TRA: Mapato yanayokusanywa Zanzibar yanatumika Zanzibar
Na Hafsa Golo
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema inatekeleza majukumu yake Zanzibar, huku maofisa wake wakilazimika kuvumilia kejeli na maneno ya kashfa kutoka kwa baadhi ya wateja.Ofisa wa Elimu kwa walipa kodi wa Mamlaka hiyo ofisi ya Zanzibar, Saleh Haji alielza hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Gulioni.
Alisema baadhi ya watu wakiwemo wafanyabiashara wamekuwa wakiiona TRA kama adui wa uchumi wa Zanzibar, kwa kuhamisha fedha kupelekwa bara.
Alifahamisha kuwa ipo kasumba iliyojengeka miongoni mwa jamii ambayo sio ya kweli kuwa TRA Zanzibar makusanyo ya fedha inayoyafanya Zanzibar inayapeleka Tanzania bara.
“Wananchi wanauelewa mdogo dhidi ya TRA kwa kuonekana kuwa makusanyo ya fedha wanayoyafanya Zanzibar yanakwenda serikali ya Muungano, jambo ambalo halina ukweli”,alisema ofisa huyo.
Aidha alifahamisha kuwa ufahamu huo mbaya umekuwa ukiwasababishia kukumbana na maneno mbali mbali ya kashifa, kejeli na kuonekana kama wasaliti wanapotekeleza wajibu wao.
Ofisa huyo aliwatoa hofu wananchi wa Zanzibar kuwa TRA haisafirishi
hata senti tano kwenda Tanzania bara, ambapo makusanyo ya Zanzibar yamefunguliwa akaunti maalum katika benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ).
Saleh alifahamisha kuwa msimamizi wa fedha zinazokusanywa na TRA Zanzibar ni katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha Uchumi na Mipango ya Maendeleo kutoka serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Baada ya kukamilika kwa utaratibu wa fedha tunazozikusanya kila mwisho wa mwezi huishia katika mfuko wa hazina wa Zanzibar, huu ndio ukweli hakuna fedha zinazokwenda Tanzania bara”,alisema ofisa huyo.
Alisema kasumba mbaya zinazofanywa dhidi ya TRA zimekuwa zikisababisha kushuka kwa mapato kwani baadhi ya wafanyabiashara wanakwepa wakidhani fedha hizo huishia Tanzania bara.
Ofisa huyo alisema kuwa jitihada kubwa zinahitajika kuchukuliwa katika kuielimisha jamii ya Zanzibar ili iweze kuelewa kwa undani utekelezaji wa majukumu ya TRA visiwani hapa na kuondokana na mitazamo na fikra potofu.
“Nawasihi wananchi tubadilishe fikra kwa kuwa na mtazamo chanya dhidi ya Mamlaka na mapato inayoyakusanya, kejeli na maneno mabovu hayatatufikisha katika harakati za kimaendeleo ambazo zinahitajiwa na wananchi wote”,alisema.
Aliishauri serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuliweka bayana suali la mapato ya TRA Zanzibar kwa kuwafahamisha wananchi matumizi ya fedha hizo.
No comments:
Post a Comment