Tuesday, 5 July 2011

Aga Khan ni wababaishaji?

UKODISHWAJI WA MAJENGO YA SMZ

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema uwezo wa Taasisi ya Aga
Khan Development kwa Zanzibar ni mdogo katika kuhudumia miradi mikubwa
ya Uwekezaji.Akijibu swali la nyongeza katika Baraza la Wawakilishi jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.
Mwinyihaji Makame Mwadini alisema “Mheshimiwa Spika ni kweli kwamba
uwezo wa Aga Khan kwa Zanzibar ni mdogo”
Dk Mwinyihaji alisema Baraza la Mapinduzi baada ya kutafakari kwa kina
maombi ya Kampuni ya Aga Khan liliamua kutompa fursa ya ukodishwaji wa
majengo aliyokuwa ameyaomba.
Majengo yalioombwa ni iliyokuwa Makao makuu ya Wizara ya Elimu, Jengo
la Mambo Msiinge na Starehe Club katika eneo la Ras Shangani. Kampuni
ya Aga Khan Development imekodishwa jingo la zamani la simu (sasa Serena Inn).
Waziri Mwinyihaji aliwaeleza Wajumbe wa Baraza kwamba Aga Khan ilipewa
eneo la ardhi katika Kijiji cha Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja
kwa ajili ya uwekezaji wa Hoteli,lakini kwa zaidi ya miaka 25
ameshindwa kuliendeleza eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Aga Khan amepewa eneo la Mangwapwani,lakini
hajaliendeleza, wananchi wanakosa eneo la kilimo kwa sababu yeye
amehodhi eneo kubwa” Aliliambia Baraza Waziri huyo.
Katika jibu la msingi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha,Uchumi na
Mipango ya Maendeleo,Omar Yussuf Mzee alisema sheria ya nchi, ardhi ni
mali ya Umma,hivyo, Serikali wakati wote huwa inakodisha eneo na sio
kuuza.
Katika swali la msingi, Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani (CUF),Hija Hassan
Hija alitaka kujua ni njia zipi alizotumia Mwekezaji kupata eneo la
Mambo Msiinge, Waziri Omar alisema sheria zilizotumika katika
kukodisha eneo hilo ni sheria ya Ardhi namba 12 ya mwaka 1992 na
limekodishwa kwa mita za mraba 0.42 kwa dola za Kimarekani 10,000 kwa
mwaka.
KILIMO
Waziri wa Kilimo na Maliasili,Mansoor Yussuf Himid amesema upungufu
mkubwa na ukaukaji wa maji uliojitokeza katika maeneo mengi ya mabonde
umechangiwa na uharibifu wa vianzio vya mito na chemchem.
Akijibu swali la Mwakilishi wa Viti maalum(CUF),Mwanajuma Faki Mdachi
aliyetaka kujua tatizo la upungufu mkubwa wa maji katika mabonde ya
kilimo, Waziri Mansoor alisema ujenzi usiozingatia mipango miji pamoja
na shughuli za kibinaadam umechangia hali hiyo.
Waziri Mansoor alisema ukataji miti kwa uchomaji makaa na kuni kwa
lengo la kujipatia kipato na hata kazi za kilimo huchangia kuharibu
kivuli cha njia za mito.
“Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya tabia nchi yamechangia kupungua kwa
upatikanaji wa mvua ambao una mahusiano makubwa na ukaukaji wa mito”
Alisema Waziri Mansoor.
Waziri huyo alisema zao la mpunga kwa kawaida huwa linahitaji maji
mengi sana kwa hivyo hali ya upungufu wa maji inachangia kiasi kikubwa
cha upungufu wa mavuno ya mpunga.
“Mheshimiwa Spika,napenda kulitarifu Baraza lako kwamba Wzara yangu
inamashirikiano makubwa ya kitaalam na Wizara ya Ardhi,Maji, Nishati
na Maendeleo ya Makaazi” Alisema Waziri huyo.
Waziri huyo alisema kimsingi wamekuwa wakiwasiliana na Mamlaka ya Maji
katika hatua za awali za uchunguzi wa upatikanaji wa maji pamoja na
kushauriana namna ya kufanikisha kazi za uchimbaji kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment