Wednesday, 6 July 2011


Marufuku kunyanyasa wafanyakazi

Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika, Haroun Ali Suleiman
MARUFUKU KUNYANYASA WAFANYAKAZI
Wizara ya kazi, uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika, Haroun Ali Suleiman amesema waajiri watakaowanyanyasa wafanyakazi katika sehemu za watachukuliwa hatua za kinidhamu kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mikataba ya kimataifa.
Haroun alisema hayo wakati akijibu swali lililoulizwa na mwakilishi wa viti maalumu wa chama cha (CUF) Kazija Khamis Kona aliyemuuliza waziri kama anafahamu kuwa wapo waajiri ambao wananyanyasaji watumishi wao,ikiwemo kuwaajiri bila ya kuwapa mikataba ya kudumu.
Waziri Haroun alikiri kuwepo kwa tatizo hilo zaidi katika sekta za uwekezaji ikiwemo katika hoteli za kitalii ambapo ukiukwaji wa mikataba ya kazi na unyanyasaji kwa ujumla upo wa hali ya juu.
‘Mheshimiwa spika hilo tatizo lipo na nalifahamu sana lakini serikali itachukuwa hatua za kinidhamu kwa waajiri watakaoendesha vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kuwafukuza ovyo wafanyakazi wake’alisema Haroun.
Akifafanua zaidi Haroun alisema sheria nambari 11 ya mwaka 2005 inakataza kabisa kuwepo kwa aina yoyote ya vitendo vya unyanyasaji katika sehemu za kazi na kuongeza sheria za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake.
Alisema katika kukabiliana na vitendo hivyo,wizara imesema itafanya ukaguzi katika sehemu za kazi pamoja na kusikiliza malalamiko ya watumishi katika kukabiliana na tatizo hilo.
Aidha alisema wizara ya kazi inashirikiana pia na shirikisho la vyama huru vya wafanyakazi (ZATUC) katika kupambana na vitendo hivyo kuona wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira mazuri ya kazi.
‘Ndiyo agizo la shirika la kazi duniani ILO linavyoagiza….mazingira ya kazi mazuri pamoja na kazi zenye heshima lazima yazingatiwe’alisema Haroun.
Haroun alisema wizara imekataa kuongezwa kwa mikataba ya wafanyakazi wa nje katika hoteli za kitalii ikiwemo ya Kempisky,Lagema baada ya kubainika maofisa hao kuhusishwa na vitendo vya unyanyasaji kwa wafanyakazi wake.
Kumejitokeza kwa malalamiko mbali mbali katika sekta ya utalii ambapo wafanyakazi wanadai kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kutimuliwa kazi na kushindwa kufungishwa mikataba ya kudumu.
Alisema ni marufuku kwa waajiri kuajiri wafanyakazi na kushindwa kuwapatia mikataba ya kudumu kama sheria za kazi zinavyoelekeza nchini.
MAJENGO YA SMZ KUFANYIWA UKARABATI
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imesema itajenga majengo ya ofisi zake ya kisasa na kuachana na majengo yaliyochakaa ambayo yapo katika hali mbaya ya uchakavu zaidi katika eneo la Mji Mkongwe Mjini hapa.
Hayo yalisemwa na waziri wa nchi ofisi ya rais,fedha uchumi na mipango ya maendeleo Omar Yussuf Mzee wakati akitoa ufafanuzi mbele ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kuhusu mpango wa Serikali wa kujenga majengo ya kisasa ya ofisi zake.
Alisema ni kweli majengo mengi yanayotumiwa na ofisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliopo mji mkongwe yamechakaa na hivyo mengine kuhatarisha usalama wa wafanyakazi pamoja na raia wengine.
Omar alisema katika mpango huo Serikali inakusudia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 5.3 kujenga ofisi za Serikali katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba.
Aliyataja baadhi ya majengo ambayo ofisi za Serikali zimelazimika kuhama kutokana na majengo hayo kuwa tishio kwa usalama wa wananchi ikiwemo wizara ya mawasiliano na miundo mbinu liliopo Forodhani.
Aidha alisema jengo la ofisi ya wizara ya katiba na sheria liliopo Shangani lipo katika hali mbaya,kutokana na uchakavu wake.
‘Baadhi ya wizara tayari tumezipatia majengo…..kuna utawala bora pale tumewapa jengo la mamlaka ya mapato (ZRB) pamoja na wizara ya wanawake na watoto’alisema Omar.
