Bajeti ya Wizara ya Afya Z`bar yakwama
Waziri wa Afya, Juma Duni Haji
Kamati ya Baraza la Wawakilishi (BLW) inayoshughulikia masuala ya utawi wa jamii, wanawake na watoto imegoma kupisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo
Kwa maelezo kuwa shughuli za manunuzi ya dawa kutotengewa fedha kutawakosesha wananchi huduma ya afya.
Kikao cha kamati hiyo kilichokutana katika ukumbi wa BLW chini ya Mwenyekiti wake, Amina Iddi Mbarouk sio kwa serikali kutotenga fedha za kununulia dawa na badala yake kutegemea kasma ya shughuli hiyo ichangiwe na wahisani peke yao.
Mjumbe wa kamati hiyo, Jaku Hashim Ayub (Muyuni), alisema kamati haikuona kuwa ni busara kupitisha makadirio hayo kwa vile yamebainika kuwa na upungufu mkubwa katika maeneo mengi ya msingi kwa huduma ya afya.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa mambo mengine yaliyokwamisha bajeti ni pamaoja na kitengo cha huduma kwa wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya Mnazimoja kutotengewa fedha.
Kitengo hicho hivi sasa hakina mashine za kuwasaidia wagonjwa mahututi, baada ya mashine tano aina ya HP/Hewlett Packard, ziitwazo Monitor Machine kuharibika kwa muda wa zaidi ya mwaka moja sasa.
Mambo mengine yaliyosababisha kamati hiyo kuchukua uamuzi wa kugoma kupitisha bajeti ya wizara hiyo, ni baada ya kuona ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imetengewa Sh. milioni mbili kwa ajili ya kasma ya mafunzo.
Imeelezwa kuwa kwa kauli moja wajumbe wa kamati hiyo walisema kiwango hicho ni sawa na mzaha na imeagiza makadirio ya bajeti ya wizara hiyo yapitiwe upya kabla ya kikao cha bajeti kuanza Juni 15, mwaka huu.
Wakati bajeti hiyo imekwama kupitishwa kwa kukosa kasma ya manunuzi ya dawa na Mkemia Mkuu kutengewa Sh. milioni mbili tu kwa ajili ya mafunzo, kamati pia imeona si busara kwa wizara hiyo kutenga Sh.milioni 600 kwa ajili ya semina za watendaji wakuu wa wizara hiyo.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa wajumbe wa kamati walikuwa wakali kutokana na viongozi muhimu Wizara ya Afya kutohudhuria kikao hicho, akiwemo ofisa mdhamini wa wizara hiyo Pemba na Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, ambaye yuko safarini nje ya nchi .
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Sira Ubwa Mamboya, alisema kutopitishwa kwa bajeti hiyo kumesababishwa na idadi ya wajumbe wa wizara katika kikao hicho kutokamilika.
Wizara ya Afya inatarajia kutumia zaidi ya Sh. bilioni nne katika mwaka ujao wa fedha.
No comments:
Post a Comment