Wednesday, 2 February 2011

Kupanda kwa gharama za umeme

*Bidhaa zapaa
*Sukari, mafuta, mchele bei juu



Soko la Kariakoo





Na Waandishi Wetu, jijini
ATHARI za kupanda kwa gharama za umeme kuanzia Januari Mosi mwaka huu,zimeanza kujitokeza ambapo hivi sasa kila kona wananchi wamejikuta wakibaki namanung'uniko kutokana na mfumko wa bei mpya.

Uchunguzi uliofanywa na Dar Leo katika maeneo mbalimbali ya jiji umebaini kupanda kwa gharama za bidhaa hizo na kusababisha wananchi kuendelea kuishi kwa taabu.

Dar Leo imebaini kuwa, baadhi ya wafanyabiashara wamepandisha bidhaa zao kwa kisingizio cha gharama za umeme huku wengine wakisingizia gharama za usafiri.

Waandishi wa habari hizi wamebaini kuwa, sukari iliyokuwa ikiuzwa kati ya sh.1400 - 1500 hivi sasa inauzwa sh.1600- 1800- 2000.Pia mafuta ya kupikia ya lita moja yaliyokuwa yakiuzwa sh.2500 hivi sasa sh. 3000 hadi 3500, na yale ya lita tatu yaliyokuwa yakiuzwa sh.6000 hivi sasa yanauzwa sh.8000 ambapo ndoo moja ndogo iliyokuwa ikiuzwa sh.22,000 hivi sasa ni sh.28,000.

Kupanda kwa gharama za umeme pia kumeathiri utendaji kazi kwa wajasiriamali wa bidhaa mbalimbali na wale wa saluni ambapo wamelazimika kutumia jenereta linalotumia mafuta mengi na kusababisha kupanda kwa gharama za biashara zao.Kwa upande wa saluni za kike ambako nywele zilikuwa zikitengenezwa kwa gharama ya sh.1500 - 2000 hivi sasa wanatoza sh. 2,000 mpaka 2,500 kwa kuosha na kuseti.

Kwa zile saluni za kiume kunyoa nywele watoto wadogo ilikuwa sh.700 hivi sasa ni sh.1,000 ambapo kwa watu wazima ni sh.1,500 hadi 2,000.

Kutokana na hali hiyo wananchi mbalimbali waliongea na Dar Leo wameiomba Serikali kufanya jitihada za kusimamia upandishaji kiholela wa bidhaa na gharama za vitu mbalimbali kwakuwa zimekuwa zikiwaumiza wananchi hasa wale wa kipato cha chini.

Wamesema kuwa, kwakuwa wafanyabiashara wengi wamekuwa wakitoa kisingizio cha kupanda kwa gharama za umeme ni vyema serikali ikalitupia macho suala hilo na kulifanyia marekebisho.

" Hawa wafanyabiashara ni watu wanaofuatana kama kinyonga wakianza hawa wa vinywaji baridi, saluni, kusingizia umeme basi kila mmoja atapandisha bidhaa kwa kisingizo kingine ili mradi tu wajipatie faida mara dufu,"amesema Rose James mkazi wa Ulongoni, Ukonga.

Amesema kuwa, endapo serikali haiwezi kutoa haraka tamko la udhibiti wa upandaji wa bidhaa hizi wananchi watazidi kuumia na hata wengine kushindwa kumudu gharama za mlo mmoja.

Januari Mosi mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), lilipandisha gharama za umeme kwa kile walichodai kunatokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji hali ambayo ilipokelewa kwa simanzi na wananchi.

Habari hii imeandaliwa na Christina Gauluhanga, Stella Aron na Heri Shaaban.
 

No comments:

Post a Comment