Tuesday, 31 May 2011

Mbunge wa CUF anyimwa dhamana

 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow
Wajumbe wanne wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), na maofisa wengine saba wa chama hicho akiwemo Mbunge wa Viti Maalum (Tabora), ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa CUF, Magdalena Sakaya, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Urambo mkoani Tabora kwa shtaka la kufanya mkutano bila kibali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, aliliambia NIPASHE jana kuwa walifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi chini ya ulinzi mkali wa polisi na kusomewa mashtaka ya kumshambulia mpelelezi, kutojitambulisha kwa makusudi kwa askari polisi na kwenda kuchukua mifugo ambayo inashikiliwa na polisi.
Kamanda Barlow alisema walifikishwa mbele ya Hakimu Oscar Burugu wa mahakama hiyo, baada ya kusomewa mashtaka walinyimwa dhamana.
Alisema mahakama hiyo ilikataa dhamana yao kwa kuhofia kuvunjika kwa amani kwani wangeweza kwenda kuhamasisha wananchi kwenda kuchukua mifugo ambayo bado inashikiliwa na polisi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, alisema mahakama hiyo imewanyima dhamana ikidai kuwa iwapo wataachiwa amani inaweza kuvurugika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 6, mwaka huu na washtakiwa wote walirudishwa rumande.
Wajumbe hao wa Baraza Kuu waliofikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana pamoja na mbunge huyo, ni Doyo Hassan, Yassin Mrotwa, Zainabu Nyumba na Masoud Omar.
Wengine ni Ofisa Haki za Binadamu na Sheria Makao Makuu ya CUF, Hashim Bakari na aliyekuwa mgombea ubunge kupitia chama hicho Jimbo la Urambo Magharibi, Kirungi Kirungi.
Juzi polisi Mkoa wa Tabora ilidai kuwa iliwakamata kwa kuwa walifanya mkutano bila kibali cha polisi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Julius Mtatiro, alisema mgogoro huo ulianza baada polisi kwa kushirikiana na askari wa maliasili, kuvamia kijiji cha Shela, kata ya Ngusa, wilayani humo na kuchukua kwa nguvu ng’ombe zaidi 6,000 na kuwapeleka makao makuu ya kata ya Usinge.
Alisema askari hao waliwahamisha ng’ombe hao, kwa madai ya kukomesha tabia ya wanavijiji kwenda kulisha mifugo yao katika hifadhi.
Alisema katika ukusanyaji huo wa mifugo watu wanne walipigwa na kujeruhiwa vibaya kisha wakachukuliwa na kupelekwa katika gereza la Urambo.
Mtatiro alidai Mei 25, mwaka huu, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Shela, wilayani humo, Ngusa Maduhu, alikwenda makao makuu ya kata kunakoshikiliwa mifugo hiyo kuwauliza askari na mamlaka zilizokamata ng’ombe sababu ya kufanya hivyo bila kuijulisha ofisi yake.
Alidai Ngusa (30), alianza kupigwa na kuvunjwa mguu na baada ya hapo akaburuzwa hadi katika gari la polisi na kupelekwa rumande na siku iliyofuatia alifikishwa katika mahakama ya mwanzo, ambako alisomewa mashtaka ya kubambikiziwa na kunyimwa dhamana.

No comments:

Post a Comment