| MCT yawaonya wanahabari kuhusu ‘Lulu’ |
Ibrahim YamolaBARAZA la Habari Tanzania (MCT), limewaasa waandishi wa habari kuzingatia maadili ya kazi yao hasa wakati huu wa kuripoti kesi inayomhusu Elizabeth Michael ‘Lulu’. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili wa MCT, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo alisema kuwa wadau wa tasnia ya habari wamekuwa wakimuhukumu moja kwa moja Lulu kuwa ndiye aliyemuua Steven Kanumba. “Kwa mjibu wa sheria na maadili ya uandishi wa habari mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa mpaka atiwe hatiani na mahakama,” alisema Jaji Mihayo na kuongea: “MCT inasikitishwa na baadhi ya vyombo vya habari kwa ukiukwaji wa maadili uliojitokeza wakati vikiripoti kuhusu kifo cha Kanumba, vimemuhukumu Lulu kuwa ameua kinyume na maadili ya kazi yao.” Jaji Mihayo alisema kuwa MCT kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa matamko yanayowakumbusha wanahabari kujiepusha na uandishi wa habari au vichwa vya habari vinavyohukumu. “MCT inatambua fika kesi zilizoko mahakamani ni kivutio kwa umma kutaka kujua kinachopendelea ili kuona haki ikitendeka na pia wanahabari wana haki ya kujua na kuripoti yanayojiri huko na katika vyombo vingine vya sharia,” alisema Jaji Mihayo na kuongeza: “Wanahabari ni lazima watambue kuwa kuna taratibu na makubalianao ya kijamii juu ya namna taarifa zinavyopaswa kuripotiwa ili kutowadhuru watu wengine.” Naye Katibu Mkuu wa (MCT), Kajubi Mukajanga alisema kuwa mwandishi wa habari ana uwezo wa kuifanya jamii ikaamini na kumfikiria Lulu moja kwa moja kuwa ndiye aliyemuua Kanumba jambo ambalo si kweli mpaka lithibitishwe mahakamani. Kuhusu taarifa ambazo zimekuwa zikienezwa na mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Kanumba kuwa zimesabishwa na Lulu alisema Mukajanga alisema kuwa MCT hawahusiki na mitandao hiyo. Mukajanga alisema atafuatilia kujua nini kilisababiaha kuwepo kwa usiri kwa polisi kutotoa taarifa ya wapi Lulu alitakiwa kufikishwa mahakamani ili waandishi wa habari wapate nafasi ya kufanya kazi |
Ibrahim Yamola
No comments:
Post a Comment