Polisi yamnasa 'kigogo' wa dawa za kulevya |
Na Mwandishi Wetu JESHI la Polisi Tanzania jana lilimtia mbaroni raia wa Iran, Asaad Azizi likimtuhumu kuwa kigogo wa biashara ya dawa za kulevya. Jeshi hilo limeeleza pia kuwa limefanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa huyo baada ya kuwatoroka mara kadhaa kwenye mitego waliyokuwa wameandaa kumnasa. Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya cha Polisi, Godfrey Nzowa aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa Azizi alikamatwa juzi eneo la Namanga, mpakani mwa Tanzania na Kenya. Alisema alikamatwa akiwa katika harakati za kutoroka nchini na kwenda Kenya baada ya kubaini kuwa polisi walikuwa wakimfuatilia. "Wakati tunamkamata hakuwa na dawa za kulevya ila tumekuwa tukimsaka siku zote na mara zote anatutoroka," alisema Nzowa. Azizi anatuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya aina ya heroine na cocaine. “Huyu mtu ni mjanja sana, mara kwa mara amekuwa akiwatoroka polisi kila wanapoweka mtengo kwa ajili ya kumkamata,” alisema Kamanda Nzowa na kuongeza: “Tulishawahi kumpekua nyumbani kwake Dar es Salaam na tukamkuta na dawa za kulevya lakini alitoroka,” alidai. Kamanda Nzowa alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa huyo ni raia wa Iran ingawa mwenyewe anadai kuwa ni Mtanzania. Alisema wanatarajia kumfikisha mahakamani wakati wowote baada ya kukamilika kwa upelelezi. |
No comments:
Post a Comment