Sunday, 6 February 2011

Serikali Yaagiza Mashirika yote Kulipa Kodi



NaSalma Said Zbar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeahidi kuandaa sheria na kupitia upya muundo wa mashirika ya umma kwa kupunguza wafanyakazi wake kwa mashirika ambayo yatashindwa kujiendesha kibiashara na kutakiwa mshirika yote kuanzia sasa kulipa kodi serikalini na kuachana na tabia ya kuomba misamaha ya kodi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango, Omar Yussuf Mzee alipokuwa akiongea na wakurugenzi na watendaji wakuu wa mashirika ofisini kwake Vuga jana ambapo alisema baadhi ya mashirika yamekuwa ni mzigo kwa serikali kutokana na kushindwa kuyaendeleza kibiashara.
Akiongea na mashirika manane ya serikali alisema wingi wa wafanyakazi ni miongoni mwa matatizo ambayo hayahitaji kufanyiwa kazi ikiwa pamoja na kuondokana na mfumo wa kuyaendesha mashirika kama idara za serikali ambapo alisema kwa mujibu wa sheria mashirika yapo huru katika kujiendesha wenyewe kibiashara.
“Tabia hii iwache ya kuendesha mashirika kama idara za serikali imekuwa mkurugenzi akihitaji vifaa vya ofisi mbio anakimbilia serikalini kwani mashirika haya yafanye hivi wakati mnajiendesha wenyewe” alihoji Mzee.
Alisema baadhi ya mashirika yamekuwa yakikwepa kulipa kodi serikalini jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuzorotesha mashirika hayo na kutojitutumua katika kutekeleza majukumu yao na kukosekana ufanisi kwa kuwa kila kitu kinatoka serikalini katika malipo.
“Mashirika yote kuanzia sasa yatalipa kodi serikalini na hivyo ndivyo sheria inavyosema ….hatutaki shirika letu hata moja life mashirika tulionayo hivi sasa ni manane hayo mengine yote yameshakufa kwa hivyo tunasema tunataka tujiendeshe kibiashara zaidi” alisema Mzee.
Alisema baadhi ya mashirika yamekufa kabisa na mengine yapo hoi kutokana na tabia ya kutojituma kwa maafisa wa mashirika hayo iliyojengeka ikiwemo suala la kuitegemea kwa kila jambo serikali.
Aidha ametayaka alitoa wito kwa mashirika hayo kuanzia sasa kujitegemea wenyewe na kulipa kodi serikalini badala ya kusamehewa kodi kwa kuwa na kuoa wito kwa wakurugenzi kujitutumua ili wayaendeshe Serikali haiwezi tena kubeba Mashirika ambayo yapo katika hali mbaya huku yakikabiliwa na matatizo ya uongozi.
Waziri huyo ameshangazwa na mashirika yenye uwezo mkubwa wa kufanya biashara lakini yapo katika hali mbaya ya kifedha huku akitoa mfano wa shirika la umeme ambalo limefikia hatua ya kumalizika kutokana na hali mbaya walionayo na kujiendesha kwa kukosa fadia.
“Hili shirika la umeme linahitaji marekebisho makubwa kwa kweli….naona lipo katika chumba cha wagonjwa mahututi ICU….lakini tatizo lake kubwa sio kufanya biashara ni uongozi na kuwa na wafanyakazi wengi na tatizo hili tunataka lipatiwe tiba kwa haraka kwa sababu hatuwezi kuona mshirika yetu yanakufa wakati yanaweza kujiendesha”alisema Mzee.
Alisema Mashirika ya Serikali yapo huru kufanya shunguli zao za Kibiashara na hayana sababu tena ya kuomba ruzuku kutoka Serikalini hivyo aliwataka watendaji wakiwemo wakurugenzi, bodi na wafanyakazi kujituma ili kuhakikisha mashrika hayo yanajiendesha kibiashara.
“Mashirika yetu yangeweza ku survive lakini tatizo liliopo ni uongozi, bodi na wafanyakazi wenyewe ndio wanaouwa mashirika haya yasiweze kufnaikiwa sasa hilo hatulitaki tena lazima kufanyike marekebisho ya kupunguzwa kazi wafanyakazi wasiokuwa na taaluma wengine watafutiwe sehemu nyengine maana hawezekani shirika dogo liwe na wafanyakazi mia tano ,….hiyo haiwezekani” alisema waziri huyo.
Kati ya mashirika yote manane viongozi wake waliokuwepo katika kikao hicho ni shirike moja pekee ndilo lililojieleza kuwa lipo katika hali ya afadhali kulingana na mashirika mengine ambapo mengi yao yamesema yapo katika hali mbaya kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo wingi wa wafanyakazi, kukosa mitaji ya kujiendesha, uhaba wa vifaa vya kufanyika kazi, ukosefu wa watendaji wazuri wenye ujuzi na kukabiliwa na madeni zikiwemo taasisi za serikali.
Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ndio pekee iliyoweza kujiendesha kwa miguu yake ambapo kwa mujibu wa Meneja wake Juma Amour Mohammed alisema kwamba jambo la mwanzo lililowapa mafanikio ni kupunguza idadi ya wafanyakazikatika benki hiyo, na mnamo mwaka 2000 benki ilikuwa na shilingi billioni 6 ambapo mwaka 2006 ilipata billioni 12.5 na sasa imefikia billioni 142 ambapo benki hiyo inataka kufungua matawi mengine nchini.
Meneja huyo amesema kwamba hivi sasa Benki inakabiliwa na ushindani mkubwa wa kiwango cha mtaji kinachotakiwa na Benki kuu ifikapo mwaka 2013 ambacho ni shilingi billioni 15 ambapo changamoto hiyo ndio inayohitaji kufanyika wazi kwa sasa.
Wakurugenzi waliohudhuria katika kikao hicho ni kutoka shirika la Bandari, Umeme, Utalii, Meli, Magari, ZSTC na PBZ na Bima ambapo kwa pamoja walisema wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika utekelezaji wa majukumu yao na kuiomba serikali iyatupie macho mashirika yake ili yaweze kujiendesha kibiashara.
Walisema mashirika hayo yanakabiliwa na ugumu wa kufanya biashara kufuatia utandawazi uliopo sasa na ushindani wa kibiashara uliopo katika soko huria jambo ambalo Zanzibar bado ipo nyuma katika utekelezaji wa majukumu hasa katika sual la kujiendesha kibiashara.

No comments:

Post a Comment