Sunday, 12 June 2011

                                      TISHIO LA TETEMEKO LA ARDHI
                                                            Zanzibar

 Serikali imewataka wananchi wa Zanzibar kuchukua tahadhari kwa kipindi hiki kufutia kuwepo kwa uwezekano wa kutokea kwa tetemeko la ardhi baada ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam kutokea mtikisiko siku ya Ijumaa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar ambayo imesainiwa na Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dk Khalid Mohammed imesisitiza ulazima wa wananchi kutoa taarifa kwa Mamlaka zinazohusika wanapoona jambo si la kawaida katika shughuli zao.

Dk. Khalid amesema taarifa za kitaalamu zinaonesha kuwa upo uwezekano wa tetemeko hilo kutokea tena, hivyo ingawa tetemeko hilo halikuripotiwa katika maeneo ya Zanzibar kutokana na umbali uliopo kutoka eneo lilipoanzia tetemeko hilo hadi Zanzibar.

Amesema Juni 10 mwaka huu saa 5:28 asubuhi lilitokea tetemeko katika bahari ya Hindi umbali wa Kilomita 52 Kusini Mashariki ya Dar es Salaam na Kilomita 105 Kusini Mashariki mwa Zanzibar likiwa na ukubwa wa kipimo cha Richater 4.8 ambalo lilitokea katika kina cha kilomita 10 chini ya bahari.

Amesema bado Zanzibar ipo katika tishio la kupata tetemeko hilo endapo litatokea tena, hivyo Serikali inawataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kipindi hiki na kutoa taarifa kwa vyombo vinavyohusika.

Katibu Mkuu huyo amesema Serikali inaendelea kufuatolia mwenendo wa matukio hayo kupitia Taasisi na vyombo vinavyohusika na itakuwa inatoa taarifa mara kwa mara. Dk Khalid alisema Serikali inaendelea kusisitiza kwamba wananchi waendelee kusikiliza na kufutialia taarifa na maelekezo yatakayotolewa juu ya suala hili na kuchukua hatua zinazostahiki.
                                                                IMETOLEWA NA:

                                         IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR

                                                                     12/06/2011

No comments:

Post a Comment