Marekani kuisaidia Zanzibar
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad akizungumza na ujumbe wa Shirika la Kimataifa la misaada la Marekanii (USAID) Ofisisni kwake Migombani.Kulia ni kiongozi wa ujumbe huo Robbert Cunnane
Na Salma Said
MAKAMU wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema azma ya Marekani kuisaidia Zanzibar itasaidia sana katika hatua zakukuza maendeleo nchini.
Serikali ya marekani imedhamiria kuisaidia Zanzibar katika sekta ya kilimo cha uwagiliaji maji na uhifadhi wa chakula jambo ambalo litasaidia sana hasa wakati huu, ambapo Zanzibar imo katika jitihada za kujitosheleza kwa chakula.
Maalim Seif amesema hayo leo ofisini kwake Migombani, wakati alipokutana na ujumbe kutoka Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani (USAID).
Alisema uamuzi wa huo wa kuisaidia Zanzibar kutasaidia katika mradi wa kilimo cha umwagiliaji, hususan katika zao la mpunga ni muhimu kwa vile Serikali tayari imetenga kiasi cha hekta nane kwa ajili ya kuendeleza kilimo hicho, ili kupunguza kasi ya uagiziaji wa mchele kutoka nje.
Alisema wakati huu nchi inakabiliwa na mfumko mkubwa wa kupanda kwa bei za bidhaa ikiwemo mchele, kutokana na uzalishaji duni wa chakula hicho tofauti na mahitaji yaliopo.
Alisema baadhi ya maeneo ya nchi kama vile Micheweni,Mkoa wa Kaskazini Pemba, hali ni mbaya kukiwa na ongezeko kubwa la utapia mlo kwa watoto.Akizungumzia uzalishaji wa mbogamboga uliomo katika mradhi huo, Maalim Seif alisema ni muhimu sana kwa vile baadhi ya Mahoteli ya kitalii yaliopo, hutegemea zaidi bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Hata hivyo Makamu wa Kwanza wa Rais, aliuomba ujumbe huo kuzingatia suala la kuipatia Zanzibar kasma yake,kama hatua ya kuepuka “kusahauliwa” wakati wautekelezaji wa mradi huo unaohusisha sehemu ya pili ya Muungano.
Alisema suala la Kilimo sio la Muungano, hivyo ni vyema Zanzibar ikatengewa kasma yake kama nchi, ili kuepuka sintofahamu wakati wa utekelezaji.“Kuna masuala ya Muungano na yasio ya Muungao, Kilimo sio suala la Muuungano, Zanzibar ina mambo yake , ni vyema ikapewa kasma yake kuepusha kusahauliwa wakati wa utekelezaji”, alisema.
Akizungumzia mradi wa elimu utakaohusisha matumizi ya Teknolojia ya Komputa maskulini (education for 25 th Century),alisema ni muhimu katika karne hii ya 21wakati Dunia ikiwa imejikita katika matumizi ya teknoljia ya Habari na Mawasiliano.
Alisema hatua hiyo italeta mustakbali mzuri na faida kubwa kwa kizazi kijacho.
Kuhusiana na mradi wa Afya, Maalim Seif alipongeza Shirika hilo kutokana na msaada mkubwa katika udhibiti wa ugonjwa wa Malaria, kushuka hadi kufikia asilimia moja.
Alishauri mradi huo kuendelezwa kwa kuzingatia kuwa hivi sasa kumekuwepo na ongezeko kubwa la mazalia ya mbu, wakiwemo wale wanaosababisha Malaria.
Katika hatua nyingine Maalim Seif, aliliomba shirika hilo kutupia macho changamoto mbali mbali zinazoikabili Zanzibar zikiwemo za uharibifu wa kimazingira, zinazotokana na binaadamu.
Akitolea mfano, Maalim Seif alisema kumekuwepo wimbi kubwa la ukataji wa mikoko kisiwani Pemba, hatua inayopelekea maji ya bahari kupanda na kumega maeneo ya ardhi.
Alisema Serikali kwa upande wake imekuwa ikichukua juhudi za kuwashajiisha wananchi kupanda miti kwa wingi ili kuepusha uwepo wa jangwa au mmong’onyoko wa ardhi.
Mapema Kiongozi wa ujumbe huo kutoka Shirika la misaada la Kimataifa la Marekani (USAID) Robbert Cunnane, alisema Shirika hilo linalenga kusaidia Zanzibar katika miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji, uzalishaji wa mboga mboga pamoja na huduma za Afya.
