Vurugu za uamsho Zanzibar: Je, tutangaze kuchafuka hewa kisiasa?
Nasaha za Mihangwa
Joseph MihangwaToleo la 242, 6 Jun 2012
JUMAPILI, Mei, 27 mwaka huu, nilitembelea Zanzibar na kurejea Dar es Salaam nikiwa nimejawa huzuni kubwa kuliko nilivyoondoka.
Niliyobaini huko Unguja kuhusu joto la kisiasa, hususani kuhusu Muungano, ni ishara ya kutosha kwamba Muungano wetu unaelekea kubaya.
Maandishi ya kichochezi na lugha za kashfa dhidi ya “ubara”, zimezagaa pembe nyingi za mitaa ya Unguja. Kichocheo cha haya yote kimekuwa ni kile kinachoitwa “mchakato wa Katiba mpya”.
Kwa hali nilivyoiona, nashawishika kuamini kwamba, vurugu zinazoendelea sasa, za maandamano na kuchoma makanisa na baa Visiwani, haziwezi kutulizwa kwa nguvu ya dola pekee, wala lugha kali kali za viongozi serikalini. Serikali inatakiwa kuchimbua zaidi kujua chanzo na mzizi wa tatizo.
Haiingii akilini, kwamba kikundi cha kidini kama kile cha “Jumuiya ya UAMSHO na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMUKI) kinaweza kuzua tafrani, taharuki na mitafaruku ya kisiasa kama hiyo Zanzibar na Serikali ikaishia kutoa hotuba tu za kuomba utulivu, kisha ikanyamaza, wakati Zanzibar pakiendelea kufuka moshi.
Nilichobaini ni kwamba, hoja za kikundi cha Kiislamu cha UAMSHO zinaungwa mkono na zaidi ya asilimia 80 ya Wazanzibari. Asilimia 99 ya Wazanzibari ni Waislamu.
Huenda ni kwa sababu hii, kiongozi wa UAMSHO, ameweza kupata ujasiri wa kuitangazia dunia kuwa, wataendelea kupinga Muungano wa Tanzania “hadi kieleweke” wala asiguswe na Serikali.
Ni ukweli usiopingika kuwa, “Siasa na dini” haviwezi kutenganishwa. Hii ni kwa sababu lengo la dini ni maisha bora ya wafuasi wake hapa duniani wakati wakijiandaa kwa maisha ya utukufu mbinguni. Zaidi ya hilo, Wafuasi wa dini wanaguswa kwa nyanja zote na kuathirika kwa njia moja au nyingine na maamuzi ya wanasiasa hapa duniani. Isitoshe, Wafuasi hao ni sehemu ya umma unaopiga kura kuweka Viongozi madarakani.
Kwa sababu hiyo, viongozi wa dini wana haki stahili kuzungumzia au kukemea maovu yote ya kisiasa na ya wanasiasa yanayoonekana kuwakandamiza wananchi, wakiwamo wafuasi wa dini.
Kwa misingi hii, UAMSHO, kupitia wafuasi wao, wana haki ya kujadili Katiba, na vivyo hivyo kujadili Muungano.
Lakini kwa chombo cha kidini kupinga au kupambana na Serikali kisiasa juu ya jambo la kisheria na kikatiba kama “Muungano” kwa njia ya harakati za kidini, ni kuvuka mipaka ya uhuru wa dini kushiriki katika siasa. Inaweza kuwa hivyo kwa Taifa linaloongozwa kidini (theocratic state), lakini si kwa nchi isiyo na dini kama yetu. Hilo ni la kwanza.
La pili ni hili: Kitendo cha Uamsho kuungwa mkono na zaidi ya asilimia 80 ya Waislamu Visiwani ni kisirani na ishara mbaya kwa Muungano, kwa maana kwamba Wazanzibari wengi hawautaki Muungano.
Inavyoonyesha, ni viongozi wa Serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wazanzibari wengineo Visiwani, ndio pekee wanaounda hiyo asilimia 20 ya watetezi wa Muungano.
Ni kwa sababu hii pia kwamba sishangazwi na lugha za kibaguzi Visiwani dhidi ya Wazanzibari wenye asili ya Bara kuitwa “Wazanzibara” na Wazanzibari wenzao. Wala sishangai kuona makanisa na baa zikichomwa moto kwa sababu zinahusishwa na Ukristo wa kibara, vitu ambavyo ni haramu kwa Mwislamu.
Ukiunganisha na Watanzania Bara wanaoungana na asilimia 20 ya Wazanzibari wasioutaka Muungano ni wazi kuwa, yamkini si shwari tena Tanzania; busara inatakiwa kutumika kutafuta suluhisho.
Bado tunakumbuka Azimio la Bunge la kikundi cha G.55 miaka 18 iliyopita, pale lilipoazimia kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika. Hii ni ishara tosha kwamba, hata Bara hali si shwari, kwa maana G.55 bado wapo, na walikwishaambukiza na wanaendelea kuambukiza sumu ya kupinga Muungano.
