Chadema, CUF waandaa maandamano

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari juu ya kutoridhishwa na maamuzi ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora ya kuwanyima dhamana viongozi wa chama hicho akiwemo Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Uchaguzi na Bunge wa chama hicho, Shaweji Nketo na Katibu wa Mwenyekiti huyo, Thomas Mongi.
Chadema watafanya maandamano ya amani mkoani Kigoma Jumamosi wiki hii, wakati CUF watafanya maadamano yao Dar es Salaam.
CUF wanapinga viongozi wake kunyimwa dhamana na mahakama mkoani Tabora.
Uamuzi wa maandamano ya Chadema ulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Mkoa wa Kigoma, Japhar Kasisiko, kwa waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa Kasisiko, maandamano hayo yatahudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wabunge na madiwani wa chama hicho.
Kasisiko alisema watazungumzia jinsi ya Mbowe alivyokamatwa na kupelekwa Arusha chini ya ulinzi mkali kama mhalifu wakati ni Kiongozi wa Upinzani Rasmi Bungeni pamoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kukamatwa kwa kosa la kuzidisha muda kwenye mkutano wake wa hadhara mkoani Sungida.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa maandamano hayo yana lengo la kuishinikiza serikali kutekeleza ahadi zake ilizotoa kwa muda mrefu za kupelaka maendeleo katika mkoa wa Kigoma.
“Hayo ndiyo tunayotaka kuyasema kwa serikali ya CCM,” alisema, na kuongeza kuwa serikali imeshindwa kupeleka maendeleo katika mkoa wa Kigoma kwa muda wa miaka mingi na kwamba Chadema inataka mabadiliko mkoani humo.
MFUASI WA CHADEMA MBARONI
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, linamshikilia na kumhoji anayedaiwa kuwa ni mfuasi wa Chadema, Prosper Mfinanga (40), mkazi wa Kijenge kwa tuhuma za kutembea na bango lenye maandishi yanayodaiwa kuwa ya uchochezi na uvunjifu wa amani.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, alisema jeshi hilo linamshikilia mfuasi huyo tangu Juni 5, mwaka huu.
Alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na bango hilo katika maeneo ya Soko Kuu majira ya saa 11:30 jioni, huku akilitembeza barabarani.
Aidha, Mpwapwa alisema bango hilo lilikuwa na maandishi katika pande mbili, ambapo upande wa kwanza ulisomeka “heri Ukimwi uendelee kuliko CCM iendelee kutawala.”
Mpwapwa alisema upande wa pili ulisomeka kama “kumkamata waziri kivuli ni kuvunja sheria za mabunge ya Jumuiya ya Madola” huku akisisitiza kuwa maandishi hayo yanaashiria uchochezi ndani ya jamii.
Alisema jeshi hilo kwa sasa linamhoji mtuhumiwa huyo, nia na madhumuni ya kuwa na bango hilo na kujua endapo maandishi hayo, aliandika mwenyewe au aliandikiwa na watu wengine.
Alisema endapo mtuhumiwa huyo atathibitika alihusika na tuhuma zinazomkabili, atafikishwa mahakamani.
MBOWE AANDALIWA MAPOKEZI
Katika tukio lingine, jana polisi mjini Dodoma walilazimika kuingilia kati kuwazuia kwa muda wafuasi wa Chadema Mkoa wa Dodoma waliokuwa wanakwenda kumpokea Mbowe katika eneo la Meriwa Kisasa akitokea Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudhuria vikao vya Bunge.
Kundi la wakazi hao baadaye liliruhusiwa na polisi kupita baada ya kuwaeleza kuwa hawakuwa na mpango wa kumpokea kiongozi huyo wa upinzani bungeni kwa njia ya maandamano.
Mbowe alichelewa kuwasilili ingawa umati huo uliendelea kumsubiri wakiwemo viongozi wa Chadema, wanachama, wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na wafuasi waliokuwa wamepanda pikipiki.
CUF NAO KUANDAMANA
Wakati huo huo, CUF, kimesema kuwa Jumapili ijayo kitafanya maandamano ya kulaani kitendo cha Mahakama ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora kumnyima dhamana Mbunge wa Viti maalum wa chama hicho, Magdalena Sakaya, na viongozi wengine wa kitaifa.
Maandamano hayo ambayo yatafanyika jijini Dar es Salaam, pia yana lengo la kulaani mauaji ya raia yaliyofanywa na polisi na kuwajeruhi watu wengine wanne katika kijiji cha Usinge.
Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahimu Lipumba, aliviambia vyombo vya habari jana kuwa, CUF kimejipanga kufanya maandamano hayo ambayo yataanzia Ubungo hadi Manzese Bakhresa ambako utafanyika mkutano wa hadhara.
Alisema tayari wameshatoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusiana na maandamano hayo hivyo wanachama na Watanzania kwa ujumla wanatakiwa kujitokeza.
Aidha, alisema maandamano yana lengo la kupinga unyanyasaji wa vyombo vya dola dhidi ya viongozi wao, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tabora wa (CUF), Magdalena Sakaya, aliyekamatwa na kusweka ndani wilayani Urambo na kunyimwa dhamana.
Wengine walionyimwa dhamana ni pamoja na wajumbe watatu wa Baraza Kuu ambao ni Yassin Mrotwa, Doyo Hassan na Zainab Nyumba.
