Sunday, 12 June 2011

Jamhuri ya Kiislam ya Iran imeanza utekelezaji wa makubaliano yake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Nyanja za maendeleo

Na Mwandishi wa MAELEZO Zanzibar.

Hatimaye Jamhuri ya Kiislam ya Iran imeanza utekelezaji wa makubaliano
yake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibat katika Nyanja za maendeleo
ikiwa ni miezi miwili baada ya ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd nchini humo.

Hahaman Ahmad, Balozi Mdogo wa Iran hapa nchini amesema kwamba
Serikali ya nchi yake tayari imeshatenga Dola za Marekani Milioni 1.5
kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo Zanzibar.

Katika mazungumzo yake na Waziri wa Kilimo na Maliasili wa Zanzibar,
Mansoor Yussuf Himid, Balozi Ahmad amesema wangependa kuona fedha hizo
zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ambapo ndio lengo la mkutano
wake na SMZ kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili.

“Mheshimiwa Waziri nimeleta kwako mwongozo wa matumizi ya fedha hizo,
bila shaka hautakuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi hiyo”
Alisema Balozi Ahmad.

Fedha hizo zitatumika katika kuimarisha Chuo cha Kilimo Kizimbani
Unguja, ununuzi wa Boti za kisasa zitakazoweza kutumika katika uvuvi
wa bahari kuu na utalii, mradi wa asali utakaohusisha pia kuwajengea
uwezo wafugaji katika kutafuta masoko.

Mbali na miradi hiyo, Balozi Ahmad amesema fedha hizo pia zitatumika
kununua matrekta aina ya Power Tiller 50 kwa ajili ya kusaidia
wakulima Visiwani Zanzibar.

Waziri Mansoor ameihakikishia Serikali ya Iran kuwa Zanzibar
itasimamia kwa umakini miradi hiyo kwa faida ya wananchi ambapo
alitumia fursa hiyo kutoa shukran kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa
msaada huo na ushirikiano wake na SMZ.

Wakati huo huo, Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo wa Zanzibar,
Abdilahi Jihad Hassan amesema ushirikiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya
Iran na Zanzibar unastahiki kuendelezwa kwa faida ya watu wa pande
mbili hizo.

Akizungumza katika kumbukumbu ya miaka 22 ya kifo cha Kiongozi wa
kidini wa Iran, Imam Ayatulah Khomenei ,Waziri Jihad ameiomba Iran
kuendelea kuisaidia Zanzibar katika sekta mbalimbali pamoja na
kuwashawishi Wawekezaji wan chi hiyo kuwekeza katika Visiwa vya
Zanzibar.

Balozi wa Iran nchini Tanzania, Muhsein Muvakhed amesema Jamhuri ya
Kiislamu ya Iran itaendelea uhusiano wake na Tanzania na kwamba
Serikali ya nchi hiyo itasimamia kwa dhati mambo yote yanayokusudiwa
kutekelezwa hapa nchini. 

No comments:

Post a Comment