Ujenzi hoteli ya kitalii jirani na kituo cha mafuta wawashtua Wawakilishi
Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Hamza Hassan Juma
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hamza Hassan Juma, wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu meli iliyozama na kuua watu 203 katika mkondo wa Nungwi Septemba 10, mwaka huu katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani, Zanzibar.
Alisema ni jambo la kushangaza Serikali kuamua kumruhusu mwekezaji kujenga hoteli ya kitalii karibu na matenki ya mafuta bila kuzingatia kuwa eneo hilo kuna wananchi wanaishi na hatari kwa usalama wao.
“Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inatoa tahadhari nyingine kwa Serikali kuwa inaweza kutokea maafa mengine makubwa kama hatua za haraka hazitachukuliwa na Serikali katika mradi huo,” alisema Hamza ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi.
Alisema pamoja na wataalam wa mazingira kuzuia mradi huo, lakini mwekezaji ambaye ni mzalendo aliendelea na ujenzi wa hoteli hiyo ya Misali Beach Resort bila kuzingatia ushauri wa wataalam hao.
Hamza alisema hatua za tahadhari zinahitaji kuchukuliwa kwa sababu hoteli hiyo imejengwa jirani na matenki ya mafuta wakati eneo hilo kuna makazi ya watu na familia nyingi zinaweza kuathirika iwapo litatokea janga la moto.
Alisema Serikali lazima iheshimu na kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalam wa Idara ya Mazingira kabla mradi kupitishwa na taasisi za serikali kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake.
“Hoteli hii imejengwa kiubabe na haikufata ripoti za wataalam isipokuwa nguvu ya pesa ilitumika na likitokea la kutokea, kamati inasema Serikali itawajibika,” alisisitiza.
Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE, Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli hiyo, Aman Ibrahim Makungu, alikanusha shutuma hizo na kueleza mradi huo umezingatia taratibu zote za kisheria kabla ya ujenzi kufanyika.
Alisema utekelezaji wa mradi huo ulianza baada ya kupatiwa hati miliki ya ardhi na mradi huo kupitishwa kuanzia ngazi ya halmashauri, na kitengo cha uwekezaji Zanzibar (Zipa) baada ya kuruhusiwa na wataalamu wa mazingira Zanzibar.
Alisema mradi huo umegharimu dola milioni mbili za Marekani na umetoa ajira kwa vijana 80 na uongozi wa hoteli hiyo umeshangazwa na malalamiko ya kamati hiyo kuwa mradi huo unahatarisha usalama wa maisha ya wananchi wanaoishi karibu na mradi huo.
Hata hivyo, alisema hivi karibuni Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff Hamad, alitembelea mradi huo na lilijitokeza suala hilo lakini aliwataka wataalamu wa mazingira kushughulikia malalamiko hayo na watoe mapendekezo yao.
“Wataalamu wametoa mapendekezo badala ya hoteli kuezekwa makuti, iezekwe bati ili kuimarisha usalama na tayari mapendekezo hayo yameshaanza kufanyiwa kazi,” alisema Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, alisema ameshangazwa na kamati hiyo kuhoji usalama wa mradi huo wakati hoteli ya Mtoni Marine imejengwa karibu na vituo mbalimbali vya kuhifadhia mafuta.
Katika siku za karibuni limeibuka wimbi la baa kuchomwa moto na watu wasiojulikana.
No comments:
Post a Comment