Saturday, 26 February 2011

Mtandao mpya wa urais CCM waundwa 
ccm flag

ccm

Mwandishi Wetu
MBIO za kuwania urais mwaka 2015. ndani ya CCM zinazidi kushika kasi, huku mtandao mpya ukiundwa na tyari umeanza kuweka mikakati kushinda ndani ya chama.

Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka kwa makada wa chama hicho zinaeleza kuwa, kada mmoja anayeitaka nafasi hiyo (jina tunalo) hivi karibuni alikusanya baadhi wapambe wake jijini Dar es Salaam kupanga mikakati ya kuuimarisha mtandao atakaoutumia kushinda nafasi ndani ya chama.

Habari za uhakika zinasema mtandao wa kada huyo wa CCM unaojumuisha baadhi ya wenyeviti wa chama wa mikoa, wabunge na wafanyabiashara wiki iliyopita na wiki hii  ulikutana jijini Dar es Salaam kuweka mikakati ya kujimarisha ndani ya chama kabla ya chaguzi zake.

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, alipoulizwa juu ya kuwepo kwa mbio hizo mapema kiasi hiki, alisema hana taarifa za kuwepo makundi yanatumiwa na makada wa chama hicho kusaka urais.

Hata hivyo, mmoja wa watu walio ndani ya mtandao huo alisema uamuzi huo wa kuanza kujiimarisha ndani ya chama, unatokana na kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete alipohutubia kilele cha miaka 34 ya CCM mjini Dodoma Februari 5, mwaka huu kwamba chama hicho kinatakiwa kufumuliwa na kuundwa upya kulingana na mazingira ya sasa.

Katika mkutano huo Rais Kikwete alisema chama hicho kinakabiliwa na matatizo makubwa kwa sasa, hivyo kinahitaji kufanya mageuzi makubwa vinginevyo kitakufa kifo cha mende.

Alisema kuwa chama hicho kimeishiwa fedha na kwamba yako maeneo ambayo yanasababishwa na kukosa uaminifu na viongozi wasiokuwa wabunifu.
Rais Kikwete alisema mabadiliko makubwa ndani ya chama hicho kikongwe nchini, yataanza mara moja mwishoni mwa mwezi ujao (Machi) Kamati Kuu (CC), itakapokutana, kupokea tathmini ya Uchaguzi Mkuu uliopita.

Hatua hiyo ya Rais Kikwete imetafsiriwa na baadhi ya makada kwamba huenda atafanya mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya chama hivyo kada huyo mkongwe ameandaa mtandao utakomwezesha kuwa na nguvu ndani ya chama.

"Ingawa tayari Bunge tumelikamata, lakini hatuna uhakika na Rais Kikwete kama anaweza kuteua watu wetu kuingia katika Sekretarieti ya chama, hivyo lazima tuweke mikakati, " alisema mtoa habari wetu.

Kambi hiyo pia imejipanga kuhakikisha kuwa inaweka watu wake katika nyadhifa za juu za uongozi wa chama na kwamba, watakwama, basi vikao vya NEC vinavyokuja vitawaka moto.

Chanzo kingine kutoka ndani ya CCM kinaeleza kuwa, mgawanyiko wa makundi ya urais ndani ya chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, unazidi kukitafuna chama.

Chanzo hicho kinaeleza kuwa hali ilivyo sasa ndani ya CCM inasababisha hata watumishi wa chama kufanyakazi kwa masilahi makundi yao hivyo kukifanya kuendelea kukosa mwelekeo.

Habari za uhakika zinasema kwamba tayari mtandao huo umeshamwandaa mtu wanayetaka ashike nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM.

Gazeti hili limedokezwa kuwa mteule huyo wa mtandao huo, sasa ni balozi wa Tanzania katika nchi moja iliyopo ulaya ambaye aliwahi kushika wadhifa mkubwa katika chama hicho siku za nyuma.

Kwa mujibu wa habari hizo, shinikizo la kutaka Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba kuondoka katika wadhifa huo limekuwa kubwa na hata kundi ambalo lililokuwa nyuma yake, limeamua kumwomba astaafu wadhifa huo mapema, ili washinikize achaguliwe mtu wao.