Mitafaruku kama hii ya Uamsho juu ya Muungano, si jambo geni Visiwani. Mwaka 1983, Wazanzibari waliodai kuchoshwa na Muungano, walianzisha redio yao mafichoni, iliyokuwa ikiingilia masafa ya iliyokuwa Redio Tanzania (RTD) wakati ule, kwa kutangaza chuki dhidi ya Muungano, pamoja na kukashifu viongozi.
Redio hiyo na kipindi chake maarufu kama “Kiroboto Tapes”, ilianza matangazo yake ya kila asubuhi kwa sauti ya jogoo kuwika, na kumaliza na maneno: “Tunataka turejeshewe Visiwa vyetu vilivyoporwa na Watanganyika”
Redio hiyo hatimaye, iligunduliwa na kuzimwa na Kikosi cha Jeshi la Wananchi, baada ya juhudi kubwa za muda mrefu kubaini ilipokuwa, lakini tayari ilikuwa imekwishaleta madhara makubwa kwa mustakabali wa Muungano.
Miezi kadhaa baadaye, Rais wa awamu ya pili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, alijiweka hadharani kutaka kuhoji mahakamani, uhalali na muundo sahihi wa Muungano. Kwa njia hiyo, akawa amejaribu kukanyaga mahali patakatifu bila kuvua viatu. Hiyo ilikuwa ni dhambi kubwa yenye kuuwa kwa mtazamo wa vigogo wa Chama tawala!
Kwa kuthubutu kwake kufanya hivyo, Kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Taifa, kikaitishwa haraka haraka kumjadili Jumbe juu ya “ujasiri” wake huo wa kuhoji Muungano; naye hakumumunya maneno; akasema alikuwa akitumia haki yake ya kikatiba chini ya ibara ya 126 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977, inayotoa nafasi kwa utata wowote juu ya tafsiri ya Muungano unaoweza kuwa unabishaniwa, kati ya Serikali ya Zanzibar, kuhojiwa mahakamani kupata suluhisho.
Jumbe alitimuliwa na kuvuliwa nafasi zote za uongozi wa CCM na Serikali; Serikali ya Muungano ikatangaza kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar.
Yanayofanywa sasa na Uamsho ni yale yale ya “Kiroboto Tapes” na ni historia kujirudia; kuna vigogo nyuma, tena ndani ya Serikali mithili ya Jumbe; Jumbe aliwekwa kizuizini nyumbani kwake.
Lakini, tatizo liko wapi, na nini kinachogomba hivi leo kuzua Uamsho?
Uamsho na Wazanzibari wengi wanataka kura ya maoni juu ya uhalali wa Muungano, kwa madai kwamba wananchi hawakushirikishwa kujadili kabla ya kufikiwa kwa Muungano huo! Kwa maoni yangu, huo ni mtazamo potofu juu ya uhalali wa Muungano.
Mkataba wa Muungano (Articles of Union) uliofikiwa na wakuu wa nchi mbili – Tanganyika na Zanzibar, Aprili 22, 1964; ni Mkataba wa Kimataifa ambao, kwa mujibu wa mfumo wa Sheria wa Uingereza (British Common Law System) uliokuwa unatawala na kutamka kwa nchi zote zilizokuwa chini ya nchi hiyo wakati huo zikiwamo Tanganyika na Zanzibar, Marais hao wawili – Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika, na Abeid Amani Karume wa Zanzibar, walikuwa na uwezo na uhalali wa kuingia mkataba kama huo bila kuwauliza wananchi wao kwa njia ya kura ya maoni.
Kilichotakiwa pekee baada ya mkataba huo kutiwa sahihi, ni Bunge la Tanganyika, na Baraza la Mapinduzi Zanzibar, kuridhia mkataba kwa njia ya sheria ya nchi hizo, ili uweze kuwa na nguvu ya kisheria na kutekelezeka.
Ninavyofahamu mimi ni kwamba, Bunge la Tanganyika liliridhia mkataba huo, Aprili 25, 1964, kabla ya Muungano kutangazwa hapo Aprili 26, 1964.
Sina hakika kwa upande wa Zanzibar, kama Baraza la Mapinduzi lilikaa na kuridhia; lakini hata kama halikukaa wakati huo, dosari hiyo inatibiwa na Baraza la Mapinduzi kupitisha Sheria ya Muungano uitwayo “Zanzibar and Tanganyika Law” (kwa kifupi Sheria ya Muungano), kwa kuzingatia yote yaliyomo kwenye Mkataba wa Muungano.
Sina ugomvi juu ya uhalali wa Muungano, na ningependa kuona ukiendelea kuwapo. Tatizo nilionalo mimi ni kupotoshwa na kuvurugwa kwa muundo wa Muungano uliokusudiwa.
Tunafahamu, Muungano uliofikiwa na kuhalalishwa mwaka 1964, Muundo na Masharti yake yamefafanuliwa vizuri kwenye Mkataba wa Muungano. Sina sababu kwa sasa kuyataja hapa, lakini nitamke tu kwamba, nchi hizi ziliungana kuweza kushirikiana kwa mambo kumi na moja tu ya kimuungano; na mambo mengine yote yasiyo ya kimuungano kuachwa kushughulikiwa c@
No comments:
Post a Comment