Wednesday, 2 February 2011

Mashtaka 85 kwa kigogo wa Tanesco

 
ATUHUMIWA KUIBA, KUHUJUMU UCHUMI
Tausi Ally
MHASIBU wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),  Lilian Chengula (42) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka 85 ya wizi wa zaidi ya Sh1.3 bilioni na uhujumu uchumi.Akisoma hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi Mustapha Siyani, Wakili wa Serikali, Zuber Mkakatu alidai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 84 ya wizi wakati akiwa mtumishi wa umma.

Pia Chengula anakabiliwa na shtaka moja la uhujumu uchumi kwa kuisababishia mamlaka iliyowekwa kisheria, hasara ya zaidi ya Sh1.3 bilioni. Chengula alirejeshwa rumande hadi kesho Februari 3,  mwaka huu, wakati Hakimu Siyani atakapotoa uamuzi iwapo apewe dhamana au la.

Mawakili wa Lilian, John Lawrance na Matongo waliiomba mahakama impatie dhamana mteja wao kwa sababu makosa yote yanayomkabili yanadhaminika.

Ombi hilo lilipingwa na wakili wa Serikali, Mkakatu aliyedai mahakamani hapo kuwa shtaka la 85 la uhujumu uchumi linalomkabili Chegula haliwezi kupatiwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na kwamba wenye uwezo wa kutoa dhamana kwa kosa hilo ni Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Matongo aliiomba mahakama itupilie mbali hoja iliyotolewa na upande wa mashtaka  kwa madai kuwa imepitwa na wakati, hivyo hakimu Siyani kuahirisha kesi hiyo hadi kesho.

Mapema wakili wa Serikali alidai kuwa mshtakiwa Chengula alifanya makosa hayo kati ya mwezi Septemba, mwaka  2009 na mwezi Septemba, mwaka  2010.

Mkakatu alidai kuwa Chengula ambaye ni mwajiriwa wa Tanesco akiwa mhasibu kwa nia ya kudanganya, alighushi hati mbalimbali za malipo na kujipatia fedha hizo ambazo ni mali ya mwajiri wake.

Katika shtaka la uhujumu uchumi, Chengula anadaiwa kulisababishia Tanesco hasara ya Sh 1,312,717,717.70.

Baada ya Wakili wa Serikali kusoma shtaka la uhujumu uchumi, hakimu Siyani aliuhoji upande wa mashtaka kama una kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kinachowaruhusu kufanya hivyo.

Wakili huyo wa Serikali alisema upelelezi wa makosa 84 ya wizi yanayomkabili Chengula bado haujakamilika na kwamba bado wanasubiri kibali kutoka kwa DPP  kinachohusiana na kosa la 85 la uhujumu uchumi.

Kukamatwa kwake………

Habari za kukamatwa kwa Chengula ziliandikwa na gazeti hili katika toleo lake la Jumatatu wiki hii, huku Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, akithibitisha kukamatwa kwa mhasibu huyo.

Mhando alisema ofisa huyo anatuhumiwa kutenda makosa kwa kushirikiana na wafanyabiashara mbalimbali waliokuwa wakinunua umeme katika ofisi hizo.
“Ni kweli huyo mtu tunaye na anatuhumiwa kushirikiana na ma-vendor wetu (wauzaji wa rejareja). Inaonekana alikuwa akiwauzia umeme mwingi kuliko umeme aliotakiwa kuutoa kulingana na gharama walizolipia,” alisema Mhando.
Alisema suala hilo lilibainika baada ya kufanyika kwa ukaguzi wa ndani ambao uliwezesha  kugundulika upotevu wa kiasi hicho kikubwa cha pesa na kwamba baada ya kubaini tatizo hilo hatua zilizochukuliwa ni kumhamishia afisa huyo makao makuu ili kupisha uchunguzi.
“Kwa kawaida huwezi kumfukuza tu mtu kazi kienyeji, kwa hiyo kwanza “tulim-charge” tukamtaka aandike maelezo ni kwa nini asifukuzwe kazi ,” alisema Mhando.
Alisema  baada ya timu iliyoundwa kushughulikia suala hiyo kukaa na kupitia maelezo yake ilibainika kuwa ofisa huyo ana hatia na kwamba hatua iliyokuliwa ni kukatisha mkataba wale wa ajira.
“Lakini kwa kuwa hizo ni pesa nyingi na ni za umma tukaona ku-terminate (kukatisha) tu mkataba wake haitoshi hivyo wakaguzi wakaamua kumfikisha polisi kwa hatua zaidi za kisheria;“Kwa hiyo baada tu ya kukatisha mkataba wake na askari wakamkamata hapo hapo ofisini,” alisema Mhando.
Kwa mujibu wa habari kutoka kwa vyanzo hivyo ofisa huyo alitiwa mbaroni Ijumaa iliyopita akiwa ofisini kwake makao makuu ya Tanesco ambako alihamishiwa wakati uchunguzi wa tuhuma zake ukiendelea .“Mpaka ninavyokwambia hivi sasa yuko Central (Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam), kilidokeza chanzo chetu na kuongeza kuwa huenda leo ofisa huyo akapandishwa kizimbani kwa tuhuma hizo zinazomkabili,".
Habari zaidi zilidai kuwa polisi wanaendelea kuwasaka washirika wa Chengula katika tuhuma hizo ili nao waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Wizi kupitia mashine za Luku
Septemba 7, mwaka jana
Tanesco lilitanga kubaini kuwepo kwa mtandao wa wezi wa umeme kupitia mashine za Luku na vituo feki vya kuuzia umeme huo.

Kufuatia hali hiyo, shirika hilo lilianzisha operesheni endelevu ya kuwasaka wahusika wakiwemo watumishi wake wanaohisiwa kuhusika.

Katika siku ya kwanza ya utekelezaji wa operesheni mashine 7 kati 11 za Luku ambazo awali zilibainika kuwa na tatizo, zilihakikiwa katika maeneo ya Mwenge na Kariakoo zilihusishwa na wizi wa umeme.

Msemaji wa Tanesco, Badra Masoud alisema kupitia kitengo maalumu cha Luku kilichoanzishwa na shirika hilo walikuwa wakifuatilia taarifa za kuwepo kwa hujuma katika shirika hilo kupitia Luku na mita za kawaida, zinayofanywa na baadhi ya wafanyakazi halali wa shirika hilo.

No comments:

Post a Comment