Monday, 18 April 2011

Sumaye, Malecela mambo magumu

 
  Wakataa kujibu tuhuma za ufisadi
  Ni orodha mpya iliyotajwa na Dk. Slaa Tabora
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Dk. Willibrod Slaa

Vigogo waliotupiwa kombora la ufisadi na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Dk. Willibrod Slaa, wamegoma kujibu mashambulizi.
Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, John Malecela, amesema hana majibu ya tuhuma zilizotolewa Dk. Slaa.
Dk. Slaa juzi aliongeza orodha ya majina ya watu aliodai kuwa ni mafisadi likiwemo jina la Malecela, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Phillip Mangula na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Akizungumza na NIPASHE jana, Malecela alisema hayuko tayari kujibu shutuma hizo na aliomba aachwe apumzike.
“Niacheni nipumzike kama ni hayo mambo yenu ya magazetini sitaki kabisa kuyazungumza kwa sasa na nina haki ya kutozungumza…Lazima mtende haki mimi silazimiki kujibu kila kitu kinachosemwa juu yangu kama kasema hivyo si amesema yeye,” alisema Malecela.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Sumaye, alipoulizwa na NIPASHE kuhusu shutuma hizo, alisema hajasoma taarifa hizo kwa kuwa yuko kijijini kwake.
“Sijasoma hizo habari ndio nazisikia kwako, mimi niko kijijini na huku hakuna magazeti sina taarifa zozote kuhusiana na hayo,” alisema Sumaye.
Waziri wa Miundombinu, Dk. John Magufuli, hakuweza kujibu shutuma hizo kwani muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na baadaye ikazimwa.
Dk. Slaa anawashutumu kuwa walihusika na wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa).
Akizungumza kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora juzi, Dk. Slaa alisema orodha hiyo ni mwendelezo wa majina ya mafisadi 11 aliowataja Septemba 15 mwaka 2007 kwenye viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam.
Alipotafutwa kujibu makombora ya Dk. Slaa, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, John Chiligati, alisema yeye si msemaji wa chama hicho.
“Mtafute Nape, yeye ndiye msemaji wa chama unajua kila mtu akisema itakuwa tabu, mtafute atazungumza,” alisema Chiligati.

No comments:

Post a Comment