Saturday, 26 February 2011

Taasisi binafsi zaongoza kwa misaada Gongo la Mboto  


Waandishi Wetu
TAASISI binafsi zinaongoza kwa utoaji wa misaada kwa waathirika wa milipuko ya mabomu Gongo la Mboto ukilinganisha na zile za umma.
  Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa na Kaimu Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Saidi Sadiki, umebaini kwamba Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ndiyo taasisi pekee ya umma iliyojitokeza na kuwasaidia waathirika.   Vyombo binafsi vilivyotajwa kutoa misaada  ni Vodacom,Tigo, Barclays, Wama Saccoss, Al-Muntazir, na Chama cha Waimbaji Muziki wa Injili Tanzania (Chamwita).
  Vingine binafsi ni Dar es Salaam Independent School (DIS), NBC, Baraza Kuu la Waisilamu Tanzania (Bakwata), Ecobank, klabu za Yanga na Simba.   Vikundi vingine binafsi ni Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wake za wanajeshi na vyama vya siasa vya   Chadema na CUF.  "Ni kweli taasisi, kampuni binafsi zimekuwa zikijitokeza kwa wingi kuchangia waathirika," alisema Sadiki akihimiza watu wote wenye uwezo kuweka nguvu pamoja katika kutoa misaada.   Wakati huo huo mabomu 2,400 yaliyotawanyika katika makazi ya watu yameokotwa hadi jana mchana.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Luteni Kanali Kapambala Mgawe aliwaambia waandishi wa habari kuwa kazi hiyo bado haijakamilika.  Alisema badi kikosi maalumu cha jeshi kinaendelea kuokota mabaki hayo ya mabomu lakini wakawaomba wananchi wasiyaguse.  Luteni Kanali Mgawe alisema wanachoweza kufanya wananchi ni kutoa tu taarifa kwa vyombo vya usalama ili yaondolewe kitaalamu bila kusababisha madhara.  Alisema jeshi hilo limepata taarifa kuwa baadhi ya wananchi wanayatumia mabomu hayo kama vyuma chakavu bila kujali kwamba ni hatari na yanaweza kulipuka na kusababisha madhara mengine kwa binadamu.
“Ni vyema wananchi wakatoa taarifa kwa jeshi kwani ni hatari kuokota mabomu haya. Wengine wanashinda kuelewa na kuyafanya vyuma chakavu wanaweza kusabisha madhara makubwa,” alisema Mgawe.   Wakati huohuo mwananchi ilishuhudia  wananchi na vikundi mbalimbali bado wakiendelea  kumiminika  kutoa misaada kwa waathirika wa mabomu hayo yaliyolipuka katika kambi ya jeshi Gongo la Mboto, Februari 16, mwaka huu. 
Baadhi ya misaada iliyopokelewa jana ni magodoro, viatu, shuka, sabuni, vyombo vya kulia, maji, unga, maharagwe, mafuta na chumvi, vyote vikiwa na thamani ya Sh 4.4 milioni.  Baadhi ya vikundi vilivyotoa misaada hiyo ni Benki ya Afrika (BOA), Ecobank, Positive Thinker Tanzania (PTT) na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ya Kanisa Katoliki, jijini Dar es Salaam.  Habari hii imeandikwa na Zaina Malongo, Mwanaisha Swedi na Eunice Muhandia MWISHO.

No comments:

Post a Comment