Pia yashikilia wajumbe sita wa Baraza KuuJeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikilia wajumbe sita wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), akiwamo Mbunge wa Viti Maalum (Tabora), ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa CUF, Magdalena Sakaya.
Polisi imedai kuwa wamewakamata kwa kuwa walifanya mkutano bila kibali chao (Polisi).
Kufuatia hali hiyo, Chama hicho kimetangaza kufanya maandamano makubwa kupinga mauaji yanayoendelea kufanywa na polisi dhidi ya raia nchini, ikiwa ni siku mbili baada ya askari wa jeshi hilo kuua tena na kujeruhi raia kwa risasi katika Wilaya ya Tabora, mkoani Tabora.
Tamko hilo la CUF, lilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wake Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alipozungumza na waandishi wa habari, katika ofisi ndogo za chama hicho, jijini Dar es Salaam jana.
“Chama kinaandaa maandamano makubwa kupinga yanayofanywa na polisi kila kona ya nchi kwa kuwaua raia wasio na hatia na kuwabambikizia kesi. Pamoja na maandamano hayo tutazidi kuchukua hatua nyingine ikiwamo kuendelea kuwatetea wananchi dhidi ya kila unyanyasaji unaofanywa na vyombo vya dola vya serikali ya CCM,” alisema Mtatiro.
Alisema mbali na kuua na kujeruhi, askari hao pia wanawashikilia watu sita, akiwamo Mbunge wa Viti Maalum (Tabora), ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa CUF, Magdalena Sakaya pamoja na wajumbe wanne wa Baraza Kuu la Uongozi wa Chama hicho Taifa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, alithibitisha kuuawa, kujeruhiwa kwa raia hao kwa risasi, pamoja na kushikiliwa na polisi kwa mbunge huyo na wajumbe hao wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa.
Kwa mujibu wa Kamanda Barlow, aliyeuawa ni Said Juma, ambaye alisema alipigwa risasi ya mgongoni alipotaka kumnyang’anya bunduki askari polisi Shabani, wakati aliyejeruhiwa mkononi, ambaye anatibiwa katika Hospitali ya Urambo, mkoani humo chini ya ulinzi mkali wa polisi, alimtaja kuwa ni Changa Salum.
Wajumbe hao Baraza Kuu wanaoshikiliwa na polisi pamoja na mbunge huyo, ni pamoja na Doyo Hassan, Yasin Mrotwa, Zainabu Nyumba na Masud Omar.
Wengine wanaoshikiliwa na polisi ni Ofisa Haki za Binadamu na Sheria Makao Makuu ya CUF, Hashim Bakari na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia chama hicho Jimbo la Urambo Magharibi, Kirungi Kirungi, ambao Kamanda Barlow alisema wote watafikishwa mahakamani leo.
Mauaji hayo yamefanywa siku chache baada ya yale ya watu watano yaliyofanywa na askari polisi katika mgodi wa North Mara, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, wiki chache zilizopita. Mtatiro alidai mauaji hayo yalifanywa baada ya polisi kwa kushirikiana na askari wa maliasili, kuvamia Kijiji cha Shela, Kata ya Ngusa, wilayani humo na kuchukua kwa nguvu ng’ombe zaidi 6000 na kuwapeleka makao makuu ya Kata ya Usinge.
Alidai askari hao waliwahamisha ng’ombe hao, kwa madai ya kukomesha tabia ya wanavijiji kwenda kulisha mifugo yao katika hifadhi.
“Walipoulizwa kwanini wasiikamate mifugo ikiwa ndani ya hifadhi badala yake wanakuja kukusanya mifugo ndani ya kijiji walisisitiza kuwa wanatekeleza maagizo ya wakubwa. Katika ukusanyaji huo wa mifugo watu wanne walipigwa na kujeruhiwa vibaya kisha wakachukuliwa na kupelekwa katika gereza la Urambo,” alidai Mtatiro.
Mtatiro alidai Mei 25, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Shela, wilayani humo, Ngusa Maduhu, alikwenda makao makuu ya kata kunakoshikiliwa mifugo hiyo kuwauliza askari na mamlaka zilizokamata sababu ya kufanya hivyo bila kuijulisha ofisi yake.
Alidai Ngusa (30) alianza kupigwa na kuvunjwa mguu na baada ya hapo akaburuzwa hadi katika gari la polisi na kupelekwa rumande na siku iliyofuatia alifikishwa katika Mahakama ya Mwanzo, ambako alisomewa mashtaka ya kubambikiziwa na kunyimwa dhamana.
Mtatiro alidai baada ya kupata taarifa hizo, CUF makao makuu walianza kuwasiliana na viongozi mbalimbali wa jeshi la polisi walioko Tabora na makao makuu ya jeshi hilo, lakini hawakupata msaada wowote.
