| Korti yapiga 'stop' Ligi Kuu Zanzibar |
| ||
MAHAKAMA ya Mkoa wa Vuga, imeizuia Ligi Kuu ya Zanzibar baada ya wakongwe wa soka, Malindi FC kupeleka madai yao katika mahakama hiyo wakipinga kushuka daraja msimu huu. Mbali na kusimamisha ligi, Malindi wamekiuka kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa, ZFA la kupeleka masuala ya soka mahakamani wakati walipaswa kuwasilisha shauri hilo Baraza la Michezo Zanzibar, BMZ. Malindi wameteremka daraja ikiwa ni kati ya timu tatu zilizoaga ligi hiyo wakiwemo Duma na Madungu za Pemba. Kwa mujibu wa barua iliyotiwa saini na Hakimu wa mahakama hiyo, Hamisa Suleiman Hemed, imekitaka Chama cha Soka Zanzibar, ZFA, kusimamisha ligi hadi hapo mahakama itakaposikiliza shauri la Malindi na kutoa uamuzi wake. Amri hiyo ya mahakama iliyotolewa Novemba 1 mwaka huu, na hakimu huyo pia imezifika klabu zote za Zanzibar kwa ajili ya utekelezaji na kuondoa usumbufu wa kufika kiwanjani. “Shauri hili liko mahakamani hadi hapo litakopopata ufumbuzi na ndipo ligi hiyo itaendelea,” alieleza hakimu huyo. Kesi hiyo ya madai yenye namba 32/2011 inawahusisha viongozi wa ZFA inadai wamekiuka kanuni na katiba katika uendeshaji wa ligi hiyo kwa kuendesha ligi kwa mkondo mmoja kinyume na kanuni yake inayotaka ichezwe mikondo miwili. Malindi ilieleza matokeo yote ya msimamo wa ligi hiyo ni batili na kuiomba mahakama itumie uwezo wake itafasiri kanuni na sheria ili haki iweze kutendeka ikiwemo Malindi kurejeshwa katika ngazi yake ya Ligi Kuu. Katika kesi hiyo, Malindi wanatetewa na wakili Rajab Abdallah Rajab. Viongozi wa ZFA wamethibitisha kupokea amri hiyo ya mahakama. Sambamba na hilo umoja wa klabu umelaani hatua hiyo ya Malindi kwenda mahakamani wakidai ni kinyume cha utaratibu wa soka duniani. Umoja huo chini ya mwenyekiti wake, Issa Gabriel, umeelezea kushtushwa na taarifa inayoitaka ZFA kusimamisha ligi kutokana na mmoja wao kwenda mahakamani. Kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha katiba ya ZFA, kinasema adhabu kali itatolewa kwa klabu mchezaji, mwalimu atakayepeleka suala la michezo mahakamani ikiwemo kufutwa kabisa katika medani za soka. Msemaji wa ZFA, Munir Zacharia alisema wao kama ZFA hawana wasiwasi na kesi hiyo kwani wanajua watashida. |

No comments:
Post a Comment