Monday, 30 May 2011

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inahitaji kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 123




Na Mwandishi wa MAELEZO Zanzibar


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inahitaji kiasi cha Dola za Kimarekani
milioni 123 kuweza kumaliza tatizo la maji safi na salama kwa Mikoa ya
Unguja na Pemba.
Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Seif Shariff Hamad ameuambia ujumbe
wa viongozi wa Jumuiya ya Madhehebu ya Khoja Shia Ithinashir kwamba
tatizo la maji safi na salama linafanyiwa kazi na kwa sasa
zinahitajika fedha hizo kuweza kukamilisha miradi ya maji.
Kama mnavyofahamu Zanzibar kuna tatizo la maji, Serikali haijakunja
mikono, mipango mbalimbali inafanywa kukabili tatizo hilo” Alisema
Maalim Seif.
Maalim Seif amesema ikiwa fedha hizo zitapatikana basi matatizo
yanayowakabili wananchi wa Visiwa vya Zanzibar kukosa maji safi na
salama litakuwa historia hivyo aliwaomba wananchi kuendelea kuwa na
subira.
Akizungumzia suala la umasikini,Makamu huyo wa kwanza wa Rais amesema
Serikali imedhamiria kuwakwamua wananchi wake katika dimbwi la
umasikini kwa kubuni mipango mbalimbali yenye tija kwa umma.
Maalim Seif amesema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zinazoendelea
ambazo zinakabiliwa na hali ya umasikini, lakini pamoja na hali hiyo,
bado kuna matumaini ya kupunguza kwa kiasi kikubwa hali hiyo chini ya
mpango mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini(MKUZA)
Sekta kadhaa zimetajwa chini ya mikakati ya kupunguza umasikini katika
Visiwa vya Zanzibar huku kiwango cha elimu kikitarajiwa kuimarishwa
sanjari na ukuzaji wa Sayansi na Teknolojia.
Makamu huyo wa kwanza wa Rais, amesema masuala ya afya ya jamii
yamekuwa wakipewa kipaumbele ili kujenga jamii yenye afya bora ambayo
itashiriki katika uzalishaji mali.
Alisema kwa kuwa na watu wenye afya bora kunasaidia kwa kiasi kikubwa
katika kukuza uchumi wan chi kwani muda mwingi utatumika katika
uzalishaji mali na sio kwenye matibabu, hivyo aliwahakikishia msimamo
wa Serikali kuimarisha sekta ya afya Zanzibar.
Maalim Seif amepongeza uamuzi wa Jumuiya hiyo kujenga kituo cha afya
ambacho kinatumika na wananchi wote ambacho kinazingatia zaidi utoaji
huduma kwa njia isiyo ya kibiashara.

No comments:

Post a Comment