Thursday, 10 November 2011

Ni mvutano zaidi NCCR-Mageuzi

 
Mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia
Kundi linalomuunga mkono mwenyekiti wa Chama Cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia limeibuka na kudai kuwa mpango wa kutaka kumpindua kiongozi huyo hautafanikiwa kwa kuwa umefanywa na wanasiasa “Mazingaombwe”
Kadhalika, kundi hilo limeweka wazi mipango ya kufanya mapinduzi ya kuondoa uongozi wa juu ilivyokuwa imesukwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa jimbo la Kinondoni, Hemed Msabaha, ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Kafulila alisema, kamwe mipango ya kumng’oa Mbatia haitafanikiwa kwa kuwa yupo kwa mujibu wa Katiba.
Alisema Kafulila hana ubavu wa kumpindua Mbatia kama alivyotaka kufanya na kumfanisha na mwanasiasa “mazingaombwe” ambaye anafikiri vitu ambavyo hawezi kuvitenda.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Kafulila aliwahi kumshirikisha katika mipango yake ya kumung’oa Mbatia na alimwambia lengo lake ni kutaka chama hicho kiongozwe na mtu kutoka mkoa wa Kigoma.
Aliongeza kuwa Kafulila alimhakikishia kwamba baada ya kufanya mapinduzi hayo, alitaka awe mwenyekiti na hivyo mkoa wa Kigoma nao kupata uongozi wa juu kama ilivyo kwa vyama vingine kama Chadema ambacho kinaoongozwa na mtu kutoka mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa Msabaha, Kafulila alitaka kumpindua Mbatia ili yeye awe mwenyekiti, kwa kuwa kuanzisha chama kipya mchakato wake ni mrefu na huenda asingefanikiwa kukianzisha.
Hata hivyo, alisema Mbatia alinusurika kung’olewa kwa kuwa hoja ya msingi ambayo walitarajia ingeungwa mkono na wajumbe, iliwasilishwa na mtu ambaye alikuwa na kashfa ndani ya chama. Msabaha hakumtaja mtu huyo.
Mgogoro ndani ya NCCR-Mageuzi uliibuka mapema mwezi uliopita, ambapo kundi linaloongozwa na Kafulila liliibuka na kutaka Mbatia atimuliwe.
Kafulila na wenzake wanamtuhumu Mbatia kuwa ni CCM B, mtu ambaye ni mnafiki na ambaye hana mpango wa kukiimraisha chama hicho.
Hata hivyo, zoezi hilo halikufanikiwa ingawa kundi la akina Kafulila lilimpa Mbatia siku 21 ajieleze kuhusu tuhuma zinazomkabili.
Kafulila alipoulizwa juu ya tuhuma hizo, alisema sio za kweli na kwamba zinalenga kupindisha ukweli ya kwamba Mbatia anatakiwa kuondoka madarakani kwani ameshindwa kukisaidia chama hicho kusonga mbele.
Alikanusha madai kuwa yeye anataka nafasi ya uenyekiti na kuongeza kuwa mtu ambaye ameonyesha nia ya kuiwania ni Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali pamoja na aliyewahi kugombea urais kupitia chama hicho, Hashim Rungwe.
Alisisitiza kuwa baada ya siku 21 kumalizika, ikiwa Mbatia atashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha atalazimika kukaa pembeni na nafasi hiyo kuongozwa na mtu mwingine ambaye anaweza kutoa mchango mkubwa kwa chama.

No comments:

Post a Comment