa kutupwa ilhali nchi yao ina rasilimali nyingi na utajiri mkubwa.

Ni majibu ambayo Watanzania wamekuna vichwa kwa muda mrefu wakitaka kuyapata, huku baadhi yao wakiwa tayari wamekata tamaa kiasi cha kujenga dhana potofu kwamba pengine Mwenyezi Mungu amelaani nchi yetu, hasa baada ya baadhi ya viongozi wetu wakuu kusema kwamba nao hawajui kwa nini nchi yetu ni maskini.

Kufichuka kwa siri hizo hivi karibuni kumetufumbua macho kwamba umaskini wetu haukutokana na laana za Mwenyezi Mungu, bali ufisadi wa viongozi na kukosekana kwa utawala bora na uwajibikaji katika uendeshaji wa serikali tangu chama tawala cha CCM kilipolizika Azimio la Arusha.

Itakumbukwa kwamba wiki iliyopita siri ilifichuka kuwa, Watanzania sita wameficha zaidi ya Sh303 bilioni katika akaunti za benki mbalimbali nchini Uswisi na kwamba fedha hizo ziliwekwa katika akaunti hizo na baadhi ya makampuni ya kuchimba mafuta na gesi yanayofanya kazi hapa nchini. Na katika kuthibitisha kwamba fedha hizo ni za kifisadi, kwa maana ya kutolewa kwa lengo la kuwahonga viongozi, wenye akaunti hizo hawajaweka hata shilingi moja kwenye akaunti hizo.

Tayari zipo ripoti kadhaa za kimataifa kuhusiana na fedha zilizofichwa ughaibuni na viongozi wa nchi mbalimbali barani Afrika. Pamoja na Serikali ya Uswisi kukiri kwamba fedha za Watanzania hao sita ziko katika benki kadhaa nchini humo, hadi sasa majina ya watu hao bado hayajafahamika na Serikali haijaonyesha nia na dhamira ya kushirikiana na mamlaka za kimataifa kuwasaka na kuwatia mbaroni watu hao wenye fedha hizo chafu za kifisadi.

Kama hiyo haitoshi, juzi Bunge linalokutana mjini Dodoma lilipewa taarifa ya kushtusha kwamba viongozi na wafanyabiashara kadhaa nchini wametorosha na kuhifadhi katika benki nchi za nje fedha zipatazo Sh16.6 trilioni. Akichangia hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Rais, kwa mwaka 2012/13, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM) alisema ripoti ya mwaka 2008 ya taasisi ya kimataifa inayochunguza fedha chafu kutoka barani Afrika (Global Financial Intergrity Report 2008) imebainisha kwamba Sh16.6 trilioni zimefichwa nje ya nchi na viongozi na wafanyabiashara wa hapa nchini na kuituhumu Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa, pamoja na benki hiyo kufahamu suala hilo, hadi leo haijabainisha ni za nani, ziliibwa lini, majina ya wamiliki wa fedha hizo na lini fedha hizo zitarejeshwa nchini.

Kama tulivyoeleza hapo juu, ‘siri’ hizo sasa zimewafanya Watanzania wajue kwamba chanzo cha umaskini wao ni ufisadi wa viongozi na washirika wao ambao wamekuwa wakiingia katika mikataba mibovu na wawekezaji, pamoja na kutorosha fedha, maliasili na rasilimali za nchi yetu kwenda nchi za nje. Kwa mfano, Sh16.6 trilioni zilizofichwa nje ya nchi ni kikubwa mno, kwani ni zaidi ya bajeti ya Serikali ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka mmoja wa fedha, kwani bajeti ya mwaka huu wa fedha ni Sh15 trilioni.

Huo bila shaka ni uhujumu mkubwa wa uchumi wetu, kwani fedha hizo zingebaki nchini zingesaidia uchumi wetu, kwa maana ya kuziwekeza katika sekta muhimu za maendeleo. Tunapata wakati mgumu kuelewa sababu za kupeleka fedha nje kama kweli zimepatikana kwa njia halali, kwani kama ni kutafuta fedha za kigeni tayari tuna benki za kigeni hapa nchini.

Matokeo ni kwamba fedha zetu zinajenga uchumi wa nchi nyingine, zikiwamo nchi tajiri sana duniani. Haya ni matokeo ya viongozi wetu kukosa uzalendo na kukumbatia ufisadi. Tunaishauri Serikali ihakikishe fedha hizo na nyingine ambazo hazijabainishwa zinarejeshwa nchini na wahusika wote wanawajibishwa kisheria.

No comments:

Post a Comment