Saturday, 28 May 2011

Bilioni 30 zimetumika kinyume cha Sheria-Kamati

 
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imebaini zaidi ya Sh. bilioni 30 kutumiwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika manunuzi mbalimbali, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Miongoni mwa manunuzi yaliyobainishwa na wajumbe wa POAC katika kikao chake cha jana yanayodaiwa kufanywa na NHIF bila kufuata sheria hiyo ya mwaka 2004 pamoja na kanuni zake, ni pamoja na manunuzi ya mafuta, vilainishi na utoaji zabuni ya ulinzi. 
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Bunge, jijini Dar es Salaam, kilikuwa baina ya kamati hiyo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe na Menejimenti ya Mfuko huo.
Filikunjombe, ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema licha ya ripoti ya  mkaguzi kuthibitisha mahesabu ya NHIF kwamba ni mazuri, kamati imebaini upungufu mkubwa katika manunuzi mbalimbali yaliyofanywa na Mfuko huo.
Mkaguzi kasema mahesabu yenu ni safi, lakini manunuzi yenu yamekaa vibaya, ni harufu mbaya kwetu. Sh. bilioni 30 zimetumika kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma,” alisema Filikunjombe.
Hoja kuhusu ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma unaodaiwa kufanywa na NHIF, iliibuliwa na Mbunge wa Mwibara (CCM), Alphaxard Lugola katika kikao hicho cha jana.
Lugola alisema ukiukwaji wa sheria hiyo ni mkubwa katika manunuzi 16 yaliyofanywa na NHIF na kwamba, kwa mujibu wa taarifa yake iliyowasilishwa kwa kamati, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 9.7 zinaonekana kutumiwa na Mfuko huo katika manunuzi mbalimbali bila kuonekana kwenye mpango wa manunuzi ya mwaka.
Lugola alisema pia Sh. milioni 118 na Sh. milioni 89 zinaonekana kutumika katika manunuzi ya mafuta na vilainishi bila NHIF kufuata utaratibu wa kutangaza zabuni ya manunuzi hayo, badala yake wameipa kampuni moja tu ya mafuta ya Total zabuni hiyo.
Vilevile, alisema Sh. bilioni 7.5 zinaonekana kutumiwa na NHIF katika manunuzi, ambayo hayakuwamo kwenye zabuni wakati wakijua fika kwamba, kufanya hivyo, ni kukiuka sheria.
Alisema pia Sh. bilioni 12.7 zilitumika katika manunuzi kwa kukiuka viwango, ambavyo NHIF wanapaswa kuviainisha na kwamba, wamekuwa na mtindo wa kugawa zabuni kidogo kidogo, hali inayoashiria kuwapo tabia ya ‘kuwabeba’ baadhi ya watu na harufu ya rushwa.
Hivyo, POAC imeiagiza NHIF, pamoja na mambo mengine, kurekebisha dosari hizo mara moja; pia Msajili wa Hazina atoe waraka utakaotoa ufafanuzi kuhusu wajumbe wanaopaswa kuunda kamati ya ukaguzi kwa vile Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo kuwa mjumbe wa kamati hiyo ni kinyume cha utawala bora.   
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emmanuel Humba, alisema kasoro hizo zinachangiwa na upungufu wa wafanyakazi na mchakato wa kumpata mtaalamu mwingine baada ya yule wa aliyekuwapo awali kuondoka.

No comments:

Post a Comment