Tuesday, 31 May 2011

Slaa, Lema wawazidi askari Polisi ujanja

 
  Wafika kortini kuwakamata watoka patupu
  Hukumu kuamua majaliwa ya dhamana yao leo
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa (katikati), akiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya kujisalimisha kufuatia amri ya Mahakama hiyo kumataka yeye na viongozi wenzake wakamatwe.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, jana waliwazidi kete askari polisi waliokwenda kuwakamata walipojisalimisha wenyewe.
Viongozi hao walijisalimisha wenyewe mahakamani hapo, mapema jana saa 2:00 kamili asubuhi, kufuatia amri ya mahakama ambayo iliagiza wakamatwe kwa kutofika mahakamani Mei 27, mwaka huu.
Wakiwa mahakamani hapo saa 9.10 jioni, katika hali isiyo ya kawaida, ilitokea purukushani, baada ya Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kufika mahakamani hapo na kutaka kuwakamata washtakiwa hao ili kuwarudisha polisi.
Hata hivyo, washtakiwa hao, Dk. Slaa na Lema, walikataa kupelekwa polisi na waliwashutumu polisi hao kuwa wameshindwa kazi yao ya kuwakamata.
Mvutano huo uliendelea na kusababisha Goodbless Lema kurusha maneno makali kwa askari akiwataka waache kuwakamata kwa sababu wameshindwa kazi.
“Nyie mmeshindwa kutukamata sisi tumekuja wenyewe kama mnataka kutupa lifti sawa ila siyo kutukamata, sisi tumekuja mahakamani na huku ndiko tunakohitajika mnataka kutupeleka wapi,” alihoji Lema.
Naye Dk. Slaa alikataa kukamatwa na askari hao huku akisisitiza kuwa hakuna sababu ya polisi kuwabugudhi wakati wamejisalimisha wenyewe.
“Nyie polisi mnachekesha mtukamate hapa wakati sisi tupo wenyewe tangu asubuhi, ebu acheni hizo mmeshindwa kazi,” alisema Dk. Slaa.
Baada ya malumbano hayo mahakamani hapo, hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Hakimu Mkazi, Charles Magesa, aliwaita na kuanza kusikiliza kesi yao.
Wakiwa mahakamani, wakili wa upande wa utetezi, Method Kimomogoro na Albert Msando, waliiomba mahakama hiyo, kuondoa amri ya kukamatwa kwa washtakiwa wao.
Alisema sababu kubwa ni mkanganyiko uliotokea siku ilipotajwa kesi hiyo Aprili 29, mwaka huu ambapo ilielezwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa ambao ni wabunge, Philemon Ndesamburo, Lema, Joseph Selasini na Freeman Mbowe, hawataweza kuhudhuria kesi hiyo kwa sababu ya vikao vya Kamati za Bunge.
“Mheshimiwa wewe mwenyewe ulikubali ombi hilo na ndiyo sababu washtakiwa hawakufika mahakamani na walishangaa kusikia amri ya kutaka wakamatwe,” alisema Kimomogoro.
Alisema kwa kuwa washtakiwa wametii amri ya mahakama hiyo na kufika wenyewe basi mahakama iondoe amri ya kuwakamata.
Wakili Kimomogoro aliwataja washtakiwa ambao hawakufika mahakamani Mei 27, mwaka huu kuwa Mbowe, Dk. Slaa, Lema, Aquline Chuwa ambaye ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Moshi Mjini, Josephine Slaa na Richard Mtui.
Hata hivyo, kabla ya Hakimu kuendelea na kesi hiyo, alimpa nafasi wakili upande wa serikali, Edwin Karokola, ambaye aliomba Mahakama kutoa muda mpaka kesho (leo) ili kujiridhisha na hati ya daktari wa Hospitali ya Mawenzi Mkoani Kilimanjaro, kama kweli Aquline Chuwa alikuwa mgonjwa.
Hakimu Charles Magesa, alikubaliana na maombi ya pande mbili na kufuta amri ya kukamatwa kwa washtakiwa na kuweka dhamana ya muda hadi leo kesi itakapoendelea tena. Pia kujiridhisha kwa upande wa wakili wa serikali, ili atoe dhamana au la.
Awali, wakati kesi hiyo ikiendelea NIPASHE ilishuhudia magari mawili ya Jeshi la Polisi yenye namba za usajili PT.1414 na PT 1177 yakiwa na askari waliosheheni silaha yakiwa tayari kwa kuwachukua washtakiwa hao kwenda mahabusu, hata hivyo walishindwa kufanya hivyo.
Magari hayo yaliondoka mahakamani hapo yakiwa tupu, baada ya mahakama kuamua kufuta amri ya kukamatwa kwao.
Washtakiwa 19 wakiwemo viongozi wa chama hicho na wafuasi wao, walishtakiwa kwa kosa la kufanya mkusanyiko pasipo kibali na kutoa lugha ya uchochezi kwa viongozi wao.
Washtakiwa walikana mashtaka yote na wako nje kwa dhamana hadi leo kesi itakapotajwa tena.

No comments:

Post a Comment