"Makamba amekitumikia chama kwa muda mrefu, lakini kwa sababu kuna shinikizo kubwa juu yake ndani ya chama, tutapendekeza apumzishwe, halafu tufanye kila linalowezekana mtu wetu achaguliwe kuchukua nafasi hiyo," alisema mtoa habari huyo ambaye ni kada wa chama aliyeko kwenye mtandao huo.

Kwa mujibu wa mtioa habari wetu, mtandao huo unataka hata baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti ya chama ambao hawamuungi mkono mgombea wao wang'oke ili wafanye ushawishi kwa Mwenyekiti Rais Kikwete kuwateua watu wao.

Wajumbe wa Sekretarieti waliopo hivi sasa ni Katibu Mkuu, Yusuf Makamba, Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu, George Mkuchika, Waziri wa Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mweka Hazina, Amos Makalla, Hamida Kidawa Salehe, kutoka Zanzibar. 

Hata hivyo, habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa mtandao huo umechochoa watu wengine kuunda makundi ya kuwania urais huku watu watatu wakitajwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo nyeti na ya juu nchini.

Wanaotajwa na wanaCCM kuwa wanaonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ni Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Hata hivyo, kasi hiyo ya kuwania urais mwaka 2015 ndani ya CCM inaelezwa kuwa imewagawa mawaziri hasa vijana ambao wameelezwa kuangukia katika makundi hayo jambo linaloelezwa kushusha ufanisi katika utendaji ndani ya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Mawaziri hao vijana wanadaiwa kuelekeza nguvu na mikakati yao kwenye makundi hayo, wakianza kufikiria na kujipanga ili kupata makundi yenye nguvu za kutwaa urais kwa matarajio ya wao kuwemo katika serikali hiyo ya mwaka 2015.

Akizungumza na Mwananchi Jumapili mjini Dodoma hivi karibuni mmoja wa wanaCCM vijana ambaye pia ni mbunge alisema kuwa kuwepo kwa mitandao inayowania urais mwaka 2015 inashusha ufanisi na kuongeza hatari ya kumhujumu Rais aliye madarakani na serikali yake.

"Ndiyo nimesikia, najua kuwepo kwa watu wanaosaka urais mwaka 2015, lakini labda niseme pamoja na ukweli kuwa Kikwete anamaliza muda wake wa miaka 10 ya utawala, jambo hilo ni hatari kufanyika kwa sasa," alisema.

Aliongeza: "Pamoja na ubaya uliopo, we acha wafanye, lakini hatari yake ni hiyo pia watayumbisha chama, lakini pia kwao hawataona vibaya kumhujumu rais aliye madarakani ili wafanikishe malengo yao, hii ndiyo hatari yenyewe kwani nchi inaweza kwenda pabaya."

Mbunge huyo kijana alisema kwa maoni yake na anavyoshauri watu hao bora wakaimarisha kwanza chama chao ambacho alisema kina majeruhi ya uchaguzi mkuu na changamoto mbalimbali zinazotakiwa kufanyiwa kazi ili kiweze kubaki madarakani kwa uhakika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Vuguvugu hilo linakikumba chama hicho wakati serkali ya CCM chini ya Rais Kikwete ikabiliwa na changamoto nyingi kubwa zaidi ikiwa ni kupanda kwa gharama za maisha kunakosabishwa na mfumuko wa bei.

Mbali na uchumi wa nchi kushamiri kwa mgawo wa umeme kumeongeza ugumu wa maisha na kuteremsha uzalishaji katika sketa zote, ikiwemo sekta isiyorasmi ambayo kwa sasa ndiyo kimbilio la wengi baada ya serikali na taasisi zake kushindwa kutoa ajira kwa wananchi wake na hasa vijana.

Taarifa za uchumi zinaonyesha kuwa kadirio la Sh10 bilioni zinaweza kuwa zinapotea kila siku kutokana na mgao wa umeme na matatizo mengine yanayodumaza uchumi wa Tanzania na kuifanya serikali kuwa katika wakati mgumu.

No comments:

Post a Comment