Mafuta yapandishwa Bei kimya kimya Zanzibar
Bei ya mafuta ya petroli, dizel na mafuta ya taa imepanda kimya kimya Zanzibar, kufuatia bei za bidhaa hizo kupanda katika soko la dunia.
Viwango vya bei mpya ya mafuta vilianza kutumika wiki hii ambapo lita moja ya petroli inauzwa sh 2,000 kutoka 1,870, dizel inauzwa sh 2,085 kutoka sh 1,930 huku mafuta ya taa yakiuzwa sh 1,650 badala ya sh 154 kwa lita moja.
“Mafuta yote yemepanda bei na hali hii imesababishwa na mabadiliko ya bei katika soko la dunia,” alithibitisha Meneja wa kampuni ya mafuta ya United Petroleum, (UPZ) Collins Chomngorem.
Alisema kwamba mabadiliko ya bei yaliyotokea ndiyo yaliyosababisha wauzaji wa nishati hiyo kupandisha bei kwa vile bila ya wao kupandishwa wangeshindwa kuendelea na biashara hiyo.
Hata hivyo, Meneja Collins hakuweza kueleza viwango vya bei za mafuta hayo katika soko la dunia.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Zanzibar, Khamis Mussa, hakuweza kupatikana kuzungumzia mabadiliko hayo ya bei, baada ya simu yake ya kiganjani kutopokelewa.
Hiyo ni mara ya pili mafuta kupanda bei Zanzibar katika kipindi cha mwezi mmoja na kusababisha nauli za daladala na baadhi ya bidhaa muhimu kupanda bei na kuathiri wananchi wenye kipato cha chini.
Mwezi uliopita Bodi ya usafiri Zanzibar ilipandisha nauli kutoka sh 250 hadi sh 300 ambazo hutembea kwa masafa ya kilomita 10, wakati magari yanayotoa huduma za usafiri vijijini yalipandisha bei kwa wastani wa sh 300.
Gari za abiria ziendazo Makunduchi zilipandisha nauli kutoka 1,700 hadi 2,000, Nungwi zilipandisha hadi 2,000 kutoka 1700, Mkokotoni 1,400 kutoka 1,200 na Uroa 1,400 badala ya 1,300.
Kwa upande wa kisiwa cha Pemba bodi ya usafiri wa barabarani ilitangaza nauli mpya kuwa ni Konde sh 2,800 badala ya sh 2,400, Wete – Mkoani sh 2,800 kutoka sh 2,400, ambapo bodi hiyo ilisema hatua hiyo ilifuatia kupanda kwa gharama za uendeshaji baada ya kupanda mafuta katika soko la dunia.
Wananchi katika manispaa ya mji wa Zanzibar jana walisikika wakilalamikia hatua ya mafuta kupanda bei kimya kimya, bila ya serikali kutoa taarifa juu ya viwango halali na sababu za kupanda kwa bei pamoja na hatima ya nauli za usafiri wa magari ya abiria Zanzibar.
No comments:
Post a Comment