Friday, 4 February 2011

Walimu Kufunzwa Kiingereza Kupitia Radio Zanzibar


Na Salma Said Zbar
MKURUGENZI British Council, Sally Robinson amesema progaramu ya vipindi vilivyoandaliwa na shirika hilo ambavyo vitatangazwa na Sauti ya Tanzania Zanzibar, vimelenga kuinua kiwango cha ufundishaji wa lugha ya kiingereza kwa walimu wa Zanzibar .
Mkurugenzi huyo alieleza hayo jana katika kituo cha walimu Bububu (TC), kwenye uzinduzi rasmi wa urushwaji wa vipindi hivyo.
Alisema vipindi hivyo vimetengenezwa makusudi kwa lengo la kuwajengea uwezo walimu na watu wanapenda kujifunza lugha ya kiingereza hapa Zanzibar .
Robinson alifahamisha kuwa kila kipindi kitahusishwa mbinu za ufundishaji wa lugha ya kiingereza kwa kutumia njia mbali mbali sambamba na kuweza kufundisha darasa lenye idadi kubwa ya wanafunzi.
“Mpango huu ni mzuri sana kwani ni wa kirafiki na unaomuwezesha mwalimu, kuwa huru katika ufundishaji pamoja na kutoa mawazo”,alisema Robinson.
Akizungumza kenye uzinduzi huo, Kamishna wa Elimu Mariam Abdulla Yussuf aliwaomba walimu kuvitumia vyema vipindi hivyo kwani vitawasaidia kikamilifu katika kumudu kufundisha lugha ya kiingereza hapa Zanzibar .
Alisema vipindi hivyo vimekuja kwa wakati muafaka kwani sera mpya ya elimu inasisitiza umuhimu wa kufundisha kiingereza katika skuli za Zanzibar na kuwataka walimu hao wawe wafuatilia vyema programmu hiyo ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwao.
“Nawaomba sana walimu wasisingizie hawana muda wa kusikiliza vipindi hivi, vimeletwa kwa faida yao na naamini vitawasaidia sana na kuwajengea uwezo wa kufundisha”, alisema Kamishna huyo.
Kamishna huyo alisema lugha ya kiingereza ni muhimu sana kwa kuwa lugha ya kiingereza inatumika sehemu mbali mbali katika masomo hivyo kila mwalimu awe anajifunza lugha ili aweze kuongeza ufanisi katika elimu yake kwani wakati mwengine usipofahamu lugha unaweza kukosa fursa muhimu katika kazi zao.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Sauti ya Tanzania Zanzibar, Hassan Vuai alisema vipindi hivyo vitarushwa kuanzia Jumatano ya Februari 9 majira ya saa 11:30 na kurejewa Jumapili saa 1:30 usiku katika idhaa hizo.
Alisema vipindi hivyo vya robo saa vitadumu kwa miezi mitatu ambapo vitatangazwa kupitia mawimbi ya FM 90.5, masafa ya kati 585 (MW) na masafa mafupi 25 na 45 (SW) na kuwataka walimu na wananchi kwa ujumla waweze kusikiliza kwani kuna manufaa makubwa na faida kwa watakaosikiliza katika kujifunza lugha hiyo

No comments:

Post a Comment