Sunday, 8 July 2012

Madaktari: Mate yaweza kueneza virusi vya Ukimwi 

 
undefinedLeon Bahati
WATAALAMU wa afya nchini wamefafanua kuwa kuna uwezekano mate kuwa na virusi vya Ukimwi (VVU).
Ufafanuzi huo umetolewa kufuatia watu wengi kukumbwa na utata baada ya ugunduzi wa hivi karibuni wa kipimo cha kutambua waathirika wa Ukimwi kwa kutumia ute unaopatikana katika kinywa.
Watu mbalimbali waliokuwa na dukuduku hilo walipiga simu kwenye ofisi za gazeti hili baada ya kuripoti kuhusu Mamlaka ya Kudhibiti Chakula na Dawa Nchini Marekani(FDA), kuthibitisha na kupitisha matumizi ya kifaa hicho kinachojulikana kwa jina la OraQuick.
Madaktari waliohojiwa na Mwananchi Jumapili walisema kuwa kipimo hicho hakipimi uwepo wa VVU kwenye mate bali aina maalumu ya chembe kinga zinazojulikana kwa jina la kitaalamu kama ‘antibodies’, ambazo huzalishwa na mwili baada ya virusi kuingia katika mwili wa binadamu.
“Kinapima uwepo wa antibodies kwenye mate na siyo virusi vya HIV (VVU),” alisema Mtaalamu wa Afya wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania (NACP), Dk Josiah Mwandry.
Aliongeza: “Hizi antibodies(chembe kinga), huweza kupenya na kupatikana sehemu yoyote yenye umajimaji mwilini.”

Tofauti na chembe kinga, Dk Mwandry alisema VVU havina kawaida kuwa kwenye mate kwa sababu siyo mazingira yake, yanayoviwezesha kuishi na kuendelea kuzaliana.
Mtaalamu huyo ambaye amekuwa akishiriki mapambano dhidi ya VVU nchini, alisema iwapo damu itatoka sehemu yoyote ya kinywa na kuchanganyika na mate pale mtu anapokuwa na vidonda au kuumia, virusi navyo vitakuwepo.
Kulingana na maelezo ya mtaalamu huyo, mate yanaweza kusambaza virusi vya Ukimwi kwenda kwa mwingine pale yanapotoka kwa mtu mwenye vidonda au michubuko na kuingia kwa mtu mwingine ambaye pia ana tatizo hilo kinywani.
Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania(Tacaids), Morice Lekule aliwataka watu kutochanganyikiwa akieleza kuwa havikai katika mate na kwamba wazingatie elimu kuhusu Ukimwi wanayoitoa sehemu mbalimbali nchini.
Alifafanua kuwa kwa kawaida mate siyo eneo muhimu kwa VVU kukaa, lakini akasema wanaweza wakawepo kama ajali.
Kuhusu mate kuwa na chembe kinga, Lekule alisema kuwa mwili wa binadamu una aina nyingi ya chembe kinga, lakini zinatofautiana kwa kuwa hutengenezwa kulingana na aina ya adui aliyeingia.

Kuhusu namna OraQuck inavyofanya kazi, Lekula alisema: “Ni sawa na wewe upande kwenye mti, au mlima na kwa mbali ukaona askari wamejipanga eneo fulani, utagundua kuna vita.”
Baadhi ya watu waliopiga simu kwenye gazeti hili, walieleza kuwa wamekuwa wakipigana busu na wapenzi wao, hata kunyonyana ndimi wakati wa mapenzi, wakiamini mate hayana VVU.
Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina, watu hao walisema taarifa za kipimo hicho cha OraQuick zimewashtua kwa kuwa wanaamini njia hiyo haisambazi VVU.
Wiki iliyopita, FDA ilitangaza kuthibitisha kipimo cha OraQuick baada ya kubaini kina uwezo wa kutoa majibu sahihi kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kati ya dakika 20 na 40 baada ya kupima.
Wataalamu hao wa Marekani walisema kifaa hicho kimebuniwa siyo tu kwa ajili ya matumizi ya hospitalini, bali pia nyumbani na kitaanza kupatikana katika maduka ya dawa nchini Marekani kuanzia Oktoba mwaka huu.
FDA ilieleza kwenye ripoti yake kwamba wakati huo kipimo hicho kitaanza pia kusambazwa sehemu nyingine duniani kwa taasisi, mashirika na hata watu binafsi watakaokiagiza kwa kutumia mtandao wa kompyuta.
Marekani inaamini kifaa hicho kitasaidia kupunguza maambukizo ya VVU kwa kubadili tabia ya watu wanaoishi na virusi hivyo bila kujua.
Wataalamu mbalimbali wa afya walikielezea chombo hicho kuwa ni hatua nyingine muhimu kwa dunia katika jitihada zake za kudhibiti maambukizo ya VVU.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Marekani ya Kupambana na Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (NIAID), Profesa Anthony Fauci alisema: “Hii ni hatua nyingine ya kisayansi ya kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi.”
Alisema kipimo cha OraQuick ni moja ya hatua muhimu ambayo wanasayansi walikuwa wakihangaika usiku na mchana katika jitihada za kupata vipimo rahisi na tiba.
Profesa Fauci alisema jitihada za wanasayansi hao katika kupambana na Ukimwi zimewezesha kudhibiti maambukizo ya VVU kwa asilimia 96, sasa.
Dk Robert Gallox aliyemgundua mtu wa kwanza mwenye VVU mwaka 1984 nchini Marekani, alisema hatua ya FDA kupitisha kipimo hicho itasaidia kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi hivyo duniani.

Kinavyotumika
OraQuick hakina tofauti na vipimo vingine vya kisasa, ambavyo vimebuniwa kwa ajili ya kupima magonjwa kwa haraka, kama vile vya malaria, Ukimwi na kisukari.
Tofauti yake ni kwamba, badala ya kuwa na sehemu ya kudondoshea tone la damu, kina sehemu laini iliyojitokeza, maalumu kwa ajili ya kunyonya ute.
Mtumiaji wa kipimo hicho hapaswi kukitemea mate, bali kwa kutumia sehemu hiyo maalumu, atakiingiza kifaa hicho mdomoni na kuchukua mate katikati ya fizi na midomo chini au juu.
Sehemu hiyo laini italoa mate na kuyanyonya ambapo mpimaji atapaswa kukiondoa na kukiweka sehemu kavu kusubiri kumpatia majibu ndani ya muda huo wa kati ya dakika 20 na 40.
Gharama zake
Hakuna uhakika juu ya bei kamili ya kipimo hicho. Taarifa za awali zinaonyesha kuwa kitauzwa kwa Dola za Marekani 17.50 sawa na Sh27,300.
Moja ya masharti yaliyowekwa na FDA ni kuuza kipimo hicho kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 17 na kuendelea.

No comments:

Post a Comment