Pinda: Maandamano, fujo, vurugu havina tija
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Pia amesema si busara kubeza viongozi waliopo sasa na waasisi wa taifa hili au katiba ya sasa kwani ni kudhalilisha taifa.
Alisema hayo bungeni jana wakati akiahirisha Mkutano wa Tatu wa Bunge hadi Juni 7, 2011 katika Mkutano wa Nne ambao ni mahsusi kwa ajili ya bajeti.
Alitoa wito kwa wananchi kuwa hawana budi kuendelea kuiheshimu na kuifuta katiba iliyopo mpaka pale katiba mpya inayoanza mchakato wake sasa itakapokamilika.
“Ningependa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa, Tanzania siyo kama inatunga Katiba Mpya kwa kuwa hatuna Katiba, wala kana kwamba tumetoka katika ukoloni, la hasha. Tunatunga Katiba Mpya kwa ajili ya kukidhi mazingira mapya na matakwa ya wananchi wa leo baada ya miaka 50 ya uhuru,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, aliwakumbusha Watanzania kushirikiana katika hatua zote zinazofuata katika mchakato wa kuelekea kutungwa kwa katiba mpya.
“Sasa tunayo fursa nyingine ya kutazama upya katiba yetu. Basi sote tushirikiane kwa dhamira moja ya kutoa maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali ili kwa pamoja tuweze kupata katiba itakayowanufaisha Watanzania wote,” alisema.
Alisema katiba inayotokana na michango yao mbalimbali na kumilikiwa na wananchi wenyewe, haina budi kutokana na Watanzania wote wenye nia ya kulitakia taifa hili na wananchi amani, upendo na utulivu.
Kuhusu muswada wa kuunda tume ya kukusanya maoni ya wananchi, alisema serikali itahakikisha muswada huo unachapishwa kwa lugha ya Kiswahili na kuusambaza kwa wananchi kwa lengo la kuwawezesha kujadili kwa wepesi na kueleweka.
Alisema serikali kwa upande wake imeweza kushiriki kikamilifu katika upokeaji wa maoni ya wananchi katika vituo vyote vitatu vya Dodoma, Dar es Salaama na Zanzibar kupitia mawaziri na watendaji wake na kwamba wananchi wengi wameonyesha shauku kubwa ya kutoa maoni yao katika mikutano hiyo ya kupokea maoni.
“Napenda kuliarifu Bunge lako kuwa serikali inakubaliana na uamuzi wako (Spika) wa kuongeza muda zaidi kwa lengo la kuendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau na wananchi ili kuboresha muswada kadri itakavyowezekana,” alisema.
Alisema wakati muafaka utakapowadia, serikali itatoa ushirikiano thabiti kwa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, ili kuwasilisha muswada bungeni utakaozingatia mambo ya msingi yatakayotolewa na wananchi kuanzia sasa.
Pia alisema itatoa ushirikiano wa dhati kwa viongozi na serikali ili taifa na wananchi wake waweze kujiletea maendeleo katika hali ya amani, upendo, mshikamano na utulivu.
Mgawo wa umeme:
Waziri Mkuu Pinda amesema ni matumaini ya serikali kuwa kuanzia mwakani, Watanzania wataondokana na tatizo la upungufu wa umeme.
Alisema hatua za muda mfupi za kukabiliana na upungufu wa umeme nchini zimeendelea kuchukuliwa tangu Novemba 2010 hadi sasa.
Alisema kwa mfano, serikali imelazimika kugharimia ununuzi wa mafuta mazito ya mitambo ya IPTL ili kuimarisha kiwango cha uzalishaji wa umeme kwenye gridi ya taifa.
Aidha alisema Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco), linaendelea na mchakato wa kukodi mitambo ya dharura yenye uwezo wa kuzalisha megawati 260.
“Zabuni za kuzalisha umeme wa dharura zilitangazwa Machi 18, mwaka huu, na ilipangwa zifunguliwe Aprili 15, mwaka huu, na kwamba mkataba unatarajiwa kusainiwa Aprili 30, mwaka huu na mradi unatarajiwa kukamilika Julai 2011.
Akizungumzia mgao wa umeme kwa sasa alisema unatokana na upungufu wa wastani wa megawati 60 katika gridi ya taifa ikilinganishwa na mgao wa umeme katika mwezi Februari 2011 uliokuwa unatokana na upungufu wa megawati 264.
“Nchi yetu inatarajia kuwa na upungufu wa umeme wa wastani wa megawati 60 katika mwaka wa 2011 na sababu za upungufu huo ni kutokana na mahitaji yake kuongezeka kwa kasi kuliko uwekezaji katika miradi mipya ya kuzalisha umeme ambapo mwaka 2008, mahitaji ya juu yalikuwa megawati 729 na mwaka 2010 mahitaji ya juu yalifikia megawati 833, hivyo kuwa na upungufu wa zaidi ya megawati 100 katika gridi ya taifa,” alisema.
Alitaja sababu nyingine kuwa hali ya hewa iliyosababisha kupungua kwa maji katika Bwawa la Mtera na kupunguza uwezo wa kuzalisha umeme unaokidhi mahitaji.
No comments:
Post a Comment