Monday, 18 April 2011

UVCCM Tanga nao wacharukwa


Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), wilaya ya Tanga limepanga kuandamana kuwaondoa watendaji wabovu wa serikali za Mitaa iwapo hawatajivua magamba kwa kipindi cha siku tisini.
Baraza hilo pia limesema halitasita kuwaumbua wataalamu waliopo katika ngazi ya halmashauri ambao wamekuwa wakilalamikiwa na wanachi kwa kutotimiza wajibu wao kiutendaji na badala yake wamekuwa wakizitumia fedha za umma kwa manufaa yao binafsi.
Akitoa maazimio ya baraza hilo jana,Katibu wa UVCCM wilaya ya Tanga Elias Mpanda alisema kuwa chama hicho kimekusudia mabadiliko ya kivitendo zaidi hivyo ili kuhakikisha kwamba wananchi wanarudisha imani na CCM hakitasita kupokonya nyadhfa walizonazo watendaji wa Serikali wanaoshutumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za wananchi.
“Watendaji hasa katika ngazi za serikali za mitaa utendaji wao wa kazi sio wa kuridhisha hata kidogo sasa kwa sababu hiyo tunawataka waanze kujiondoa wao wenyewe vinginevyo hatutalala mpaka wang’oke ikibidi kwa maandamano ya usiku na mchana yaani utashangaa mtaalamu anakuja kufanya kazi kwenye halmashauri mwembamba hana kitu baada ya mwezi magari manne,nyumba mbili zote hizo ni pesa za wananchi kweli tutakula nao sahani moja”,alisisitiza Mpanda kwa naiba ya baraza hilo.
Likitoa kauli kuhusiana na vuguvugu linaloendelea hapa nchini la mapendekezo ya muswada wa Katiba mpya Baraza hilo limekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema)kutowachanganya wananchi kwa kile walichodai kuwa ajenda hiyo haikuanzishwa na Chadema bali ya chama cha Wananchi CUF ambapo Rais kikwete aliridhia kutokana na hekima yake ya kuongoza nchi kwa kufuata utawala wa sheria.

No comments:

Post a Comment