Alisema uongozi wa awamu ya rais Dk Ali Mohamed Sheni imeazimia na kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanafanya kazi zao katika mazingira mazuri ikiwemo katika majengo bora yenye hadhi.
Bado baadhi ya ofisi nyingi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinatumia majengo yaliopo katika Mji Mkongwe wa Zanzibar ambayo yamechakaa huku mengine yakiwa hayana haiba nzuri.
Baadhi ya wizara ambazo zinatumia majengo ya kisasa yalijengwa na serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ni, wizara ya elimu yenye ofisi zake huko Mazizini, pamoja na wizara kazi,uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika na baraza la wawakilishi wanaotumia jengo la kisasa liliopo Chukwani nje kidogo ya mji wa Unguja.
MABILIONI YA JK NA AK KUANZA KUTOLEWA
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imeanza kutoa mikopo kwa wajasiriamali katika mfuko maarufu kwa jina la mabilioni ya JK na AK Zanzibar baada ya kusitishwa kwa zoezi hilo kutokana na kuzorota kwa urudishaji wa mikopo hiyo.
Hayo yalisemwa na waziri wa kazi,uwezeshaji wananchi kiuchumi na ushirika Haroun Ali Suleiman wakati akijibu swali la mwakilishi nafasi za wanawake kutoka CUF Bikame Yussuf Hamad aliyetaka kujuwa lini mikopo ya JK na AK itaanza kutolewa kwa wajasiriamali Zanzibar.
Haroun alisema ni kweli mikopo hiyo ilisitishwa baada ya kujitokeza kwa kasoro mbali mbali ikiwemo wakopaji kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
‘Napenda kuwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba mikopo kwa ajili ya wajasiriamali maarufu kwa jina la JK na AK tayari imeanza kutolewa kwa walengwa baada ya marekebisho ya kasoro mbali mbali’alisema Haroun.
Alitaja baadhi ya kasoro zilizorekebishwa ikiwemo walengwa kupewa mafunzo kuhusu madhumuni ya fedha hizo ambazo ni kwa ajili ya kuendeleza miradi yao.
Alisema wakopaji wamekuwa wakipatiwa elimu ambapo wanatakiwa kujuwa kwamba mikopo wanayopewa inatakiwa kurudishwa na sio sadaka kutoka serikalini.
‘Elimu hiyo tumekuwa tukiwaambiya…unajuwa wengine walidhani kwamba fedha wanazopewa ni sadaka na hawalazimiki kuzirudisha ili ziweze kuwakopesha watu wengine’alisema Haroun.
Alisema mazingira hayo na dhana hiyo kwa kiasi kikubwa ndiyo iliyowafanya baadhi ya wakopaji kushindwa kurudisha fedha walizokopeshwa hatua ambayo ilipekekea kusitishwa kwa mikopo hiyo kutoka kwa taasisi za fedha.
Alisema wizara kabla ya kuanza kazi ya kutowa fedha hizo ilikaa pamoja na maofisa wa Benki kuu (BOT),Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) pamoja na wajasiriamali wenyewe.
Alisema jumla ya sh.Bilioni 3.6 zilitengwa kwa ajili ya kuwakopesha wajasiriamali mbali mbali Unguja na Pemba kwa ajili ya kuendesha miradi yao na kuondokana na tatizo la umasikini.
Hata hivyo alisema tatizo la baadhi ya wajasiriamali kushindwa kurejesha mikopo hiyo kwa kiasi kikubwa imeathiri maendeleo ya mfuko huo malengo yake.
Haroun alisiitiza na kusema fedha zinazotolewa kwa ajili ya wajasiriamali mbali mbali hakuna upendeleo kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo na dhamira ya mifuko hiyo.
Waziri alikuwa akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na mwakilishi wa jimbo la MTAMBWE kwa tiketi ya CUF, Salim Abdalla Hamad aliyesema kwamba kuna upendeleo katika utoaji wa mikopo hiyo ambayo huwashirikisha masheha pamoja na wakuu wa wilaya.
Haroun alisema hakuna kitu kama hicho kwani dhamira ya mfuko huo kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi kutoa mikopo kwa wananchi kwa lengo la kupunguza umasikini na sio kwa malengo ya kisiasa.
MASLAHI YA WAFANYAKAZI KUANGALIWA
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inakusudia kuboresha maslahi ya madaktari Unguja na Pemba na kuweka mazingira mazuri ya utendaji katika kada hiyo ili kupunguza tatizo la madaktari kuondoka nchini.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya Juma Duni Haji wakati akiwasilisha makadirio mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2011-2012 hapo katika baraza la wawakilishi.
