Saturday, 28 May 2011

JK asisitiza fedha za rada ipewe serikali

 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe
Rais Jakaya Kikwete, ameitaka Serikali ya Uingereza kuhakikisha kwamba Kampuni ya Utengenezaji wa Vifaa vya Kijeshi ya Uingreza ya BAE inarudisha zile fedha zilizozidi kwenye ununuzi wa rada ya kijeshi iliyoiuzia Tanzania moja kwa moja katika Hazina ya Tanzania na si kuzipeleka kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs).
Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kuhusiana na ziara iliyofanywa na Waziri Mdogo wa Mambo ya Nje wa Uingereza anayeshughulikia Bara la Afrika, Henry Bellingham.
Waziri Membe alisema Bellingham alikuwa ameitembelea Tanzania mahsusi kuja kuangalia maendeleo ya utafiti na uchimbaji wa gesi katika eneo la kusini ambako kati ya makampuni manne yanayofanya kazi hiyo, mawili ni ya Uingereza.
Lakini katika safari yake pia, amepata fursa  ya kuongea na Rais Jakaya Kikwete ambapo Rais alimueleza Bellingham msimamo wa Tanzania kuwa tunataka fedha hizo zirudi katika Hazina ya nchi yetu na si vinginevyo, kwa kuwa ile ni haki ya wananchi wa Tanzania na haki siku zote haina mamlaka ya kimaadili,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri Bellingham alisema amelichukua suala la fedha za rada na kwamba atalifikisha katika serikali yake kwa ajili ya kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo ili fedha hizo zirudishwe kwa Serikali ya Tanzania.
Aidha, alisema mbali na suala la fedha za rada, walizungumzia  masuala mbalimbali ya kimaendeleo yanayozihusu nchi hizo mbili ambazo kwa mujibu wa maelezo yake, zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu.
Tulizungumzia suala la kuimarisha zaidi uhusiano wa kibiashara kati yetu ambao ilikuwa mojawapo ya malengo ya ziara yangu. Mimi na  Waziri Membe, tulifanya ziara ya kwenda Mtwara kuona maendeleo ya utafiti na uchimbaji wa gesi ulipofikia, kwa kuwa tuna makampuni yetu mawili yanayofanya kazi za utafiti na uchimbaji wa gesi,” alisema.
Hivi karibuni serikali kupitia kwa Waziri Membe, iliupinga hadharani uamuzi uliokuwa umefanywa na kampuni ya BAE ya kuilipa Tanzania fedha zake za rada zinazofikia kiasi cha Paundi za Uingreza milioni 29.5 kupitia kwenye mashirika NGOs badala ya kuzilipa serikalini moja kwa moja.
 

No comments:

Post a Comment