Alisema mradi wa elimu,utatoa fursa kwa walimu wa Zanzibar kupata mafunzo na hatimae kuweza kufundisha wanafunzi kupitia mtandao.Alisema matumizi ya vyandarua vyevye dawa yataendelezwa kwa kuzingatia kuwa mbali na kuwa kinga lakini pia vinaua mbu na hivyo kupunguza hatari ya kuongezeka kwa ugonjwa wa Malaria.Alifafanua kuwa katika mradi wa kilimo cha umwagiliaji maji pia utahusisha na kilimo cha zao la mahindi.
Katika hatua nyengine Maalim Seif Sharrif Hamad, amesema Serikali inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha wastaafu wake wanathaminiwa na kutunzwa vyema.
Amesema mchango wa wastafu katika maendeleo ya nchi kiuchumi, kijamii na kiulinzi ni mkubwa, hivyo ni vyema wakathaminiwa kutokana na kazi walioifanya.
Maalim Seif amesema hayo leo ofisini kwake Migombani, wakati alipozungumza na Kamati ya Jumuiya ya wastaafu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, waliopo Zanzibar.
Amesema kwa kutambulia hilo Serikali itaendelea kutimiza wajibu wake wa kujenga mazingira mazuri kwao, ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango mkubwa walioutoa wakati wa utumishi wao.
Alisema ni jambo la huzuni na kusikitisha kuona mfanyakazi alietumikia Taifa kwa kipindi kirefu na kutunukiwa nyadhifa mbali mbali anataabika na kupoteza utu wake, baada ya kumaliza muda wake wa utumishi.
“Kuwaenzi na kuwajali ndio njia moja ya kuwashukuru na kuthamini mchango wao mkubwa waliojitolea katika kulihudumia Taifa”, alisema.
Alisema Serikali itajitahidi kutafuta njia za kutatua baadhi ya matatizo yao yanayowakabili, sambamba na kuitaka Jumuiya hiyo kuwasiliana na Makampuni na Mashirikia ya Simu nchini ili kupata msukumo.
Aidha alishauri kuwashajiisha wafanyakazi wenye sifa, kujiunga na Jumuiya baada ya kustaafu, pamoja na kufanya kazi ya ziada ya kusaka wanachama ili kukuza Jumuiya yao.
Mapema Katibu wa Jumuiya hiyo, Rashid Ali Juma, alisema Jumuiya yake inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo uwezo duni wa kifedha unapelekea kuzorotesha uendeshaji, ukosefu wa Ofisi, sehemu za kufanyia miradi mbali mbali pamoja na jengo kwa ajili ya kuuzia madawa.
Alisema ni lengo la Jumuiya hiyo kuwa na nguvu zaidi kwa kuongeza wanachama kutoka 552 waliiopo ili kuimarisha hali za maisha ya wastaafu pamoja na kuisaidia Serikali kutokana na miradi mbali mbali watakayowekeza.
Wakati huo huo, Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, ameitaka Jumuiya ya wachangiaji damu kwa hiari Zanzibar, kuwa na takwimu za uhakika ili kufahamu wachangiaji waliopo, aina ya makundi ya damu zao na wapi walipo, ili kurahisisha uchangiaji wa damu wakati wa dharura au majanga.
Maalim Seif alishauri Jumuiya hiyo kujitangaza zaidi na kuwaomba wafanyabiashara na wenye makampuni kutoa msukumo wa fedha ili Jumuiya iweze kujiendesha kwa ufanisi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Ofisi yake inaangalia uwezekano wa kuiunga mkono Jumuiya hiyo kupitia Tume ya Ukimwi Zannzibar (ZAC).
Nae Katibu wa Jumuiya hiyo, Bakar Hamad Masarawa, alimweleza Makamo wa Kwanza wa Rais, changamoto zinazokaibili Jumuia hiyo, ikiwa pamoja na ukosefu wa usafiri unaokwamisha juhudi za kuwafikia wanachama wake wakati wa dharura pamoja na ukosefu wa Ofisi na vitendea kazi.
Aliiomba Serikali kuijuimisha Jumuiya hiyo na NGO’s nyengine zinzopata michangao kutoka ZAC kwa kuzingatia kuwa Jumuiya hiyo iko mbele zaidi katika kutoa taaluma ya kujikinga na Ukimwi sambamba na kuelimisha jamii juu ya uhifadhi wa damu salama.

No comments:
Post a Comment