Alidai Mei 27, chama kilituma ujumbe wa wajumbe hao wa Baraza Kuu la Uongozi pamoja na mbunge huyo, ambao ulifika Urambo siku iliyofuatia, ambao licha ya kuwasiliana na mkuu wa wilaya, alikataa kuwapa ushirikiano, badala yake aliwaeleza kuwa hawapaswi kujihusisha wala kuingilia mgogoro huo.
“Ikumbukwe kuwa hadi jana (juzi) ng’ombe zaidi ya 20 walikuwa wamekufa kwa kudhoofika kwa sababu ya kukosa chakula na maji,” alidai Mtatiro.
Alidai ujumbe huo ulikwenda moja kwa moja katika Kijiji cha Usinge, ambako mifugo hiyo ilikuwa ikishikiliwa na kwamba, walipofika walizungumza na mwenyekiti wa kijiji na wajumbe wake kujua hali ya mambo.
Mtatiro alidai baada ya mazungumzo, walipotoka ofisini, walistuka kuona mamia ya wananchi, ambao mifugo yao imechukuliwa wakiwa wamezunguka ofisi ya kijiji kutaka kujua viongozi wao watawasaidiaje.
“Ilibidi viongozi waanze kuongea nao katika makundi madogomadogo kuwasihi wasifanye chochote kwani suala hilo viongozi wetu wanaweza kulitatua kwa njia ya amani. Wananchi walikubali na kutawanyika. Wakati wanaanza kutawanyika ghafla walitokea polisi kwenye magari ya jeshi wakaanza kuwakamata vijana kwa nguvu,” alidai Mtatiro.
Alipoulizwa na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kamanda Barlow, alisema matukio hayo yalitokea wakati askari polisi kwa kushirikiana na askari wa maliasili na mgambo wakifanya operesheni ya kuwakamata wavamizi katika Hifadhi ya Mpanda Line, iliyoko wilayani humo.
Kamanda huyo alisema wanaovamia hifadhi hiyo, hulisha mifugo, kuchoma mkaa, kurima asali, kupasua mbao, kufanya ujangili, kuvua samaki kwenye sagara lililoko ndani ya hifadhi, kulima na kuweka makazi kwenye hifadhi hiyo.
Alisema katika operesheni hiyo askari hao walikamata mbao 178, samaki 1,780, magogo 14, milango mitano na baiskeli mbili, ambazo zilikamatwa katika eneo la Ziwa Sagara.
Kamanda Barlow alisema pia walikamata ng’ombe 820 ndani ya hifadhi hiyo na kwamba, wamiliki wa mifugo hiyo walijasalimisha katika ofisi za maliasili, ambako walitozwa faini ya Sh. milioni 6 kwa ng’ombe 100 na kukabidhiwa ng’ombe wao.
Alisema kutokana na hatua hiyo, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Shela, Maduhu, aliwahamasisha wamiliki wengine wa ng’ombe 720 waliobaki kwa kuwataka wasijisalimishe maliasili, badala yake wawavamie askari kwenye zizi la muda, ambako ng’ombe hao wanashikiliwa, kisha wawashambulie kwa mawe na kuwanyang’anya mifugo yao.
Kamanda Barlow alisema wamiliki hao waliitikia mwito huo, ambapo walianza kuwarushia askari mawe, lakini askari hao waliwamudu na kuwakamata vinara wa wamiliki hao, akiwamo Ngusa na wenzake wanne; Ngalu Mtanja (30), Bundi Lutabula (31), Sangilwa Mtara (50), wote wakazi wa kijiji cha Shela na John Charles (30) mkazi wa Kijiji cha Usinge. Wote hao wako rumande kwa tuhuma za kufanya uchochezi na kushambulia askari.
“Baada ya hapo Ngusa aliwasiliana na makao makuu ya CUF kuomba msaada. Wakaja kina Sakaya. Walifika Tabora, hawajasalimia kiongozi yeyote wa serikali, wakaenda hadi kwenye mkutano, ambao haukuruhusiwa. Wakafanya uchochezi, kupandikiza chuki na kuhamasisha wananchi kwamba, serikali inawaonea na kuwakandamiza. Hivyo, waende kuchukua mifugo yao,” alisema Kamanda Barlow.
Alisema wamiliki hao wa ng’ombe waliondoka na kuanza kumrushia mawe Mkuu wa Upelelezi Urambo na kwamba, katika vurugu hizo, mmoja wa wanakijiji alimrukia askari polisi, Shaban na kumng’ata meno katika mkono wa kushoto na kutaka kumnyang’anya bunduki.
Kamanda Barlow alisema pia askari polisi mwingine, Rajabu alijeruhiwa kwa mawe na kwamba, watu wengine, akiwamo Msafiri Alqaeda, Mkiwa Juma, Singu Yusto, Mrisho Frederick, Peter Charles na Zainabu Seif, walikamatwa kwa tuhuma za kufanya mkutano usiokuwa na kibali, kushambulia na kujeruhi askari polisi.

No comments:
Post a Comment