Duni alikiri kuwepo kwa wimbi la madaktari kuhama na kwenda sehemu nyengine kutafuta maslahi bora ya kazi hiyo,kitendo ambacho kinarudisha nyuma juhudi za Serikali kukabiliana na tatizo la upungufu wa madaktari.
‘Mheshimiwa spika kwa mwaka wa fedha 2011-2012 tunakusudia kuimarisha maslahi ya madaktari wetu pamoja na wauguzi ambapo lengo ni kudhibiti kuondoka kwa madaktari kwenda nje kutafuta maslahi bora’alisema.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kusomesha madaktari hao hivyo kitendo cha kuondoka kinaitia hasara kubwa Serikali.
Aidha Duni alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na mikakati yake ya kudhibiti mripuko wa maradhi mbali mbali hatari ambayo huathiri afya ya wananchi.
Katika mwaka huu wa fedha Serikali inakusudia kupambana na maradhi ya Kichocho,Minyoo,matende pamoja na mabusha Unguja na Pemba ambapo katika siku za hivi karibuni,maradhi hayo yameonekana kujitokeza tena.
Katika mpango huo na utekelezaji wake,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kudhibiti maradhi hayo na hatimaye kuyatokomeza kabisa pamoja na kukinga na kuzuwia ulemavu unaotokana na maradhi hayo.
Duni alisema hadi kufikiya kipindi cha Julai 2010 hadi Machi 2011,jumla ya watu 2,025 walifanyiwa uchunguzi dhidi ya ugonjwa wa kichocho ambapo kati ya hao 1,684 sawa na asilimia 83% waligundulikana na maradhi hayo.
Alisema wizara ya afya katika kudhibiti maradhi yakichocho ambayo huathiri zaidi watoto wa shule,inakusudia kufanya zoezi la kupima afya za wanafunzi katika shule za Unguja na Pemba.
Katika mikakati hiyo wizara inakusudia pia kuyaharibu mazalio ya makonokono ambao ndiyo wanaosababisha maradhi ya kichocho.
Aidha Duni alisema mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuifanya hospitali ya Mnazi mmoja kuwa ya rufaa yenye kutibu maradhi mbali mbali.
Alisema uamuzi huo wa kuifanya hospitali ya Mnazi mmoja kuwa ya rufaa kwa kiasi kikubwa itapunguza tatizo la wananchi wengi kwenda Tanzania Bara na wengine nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta matibabu mengine zaidi.
‘Napenda kuliarifu baraza lako tukufu kwamba mpango wa kuifanya hospitali ya Mnazi mmoja kuwa ya rufaa ,wizara tayari imepokea jumla ya madaktari 13 waliohitimu katika vyuo mbali mbali vya nje ya nchi’alisema Duni.
Duni aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba hospitaliya Mnazi mmoja itaendelea kutoa huduma za afya kwa akinamama wajawazito ili kuona huduma hiyo inakuwa salama.
Alisema jumla ya akinamama wajawazito 7,564 walilazwa katika hospitali ya Mnazi mmoja kati ya hao 5,593 walijifunguwa kwa njia ya kawaida na 1,322 walijifunguwa kwa njia ya upasuaji.
‘Mheshimiwa wizara yangu inajiandaa kufanya uchunguzi kujuwa kwa nini kuna idadi kubwa ya akinamama wajawazito wanajifunguwa kwa njia ya upasuaji’alisema Duni.
Mapema Duni aliwaambiya wajumbe wa baraza la wawakilishi kwamba lipo tatizo kubwa la kuongezeka kwa wagonjwa wa akili nchini.
Alisema jumla ya wagonjwa 790 walipatiwa huduma za kulazwa miongoni mwao wagonjwa 350 walikuwa wanaume na wanawake ni 440.
Alikiri kuongezeka kwa kasi ya maradhi hayo na kusema matumizi ya madawa ya kulevya miongoni mwa vijana mbali mbali ni chanzo kikuu cha maradhi hayo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika mipango ya kuimarisha hospitali kuu ya wagonjwa wa akili iliopo Kidonge chekundu kuona inatoa matibabu ya uhakika kwa wagonjwa wa akili.
Duni aliliomba baraza la wawakilishi kwa mwaka wa fedha 2011-2012 kuidhinisha jumla ya sh.Bilioni 13,227,000,000. kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida na maendeleo.

No comments:

Post a Comment