Wengine ni Ofisa wa Haki za Binadamu na Sheria Taifa, Hashim Bakari, mgombea ubunge mwaka 2010 katika Jimbo la Urambo Magharibi, Amir Kirungi na viongozi saba waandamizi wa kata ya wilaya ya Urambo ambao ni Mrisho Swedi, Singu Yustu, Changu Salum, Idd Matola, Msafiri Alkado, Ukiwa Juma na Peter Charles.
Lipumba alisema chama chake kimefanya kila jitihada za kuhakikisha watu wao wanapata dhamana, lakini juzi mahakama iliamua kutoa masharti magumu hali iliyosababisha waendelee kubaki mahabusu.
“Hakimu Oscar Burugu alitoa masharti magumu ambayo ni watuhumiwa wajidhamini kwa barua zenye ahadi ya Sh. milioni tatu, kila mtuhumiwa adhaminiwe na mtu mmoja mwenye hati ya nyumba ya thamani ya Sh. milioni tatu na kila mtuhumiwa awe na barua ya utambulisho kutoka kwa mtendaji wa kijiji iliyothibitishwa na mtendaji wa kata na sio kijiji,” alisema.
Lipumba alisema baada ya masharti hayo kutolewa, wakili wa washtakiwa, Twaha Taslima, aliiomba mahakama ilitizame suala hilo kwa upana kwani sharti la kutaka hati ya utambulisho iliyothibitishwa na mtendaji wa kata ni suala geni.
Alisema pamoja na wakili huyo kumweleza hakimu ugumu wa sharti hilo ambalo ni la kwanza kufanyika kwenye kesi hiyo, hakimu aliendelea na msimamo wake na kuihahirisha kesi hadi Juni 15, mwaka huu.
Alisema kwa kawaida barua ambazo hutolewa mahakamani huwa na sahihi ya watendaji wa kijiji, lakini katika kesi ya viongozi wa CUF hakimu alibadili utaratibu na kutaka barua ya mtendaji wa kata na kudai kuwa ni utaratibu mpya ulioanzishwa na mahakama.
Pia, alisema kitendo cha hakimu huyo kudai apewe hati ya nyumba nacho ni unyanyasaji kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania hawana hati hizo.
“Viongozi wetu wawili wakili Taslima na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Julius Mtatiro, ambao wapo huko kwa ajili ya kushughulikia dhamana walijitahidi kupata barua zenye sahihi ya mtendaji wa kata, lakini tatizo lililopo ni hilo la hati ya nyumba eneo hilo, binafsi nina nyumba Dar es Salaam, lakini hati zake sina,” alisema na kuongeza: “Kati ya wamiliki wa nyumba 100 Dar es Salaam wenye hati za nyumba ni 20 tu, hii inatokana na ugumu wa upatikanaji wake.”
Hata hivyo, alisema wananchi kadhaa waliohojiwa na waandishi walieleza kuwa Ijumaa iliyopita watu walikuwa wakidhaminiwa kwa barua kutoka wa watendaji wa vijiji na sio kata.
Alisema siku hiyo, kiongozi wa kwanza kupandishwa kizimbani alikuwa ni Idd Matola katika kesi ya jinai namba 60/2011 ambaye dhamana yake iliwekwa wazi na wadhamini walisimama na kuanza taratibu.
Alisema hakimu huyo alimtaka mwendesha mashtaka athibitishe hati ya dhamana ambaye alifanya hivyo na kuridhishwa nayo.
Alisema hakimu alipozichukua aliweka pingamizi kuwa hati husika hazijapitia kwa mtendaji wa kata kwa uthibitisho na kueleza kuwa huo ni utaratibu mpya ambao umeanza hivi karibuni na wananchi watauzoea.
LIPUMBA ANG’AKA
“Kitendo cha hakimu kuweka masharti magumu na kuahirisha kesi hadi Juni 15, kinalenga viongozi hawa kukaa gerezani siku tisa zaidi na hii itakamilisha siku 20 za kukaa humo kwa kunyimwa dhamana,” alisema Lipumba.
Alisema kunyimwa kwa dhamana kwa watu hao ni utaratibu wa makusudi unaofanywa na serikali ya CCM kudhoofisha chama chao na kuwalinda mafisadi ndani ya serikali wanaowadhulumu wafugaji mali zao.
“Vitendo hivi vinafanywa na serikali kwa makusudi ili sisi wapinzani tushughulikie kesi, baadhi ya viongozi wa Urambo ni mafisadi na majambazi ambao kazi yao ni kuwanyang’anya wananchi mifugo na mali zao, wanatumia bunduki kufanya vitendo hivyo,” alisema na kuongeza:
“Jeshi la polisi linaua raia uchunguzi wa miili haufanyiki, vitendo hivi vinaashiria kuwepo kwa makundi ya ugaidi hapa nchini, tunakitaka kitengo cha haki za binadamu wafanye uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa matukio haya Urambo hadi sasa mifugo zaidi ya 6,000 imechukuliwa.”
Alisema CUF imeshangazwa na kitendo cha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kukaa kimya licha ya wabunge wa Bunge lake kukamatwa na kuwekwa ndani.
Imeandikwa na Joctan Ngelly,Kigoma; Cynthia Mwilolezi, Arusha; Paul Mabeja, Dodoma na Romana Mallya, Dar.
No comments:
Post a Comment