Tuesday, 1 February 2011

Risasi zarindima Muhimbili

 
Wanafunzi wa Udaktari wa kinywa na meno wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba za Binadamu cha Muhimbili MUHAS jijini Dar es Salaam, waligoma kuingia madarasani na kusababisha vurugu.

Wanafunzi wa Udaktari wa kinywa na meno wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tiba za Binadamu cha Muhimbili MUHAS jijini Dar es Salaam, jana waligoma kuingia madarasani na kusababisha vurugu zilizowalazimisha polisi kufyatua risasi.
Wanafunzi hao waligoma ili kuushinikiza uongozi wa chuo hicho kuondoa utaratibu mpya uliowekwa wa kurudia mitihani.
Polisi waliokuwa eneo hilo wakilinda usalama ilibidi kuingilia kati na kufyatua risasi za moto kwa ajili kumuokoa mpiga picha wa chuo hicho ambaye alikuwa akishikiliwa na kupigwa kupigwa wanafunzi hao.
Polisi hao alifyatua hewani risasi tatu za moto ili kumuokoa mpiga picha huyo alitefahamika kwa jina la Anede Damas (54), baada ya wanafunzi hao kumkamata na kuanza kumpiga.
Wanafunzi hao walichukia kupigwa picha wakati walipovamia ofisi ya Makamu Mkuu wa chuo kwa ajili ya kumshinikiza awasikilize matatizo yao.
Wanafunzi hao walianza mgomo majira ya saa 3:00 asubuhi ambapo kundi la wanafunzi lilikusanyika katika jengo la Shule ya Matibabu ya Kinywa na Meno na kuamua kutoingia madarasani hadi hapo uongozi wa utakaporekebisha utaratibu huo.
Akizungumza wakati wa kikao kati ya wanafunzi hao na uongozi wa chuo hicho, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa MUHAS, Fidelis Bogias, alisema wanacholalamikia ni hatua ya uongozi wa chuo kubadilisha utaratibu wa kurudia mitihani bila ya kuwashirikisha.
Alisema utaratibu uliotolewa mwaka huu, unaeleza kuwa mwanafunzi atakayefeli mtihadi itambidi kusubiri hadi miaka mitano ndipo afanye mitihani ya marudio.
Alisema awali wanafunzi walikuwa wakifanya mitihani kipindi cha likizo, kitu ambacho kiliwasaidia wanafunzi kumaliza chuo kwa miaka mitano kama inavyotakiwa.
Kwa mujibu wa Bogias, chini ya utaratibu mpya mwanafunzi itambidi kutumia miaka saba au minane mpaka kuhitimu, hali itakayopelekea wengi wao kushindwa kuendelea na masomo.
Bogias alisema uongozi wa chuo hicho ulifanya ujanja wakati wa kubadilisha kipengele hicho, ambapo ndani ya miaka mitatu kilikuwa kikibadilishwa taratibu na kufikia hali ya sasa inayolalamikiwa.
Kipengele cha utaratibu tunacholalamikiwa kimeanza kubadilishwa taratibu na vikao vya Seneti, lakini tulipolalamika hakuna mtu aliyeweza kutusikiliza na badala yake kila kiongozi anasema wao hawawezi kubadilisha hadi kikao kingine cha Seneti kitakapokaa,” alisema Bogias.
Bogias alieleza kitu kingine ambacho wanafunzi hao hawajaridhishwa nacho ni hatua ya Chuo kuwafukuza wanafunzi tisa kutokana na kukosa karo na kufafanua kuwa waliutaka uongozi kuwarudisha ili waendelee na masomo.
Alimtaka, Makamu wa Chuo hicho, Profesa Kisali Palangyo, kuingilia kati suala hilo kwa kuitisha haraka kikao cha Seneti ili kutengua utaratibu huo kwa ajili ya manufaa ya chuo hicho.
Hata hivyo, Prefesa Palangyo wakati akijibu hoja hizo, aliwasihi wanafunzi hao kurudi madarasani wakati uongozi wa Chuo unaangalia namna kuangalia utaratibu huo kwa maelezo kuwa suala hilo ni la kitaaluma zaidi.
Profea Palangyo alisema kuwa kuhusu suala la wanafunzi waliofukuzwa, uongozi huo hauwezi kulaumiwa kutokana na wanachuo hao kuonyesha nidhamu mbaya baada ya kukataa kudahiliwa na wengine kutolipa karo ya miaka ya nyuma bila sababu za msingi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Faustine Shilogile, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi iliwabidi kutumia risasi kwa ajili kumukoa mtu huyo kutoka mikononi mwa wanafunzi.
Polisi walikuwa hawana njia ya kumuokoa yule mpiga picha, walifyatua risasi hewani ambayo haina madhara kwa ajili ya kuwaondoa wanafunzi wale wasimuumize,” alisema Shilogile.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment